Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda: maisha, utume na changamoto zake

Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda wakati wa hija yao ya kitume mjini Vatican kwa mwaka 2018.

19/06/2018 07:14

Kanisa Katoliki nchini Uganda limegawanyika katika majimbo makuu manne, majimbo ya kawaida kumi na tano na jimbo moja ni la kijeshi. Askofu mkuu John Baptist Odama ndiye Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda. Mashahidi wa Uganda waliotangazwa kuwa wenyeheri na Papa Benedikto XV kunako tarehe 6 Juni 1920 na hatimaye, kutangazwa kuwa Watakatifu na Mwenyeheri Paulo VI tarehe 8 Oktoba 1964 ni utambulisho wa ushuhuda wa imani ya watu wa Mungu nchini Uganda. Leo hii Madhabahu ya Namgongo, yamekuwa ni kivutio kikuu cha imani kutoka kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Uganda.

Uganda inakumbukwa sana kuwa ni mahali palipozaliwa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM. Hiki kikawa ni chombo kinachoyaunganisha Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar. Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Uganda hasa katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya jamii. Kanisa pia limeendelea kuwa ni kikolezo cha mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa ikizingatiwa kwamba, Uganda ni nchi ambayo kwa miaka mingi sasa inakabiliana na vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Kati ya changamoto kubwa zinazolikabili Kanisa Katoliki nchini Uganda ni majadiliano ya kidini, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na ongezeko kubwa la waamini wenye misimamo mikali ya kidini, wanaotishia usalama, amani na haki msingi za binadamu. Ili kukabiliana na changamoto hii, Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda lilipendekeza kutolewe elimu na majiundo makini kwa vijana; kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na kwamba, familia inajengwa kati ya Bwana na Bibi na wala si vinginevyo! Hii inatokana na ukweli kwamba, nchini Uganda ndoa za watu wa jinsia moja zilianza kujitokeza kama sehemu ya haki msingi za binadamu. Lakini watu wakakumbushwa kuhusu umuhimu wa utu na heshima ya binadamu kadiri ya mpango wa Mungu.

Mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI ni changamoto pevu nchini Uganda na kwamba, maambukizi mapya yanaendelea kupungua kila mwaka, hasa kutokana na mpango mkakati wa kuzuia maambukizi kutoka kwa Mama mwenye virusi vya Ukimwi kwenda kwa mtoto mchanga. Kanisa linaitaka familia ya Mungu nchini Uganda, kuwa makini sana na ugonjwa wa UKIMWI, kwani hauna dawa wala kinga; hauchagui wala haubagui. Kanisa Katoliki nchini Uganda limekuwa pia mstari wa mbele dhidi ya adhabu ya kifo kwa kusema kwamba, adhabu hii imepitwa na wakati.

Wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum nchini Uganda ni changamoto kubwa inayofanyiwa kazi na Kanisa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali. Jeshi la waasi wa  Uganda “Lord’s Resistance Army” chini ya Joseph Kony, limekuwa ni chanzo cha: utekaji nyara, mateso na dhuluma kwa watu wasiokuwa na hatia. Wakimbizi na wahamiaji wengi wanaopewa hifadhi nchini Uganda ni wale wanaotoka Sudan, DRC pamoja na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Kuna watu ambao wanaishi kwenye kambi za wakimbizi kwa zaidi ya miaka 20 sasa.  Upandaji wa miti ni changamoto inayovaliwa njuga na Kanisa nchini Uganda, ili kudumisha mazingira nyumba ya wote.

Askofu mkuu Cyprian Lwanga wa Jimbo kuu la Kampala anasema, kwa miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na uchafuzi mkubwa wa mazingira na matokeo yake ni athari za mabadiliko ya tabianchi. Maaskofu wanaendelea kuwekeza katika njia za mawasiliano ili kukuza na kudumisha demokrasia ya kweli kama sehemu ya changamoto ya ujenzi wa umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa. Kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa mawasiliano halisi yanafumbatwa katika: ukweli, uhuru, haki na mshikamano. Hii ni misingi ambayo inaweza kusaidia ujenzi wa jamii mpya inayozingatia pia demokrasia na utawala wa sheria. Njia mpya za mawasiliano zitumike kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, changamoto kubwa inayotolewa na Askofu Giuseppe Franzelli wa Jimbo Katoliki Lira.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda linasikitika kusema, vipigo vya akina mama majumbani ni janga kubwa nchini Uganda. Maaskofu wanawataka wananchi wa Uganda kuheshimu haki na utu wa wanawake, kwani mwanamke hapigwi kwa ngumi na mateke, bali kwa kipande cha kanga! Katika mwelekeo huu, viongozi wa kidini nchini Uganda, wameungana kwa pamoja ili kukemea ukeketaji wa wanawake kwani hivi ni vitendo vinavyokiuka haki msingi za wanawake na hivyo kuwasababishi madhara makubwa katika maisha yao.

Watoto wanaopelekwa mstari wa mbele kama chambo vitani ni janga kubwa nchini Uganda. Kwa njia ya Radio Wa ya Jimbo Katoliki la Lira, Kaskazini mwa Uganda, Kanisa limefanikiwa kuwarejesha watoto waliokuwa wametekwa na kupelekwa mstari wa mbele. Kimsingi changamoto kubwa nchini Uganda zinazofanyiwa kazi kwa sasa ni haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Nyingine ni wito na maisha ya kipadre na kitawa; ndoa na familia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda linamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko aliyeweza kupamba sherehe za Jubilei ya Miaka 50 ya Mashahidi wa Uganda. Baba Mtakatifu Francisko katika barua aliyoandika kwa ajili ya familia ya Mungu nchini Uganda, aliishukuru kwa moyo wa ukarimu na upendo waliomwonesha alipotembelea nchini Uganda kunako mwaka 2016. Hapa kulikuwepo na ushirikiano wa karibu sana kati ya Serikali na Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Uganda. Ilikuwa ni fursa ya kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene; umoja na mshikamano wa kitaifa nchini Uganda.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!

19/06/2018 07:14