2018-06-15 07:28:00

Papa Francisko shikamaneni kupambana na utumwa mamboleo!


Maisha ya binadamu ni matakatifu tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti yanapomfika mtu kadiri ya mapenzi ya Mungu. Mwenyezi Mungu ni asili na kikomo cha maisha ya mwanadamu. Hakuna mazingira yoyote yale yanayoweza kujitwalia haki na mamlaka ya kuharibu zawadi ya uhai. Mama Kanisa anafundisha na kukazia kwamba, uhai wa binadamu sharti uheshimiwe na ulindwe na kwamba: Uhai ni sehemu muhimu sana ya haki msingi za binadamu. Leo hii kuna wimbi kubwa la utamaduni wa kifo unaoendelea kuwanyemelea watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia kwa kuwatumbukiza katika sera za utoaji mimba na kifo laini; mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo sanjari na biashara ya haramu ya binadamu na viungo vyake.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales, Jumapili, tarehe 17 Juni 2018 linaadhimisha Siku ya Uhai Kitaifa. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya, anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufungua macho na nyoyo zao, ili kuweza kusikiliza na kujibu kilio cha mateso na mahangaiko ya waathirika wa biashara haramu ya binadamu na viungo vyake. Anawataka kusimama kidete, kupambana kufa na kupona, ili kuvunjilia mbali mtandao wa biashara haramu ya binadamu duniani, ili hatimaye, kuleta faraja, uponyaji wa ndani na huduma kwa wahanga hawa wa nyanyaso za utu na heshima ya binadamu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza la Wales, linapenda kuihamasisha familia ya Mungu nchini Uingereza na Wales kutambua na kuthamini utu na heshima ya binadamu; wajibu na haki zake msingi, tangu pale mtoto anapotungwa mimba na katika hatua mbali mbali za maisha yake. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutambua na kuenzi utu na heshima ya binadamu kama sehemu ya mchakato wa utakatifu wa maisha, kama anavyoufafanua kwenye Wosia wake wake wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo”.

Waamini watambue vizingiti, changamoto na fursa ambazo wanaweza kuzitumia kufikia utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anawaalika waja wake ili wawe watakatifu, watu wasiokuwa na hatia mbele zake katika upendo. Wajitahidi kumwilisha Heri za Mlimani kama muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu yanayoweza kuwasaidia kufikia utakatifu wa maisha. Umaskini wa roho ni kielelezo cha utakatifu; Upole ni sehemu ya Matunda ya Roho Mtakatifu. Mwamini kwa kufikiri na kutenda katika upole, anaonesha cheche za utakatifu wa maisha. Waamini wajifunze kuhuzunika na kuomboleza na jirani zao; kwa kuwa na njaa na kiu ya haki; kwa kuona na  kutenda katika huruma; kwa kuwa na moyo safi; kwa kupandikiza na kukuza mbegu ya upatanisho na amani!

Katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita, kunako mwaka 2015, Kanisa lilianzisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na utumwa mamboleo, unaoendelea kudhalilisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Takwimu za Jumuiya ya Kimataifa zinaonesha kwamba, zaidi ya asilimia 70% ya wahanga wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni wanawake na masichana, kati yao theluthi moja ni watoto wadogo.

Hii  ni hali ya unyonyaji, unyanyasaji, na mateso ya wanyonge hawa kimwili, kiakili na kisaiokolojia na ni aibu na kashfa kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa inayoonekana hata kutojali kabisa uvunjwaji wa utu, heshima na haki msingi za watu hawa! Papa Francisko anamwomba Mtakatifu Josefina Bhakita, Msimamizi wa waathirika wa biashara haramu ya binadamu, kuwaombea watu wote waliotumbukizwa kwenye utumwa mamboleo, ili kwa neema na msaada wa Mwenyezi Mungu waweze kuokolewa na hatimaye, kusaidiwa kuganga na kuponya madonda ya nyanyaso dhidi ya utu na heshima yao.

Kikundi cha Kimataifa cha Mtakatifu Martha,  kilianzishwa kunako mwezi Aprili 2014 na Baba Mtakatifu Francisko na kuongozwa na Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales, kwa kushirikiana na wakuu wa Majeshi ya Polisi na Maaskofu kutoka sehemu mbali mbali za dunia; kinaendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kung'oa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo pamoja na kutoa huduma za kichungaji kwa wahanga wa vitendo hivi kwa kinyama. Kikundi hiki kwa sasa kinatekeleza dhamana na wajibu wake katika nchi 30 duniani.

Kikundi hiki kinapania pamoja na mambo mengine, kuibua mbinu mkakati wa kuzuia vitendo hivi vya kinyama vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu pamoja na kuendelea kutoa huduma za kichungaji. Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales, Jumapili tarehe 17 Juni 2018, litakusanya mchango kwa ajili ya kugharimia huduma kwa wahanga wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Kikundi cha Kimataifa cha Mtakatifu Martha kinataka pia kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, donda ndugu katika ulimwengu mamboleo. Takwimu kutoka Uingereza zinabainisha kwamba, nchini humo kuna zaidi ya wahanga 13, 000 wa biashara haramu ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.