Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Papa Francisko: Shuhudieni: Ukuu, uzuri na utakatifu wa familia

Papa Francisko anawataka waamini kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kama mbinu mkakati wa kupambana na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo.

16/06/2018 15:56

Jukwaa la Vyama vya Kifamilia, linalounganisha vyama vya kifamilia vipatavyo 500 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake. Hiki ni chombo muhimu sana kinacho tangaza uzuri wa umoja na nguvu ya kushirikiana kwa pamoja; chemchemi ya furaha kwa mtandao wa kifamilia. Huu ni umoja wa familia unaoendelea kushikamana kwa dhati kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia, changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga kila kukicha! Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 16 Juni 2018 alipokutana na kuzungumza na Jukwaa la Vyama vya Kifamilia. Baba Mtakatifu anakaza kusema, familia ambayo Jukwaa hili linaifanyia kazi ni kiini cha mpango wa Mungu unaojidhihirisha katika historia nzima ya wokovu. Mwenyezi Mungu alimuumba mwanaume na mwanamke, ili waweze kukamilishana na hivyo kushiriki katika kazi ya uumbaji. Kumbe, wazazi wanayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, wanawapatia: elimu, malezi na makuzi bora watoto wao.

Yesu alionesha upendo mkubwa sana kwa watoto, akajenga na kuimarisha uhusiano na Baba yake wa mbinguni; akasimama kidete kulinda na kutetea  tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu. Familia ni mahali pa kwanza kabisa katika hifadhi ya maisha; ni sehemu ya ukarimu na mahali pa kuonjeshana upendo. Familia inayo nafasi kubwa katika wito wa mwanadamu, ni sawa kama dirisha linalofungukia kwenye Fumbo la Mungu ambaye: ni upendo na umoja unaoshuhudiwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Kutokana na ubinafsi pamoja na uchoyo, walimwengu hawaoni tena maana na uzuri wa mafungamano ya kudumu katika maisha ya ndoa na familia; kwa mtu kuwajibika na kujisadaka pamoja na kuchukua majukumu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kutokana na mwelekeo huu potofu, anasema Baba Mtakatifu inakuwa ni vigumu sana kwa baadhi ya watu kutambua tunu msingi za familia na hivyo kuamua kuwajibika kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Katika kipindi cha miaka michache iliyopita, kumekuwepo na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa, lakini familia zimeendelea kuonesha kuwa ni nguvu ya jamii yenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya kila mmoja wao!

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba serikali na taasisi mbali mbali zitatoa kipaumbele cha pekee kwa familia, ili watu waweze kuthubutu kuanzisha familia, zitakazokua na kushikamana, ili kujenga utulivu, utakaowawezesha wazazi kutoa elimu na malezi bora kwa watoto wao; pamoja na kuwahudumia wale wanaoonekana kuwa ni wanyonge zaidi. Ni katika familia, watu wanajifunza kujenga mahusiano ya dhati, hali inayoweza kuendelezwa shuleni, kwenye ulimwengu wa kazi na kwamba, kwa wale wanaoheshimu na kutoa huduma bora nyumbani, wanaweza pia kufanikisha azma hii kwenye jamii na ulimwengu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu anakaza kusema, umefika wakati wa kuimarisha tunu msingi za maisha ya kifamilia, dhamana inayoweza kutekelezwa kwa njia ya majadiliano. Hii ni dhamana ambayo imevaliwa njuga na Jukwaa la Vyama vya Kifamilia katika kipindi cha miaka 25 ya uhai wake; kwa kuanzisha sera na mikakati mbali mbali; kwa kujenga na kuimarisha hali ya kuaminiana kati yao sanjari na kushirikiana na serikali pamoja na taasisi mbali mbali.

Baba Mtakatifu anawataka wajumbe wa Jukwaa hili kuendelea kutangaza na kushuhudia: uzuri, utakatifu na ukuu wa maisha ya ndoa na familia. Wawe ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya upendo katika familia. Tema hii amefafanua zaidi katika Wosia wake wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo katika familia, matunda ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia. Huu ni utajiri na amana ambayo Kanisa limegundua na linataka kuwashirikisha watu wote wenye mapenzi mema.

Kwa kusukumwa na changamoto hizi, Baba Mtakatifu anawataka wajumbe wa Jukwaa la familia kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu hakuwapatia Roho ya woga, bali nguvu, upendo na moyo wa kiasi, mambo msingi yanayoweza kuwaongoza pasi na hofu katika utekelezaji wa sera na mikakati yao kwa kuwatafuta wale walioanguka; kuwakaribisha wale waliotengwa na jamii, kama kielelezo cha huruma ya Baba wa milele. Baba Mtakatifu amewashukuru kwa ari na moyo mkuu kwa yale wanayotekeleza kwa ajili ya familia, ili kweli familia ziweze kushiriki kikamilifu na kuwajibika katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu; kwa kusimamia dhamana ya familia na haki zake msingi.

Wazazi washirikishwe kikamilifu katika masuala ya elimu kwa watoto wao. Wasisite kusimama kidete, kuragibisha familia nchini Italia kuongeza idadi ya watoto, pamoja na kuhakikisha kwamba, wanasaidia kuhamasisha taasisi mbali mbali kutambua na kuthamini watoto wanaozaliwa kuwa ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Watoto ni kitega uchumi kikuu anasema Baba Mtakatifu Francisko, lakini kwa bahati mbaya, watoto hawa wanaonekana kuwa ni sababu ya umaskini wa familia, kiasi hata cha kugeuziwa kisogo na taasisi nyingine. Matatizo na changamoto zote hizi zinapaswa kukabiliwa kwa ari, moyo mkuu na upendo, kwa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za familia zinazofumbatwa katika utu na heshima ya binadamu! Familia ni amana na utajiri mkubwa wa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kumbe, Jukwaa la Vyama vya Kifamilia linapaswa kujielekeza zaidi na zaidi katika huduma kwa familia, kwa kusimama kidete kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

16/06/2018 15:56