Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Sala ya Malaika wa Bwana

Mwenyeheri Mama Carmen Rendiles Martines, alijisadaka sana!

Mwenyeheri Sr. Carmen Rendìles Martines ni mtawa aliyejisadaka kwa ajili ya huduma kwa Kanisa na jirani zake. - AP

18/06/2018 08:39

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili, tarehe 17 Juni 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, aliwaalika waamini kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyelijalia Kanisa kumpata Mwenyeheri mpya Sr. Carmen Rendìles Martines. Huyu ni mtawa pamoja na wenzake, waliojisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa Mungu na jirani kwenye parokia, maskini na wagonjwa. Kwa maombezi ya Mwenyeheri mpya, Baba Mtakatifu Francisko ameiweka familia ya Mungu nchini Venezuela chini ya maombezi yake.

Kardinali Angelo Amato kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 16 Juni 2018 amemtangaza mtumishi wa Mungu Sr. Carmen Rendìles Martines kuwa Mwenyeheri katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa huko Caracas, nchini Venezuela. Alizaliwa mjini Caracas tarehe 11 Agosti 1903 kutoka katika familia ya wachamungu. Akafanikiwa kuanzisha Shirika la Watawa Watumishi wa Yesu Venezuela na kuwa Mama mkuu wa Shirika hadi tarehe 9 Mei 1977 alipofariki dunia.

Mama Carmen Rendìles Martines kama wengi walivyozoea kumwita, alijiweka wakfu kwa ajili ya huduma kwa Kanisa na jirani zake ili kuwashirikisha huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Alijitahidi kuhakikisha kwamba, anavuka vikwazo na majaribu katika maisha na utume wake, licha ya ulemavu aliokuwa nao! Tangu akiwa bado kijana mbichi alitamani sana kuwa mtawa, kwani aliguswa sana na karama ya mashirika ya kitawa yaliyokuwa yamefika nchini Venezuela kutoka Ufaransa.

Alijiunga na Shirika la Watawa wa Yesu wa Sakramenti kuu na hatimaye, kuweka nadhiri za daima kunako mwaka 1930. Katika maisha na utume wake, alibahatika kuwa ni Mama mlezi wa wanavosi na mkuu wa Jumuiya zilizokuwa zimeanzishwa huko Venezuela na Colombia. Mabadiliko makubwa yaliyoletwa na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ukaliangukia Shirika hili na watawa wake, wakataka kuishi kama waamini walei waliojiweka wakfu kwa Mungu na Kanisa. Mama Carmen Rendìles Martines hakulifurahia wazo hili kwani alitaka kuendelea kuwa mwaminifu kwa karama na mapokeo ya Shirika.

Huku akiwa anaungwa mkono na wakleri pamoja na watawa kunako mwaka 1965 akaomba Vatican kutenganisha watawa waliokuwa wanaoishi huko Amerika ya Kusini na wale waliokuwa wanatoka Ufaransa. Tarehe 25 Mei 1966 likazaliwa Shirika jipya, likiwa na haki za kijimbo na kuitwa Shirika la Watawa Watumishi wa Yesu Venezuela. Katika kipindi cha uongozi wake, Shirika likapanuka na kuenea katika majimbo mbali mbali nchini Venezuela na Colombia. Watawa wake, wakajikita zaidi katika kufundisha katekesi parokiani kwa watoto waliokuwa wanajiandaa kupokea Sakramenti mbali mbali za Kanisa. Walikuwa mstari wa mbele kuwaongoza wasichana waliokuwa kwenye taasisi za elimu na vyuo vikuu katika maisha ya kiroho pamoja na kujisadaka kwa ajili ya maskini na wahitaji zaidi.

Kardinali Angelo Amato anakaza kusema, Venezuela imebarikiwa kuwa na umati mkubwa wa watakatifu, wenyeheri na watumishi wa Mungu. Hawa ni kama Sr. Maria de San Josè (1875-1967), Sr. Candelaria de San Josè. Watumishi wa Mungu ni kama Josè Gregorio Hernàndez: daktari, mwanasayansi na jaalimu wa Chuo kikuu. Wengine ni Wanandoa Aristed Calvan na Adela Abbo Fontana, waliojisadaka kutolea ushuhuda tunu msingi za kiinjili huko Venezuela, nchi iliyobahatika kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili na neema, lakini leo hii, watu wake wamegeuka kuwa ni wakimbizi na wahamiaji; watu wanaoteseka kwa njaa, magonjwa na umaskini kutokana na baadhi ya watu kuelemewa sana na uchu wa mali na madaraka.

Kwa Mama Carmen Rendìles Martines kutangazwa kuwa Mwenyeheri ni kuongeza idadi ya watakatifu nchini Venezuela. Ni mtawa aliyethamini wito na dhamana yake; imani, amana na utajiri wa maisha ya kiroho. Ni Mama aliyetamani utakatifu wa maisha na kuuvalia njuga kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wahitaji zaidi. Alikuwa ni Mama mshauri wa Wakleri, mhudumu makini kwa wasichana. Alionesha upendo kwa watawa wake. Kwa wagonjwa alipenda kuwatembelea, kuwafariji, kuwahudumia na kuwasaidia kadiri alivyoweza. Mama Mama Carmen Rendìles Martines aliyapamba maisha yake kwa kuwaheshimu wengine na kuwa mwepesi kutoa msamaha.

Alipenda watawa wake wawe mstari wa mbele katika kumwilisha mashauri ya Kiinjili kama dira na mwelekeo wa maisha na utume wao. Kuwekwa kwao wakfu; na nadhiri zao, ziwe ni chachu ya kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Alikuwa anawashauri watawa wake kusali kwa ajili ya toba na wongofu wa wadhambi; aliwashauri waamini kupokea Ekaristi Takatifu si kwa mazoea, bali kwa kujiandaa kikamilifu, ili kuweza kuifia dhambi na kufufuka pamoja na Kristo Yesu. Alipenda kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, chemchemi ya neema na baraka. Hii ni changamoto kwa familia ya Mungu kujizatiti kikamilifu katika mchakato wa utakatifu wa maisha unaomwilishwa katika matukio mbali mbali ya maisha ya kila siku!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!

18/06/2018 08:39