Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Muswada wa Katiba mpya ya Kitume: Tangazeni Injili umekamilika!

Muswada wa Katika Mpya ya Kitume "Predicate evangelium" yaani "Tangazeni Injili: Mchakato wa mageuzi ya Sekretarieti kuu ya Vatican kuanzia tarehe 13 Aprili 2013 hadi 13 Aprili 2018. - RV

14/06/2018 14:42

Baraza la Makardinali Washauri, Jumatano tarehe 13 Juni 2018 limehitimisha mkutano wake wa XXV uliohudhuriwa na kuongozwa na Baba Mtakatifu Francisko. Makardinali wote washauri wamehudhuria isipokuwa Kardinali George Pell. Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican “akichonga” na waandishi wa Habari mjini Vatican mara baada ya mkutano wa Baraza la Makardinali Washauri amesema, Muswada wa Katiba Mpya ya Kitume “Predicate evangelium” yaani “Tangazeni Injili”: Mchakato wa mageuzi ya Sekretarieti kuu ya Vatican” kuanzia tarehe 13 Aprili 2013 - 10 Aprili 2018.

Haya ni matunda ya mageuzi yaliyoanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican, miaka mitano iliyopita kama sehemu ya utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Baraza la Makardinali wakati wa vikao vyake elekezi kwa ajili ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, kunako mwaka 2013. Muswada wa Katiba mpya ya Kitume “Predicate evangelium” yaani “Tangazeni Injili” unatarajiwa wakati wowote kuwasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kuupitia kwa mara ya kwanza, kuufanyia marekebisho pale atakapoona inafaa na muhimu kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Muswada huu unadadavua hatua muhimu ambazo zimechukuliwa na kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kuhusu uongozi wa Kanisa la Kiulimwengu sanjari na tema muhimu zinazogusa kwa namna ya pekee kabisa Katiba ya Kitume ya “Pastor bonus” yaani “Mchungaji mwema”.

Makardinali washauri wamepata nafasi ya kumsikiliza Monsinyo Brian Ferme, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uchumi ambaye amewasilisha mfumo wa fedha na uchumi wa Vatican. Amefafanua malengo, kanuni sheria na mbinu mkakati wa kubana matumizi, kwa kuendelea kujikita katika falsafa ya ukweli na uwazi; utekelezaji wa kanuni sheria za fedha na manunuzi; kanuni ya udhibiti mara mbili sanjari na kuzingatia viwango vya usimamizi wa fedha kimataifa. Monsinyo Ferme amebainisha matokeo yaliyofikiwa hadi wakati huu ni pamoja na kuandaa bajeti elekezi na utekelezaji wake;pamoja na umuhimu wa kuwa makini katika manunuzi.

Kumekuwepo na ushirikiano pamoja na uelewa mpana katika mchakazo mzima wa mageuzi katika masuala ya fedha. Monsinyo Brian Ferme anakaza kusema, kwamba kuna mafanikio makubwa katika utekelezaji wa kanuni ya ukweli, uwazi na uwajibikaji wa fedha ya Kanisa. Mwishoni, anasema Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican kwamba, Kardinali Sean Patrick O’Malley, alipata nafasi ya kuwajuza Makardinali washauri kuhusu maendeleo ya Tume ya Kipapa kwa ajili ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Baraza la Makardinali Washauri litakutana tena kuanzia tarehe 10-12 Septemba 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

14/06/2018 14:42