2018-06-12 11:00:00

Caritas Internationalis: Shiriki safari na wakimbizi kwa ukarimu!


Kuanzia tarehe 17- 24 Juni 2018 ni juma la utekelezaji wa sera na mikakati ya Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis kwa vitendo. Mwezi Septemba 2018, Caritas Internationalis itahamishia mchakato wa uragibishaji wa kampeni hii kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa, ili kuweza kupitisha miswada miwili ya kimataifa kwa ajili ya ulinzi, usalama na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji duniani. Mwishoni mwa mwaka 2019, Caritas Internationalis itakuwa inahitimisha kampeni hii ya Shiriki safari na wakimbizi pamoja na wahamiaji: “Share the journey”.

Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto changamani kwa wakati huu kutokana na baadhi ya nchi kufunga mipaka na kukataa kupokea na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Dr. Michel Roy, Katibu mkuu wa Caritas Internationalis katika mahojiano na Vatican News anasema, changamoto zote hizi zinapaswa kujibiwa kwa moyo wa ukarimu na upendo! Uchoyo na ubinafsi ni hatari sana katika mchakato wa ujenzi wa mshikamano na huduma ya upendo kwa waathirika wa majanga na maafa sehemu mbali mbali za dunia.

Itakumbukwa kwamba, kuna mashirika 165 ya Misaada ya Kanisa Katoliki yanayoratibiwa chini ya mtandao wa Caritas Internationalis, lengo ni kujenga utamaduni na sanaa ya watu kukutana na kusaidiana kwa hali na mali kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko. Huu ni wakati wa Caritas katika ngazi mbali mbali kuandaa matukio mbali mbali yatakayowasaidia watu kuelewa sababu zinazopelekea watu kuzikimbia nchi zao, ili hatimaye, kuvunjilia mbali mawazo mgando na maamuzi mbele yanayotishia: maisha, usalama, mshikamano na mafungamano ya kijamii.

Ni matumaini ya Caritas Internationalis kwamba, Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, Majimbo, Parokia, Familia na watu binafsi wataweza kushiriki kikamilifu katika kampeni hii kwa kuonesha ukarimu kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa si tu kwa maneno, bali kwa njia ya vitendo, kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji! Hawa ni watu wanaopaswa kuonjeshwa ukarimu katika hija ya maisha yao! Tarehe 20 Juni 2018, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani, muda muafaka anasema Dr. Michel Roy wa kujenga na kudumisha utamaduni na sanaa ya upendo na ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji.

Caritas Internationalis inasikitika kusema kwamba, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji linahitaji suluhu ya pamoja kwani kuna matatizo makubwa ambayo yamefunikwa katika janga hili! Hawa ni watu wanaolazimika kuzikimbia na kuzihama nchi zao kutokana na: vita, kinzani na nyanyaso. Ni watu wanaoteseka kutokana na majanga asilia kama vile njaa, ukame na magonjwa ya kutisha. Ni watu wanaoathirika kutokana na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Kumbe, hawa si watu wanaokimbia nchi zao ili kufanya utalii.

Caritas Internationalis inawataka wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kuguswa na mahangaiko ya wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa, ili hatimaye, waweze kuwafungulia malango ya mipaka yao. Wakimbizi na wahamiaji ni watu wenye historia, tamaduni, amana na utajiri wao unaopaswa kuheshimiwa na kudumishwa na wala wasichukuliwe na kutendewa kama “Mbwakoko”.  Jumuiya ya Kimataifa itafute kiini cha matatizo na changamoto zinazowapelekea watu kukimbia nchi zao, ili kuzipatia ufumbuzi wa kudumu.

Caritas Internationalis inasema kampeni ya “Shiriki Safari” inalenga kujenga umoja na mshikamano kwa kuwaondolea wananchi mahali hofu, mawazo mgando na maamuzi mbele ambaye yamekuwa ni kikwazo katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Dr. Michel Roy anakaza kusema, kuna umuhimu wa kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo na ukarimu unaowakutanisha watu katika medani mbali mbali za maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.