Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Watoto wanaoishi katika mazingira magumu wakutana na Papa! Yaani...!

Papa Francisko amekutana na kuzungumza na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa kukazia umuhimu wa malezi na elimu kwa makuzi na malezxi ya waoto.

11/06/2018 13:50

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 9 Juni 2018 aliugeuza ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican, kuwa ni uwanja wa sherehe na burudani kwa wanafunzi 500 kutoka Milano na Roma waliomtembelea ili kumwona, kumsalimia na kumuuliza maswali yaliyokuwa yanawasumbua nyoyoni mwao! Baba Mtakatifu akajiachia mikononi mwao kama Babu aliyekutana na wajukuu wake tayari kuwasilimua hadhithi na kuwapatia ushauri wa maisha. Kwa hakika ni tukio ambalo kamwe haitakuwa rahisi sana kusahauliwa na watoto hawa kwani wengi wao ni wale wanaotoka pembezoni mwa miji mikuu na hasa katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi na ambazo zinakabiliwa na changamoto mbali mbali za maisha.

Hii ni sehemu ya mbinu mkakati wa Baraza la Kipapa la Utamaduni kwa kushirikiana na Shirika la Reli Italia kuwakirimia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, walau siku moja ya furaha kwa kutembelea Vatican pamoja na kukutana na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Katika tukio hili, Baba Mtakatifu amejibu maswali sita kutoka kwa wanafunzi na walimu wao, kwa kuwashirikisha maisha na changamoto alizokumbana nazo wakati alipokuwa mtoto kama wao.

Kwa namna ya pekee kabisa anamkumbuka kwa heshima zote, Mwalimu wake ambaye baadaye alibahatika kuwa Askofu, akashambuliwa na ugonjwa na hatimaye, kuaga dunia. Huyu ni mwalimu aliyemsaidia katika maisha na masomo yake, akamjengea ari na moyo wa ujasiri, kiasi hata cha kuweza kupambana na changamoto mbali mbali katika maisha yake. Baba Mtakatifu anasema, familia na shule, kilikuwa ni kitovu cha malezi na majiundo yake. Alipenda sana kucheza mpira wa miguu na uwanjani walimtambua kuwa ni mlinda mlango wa kutupwa kwani nafasi nyingine hakuweza kuzimudu. Hawakuwa na mipira iliyonunuliwa kutoka dukani, bali wao wenyewe walijitengenezea mipira ya karatasi, wakacheza na kuridhika katika maisha.

Baba Mtakatifu amewaambia kwamba, alikuwa anapenda kushiriki hata katika sherehe na matukio mbali mbali katika kitongoji chake, ambacho bado anakikumbuka kwa moyo wake wote. Kama ilivyo hata sasa kwa watoto kupita mitaani kuombe “Senti kwa matukio mbali mbali” hata yeye alichangamkia sana matukio kama haya na kushiriki kwa moyo wake wote! Kuhusu maisha na wito wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anasema, tangu alipochaguliwa daima amejisikia amani na utulivu moyoni mwake, hali ambayo inaendelea hadi wakati huu.

Lakini anakiri kwamba, tarehe 21 Septemba, katika maadhimisho Siku kuu ya Mtume Mathayo, Mwinjili ambaye jina lake kwa lugha ya Kigiriki lina maanisha “Zawadi ya Mungu”. Huyu alikuwa ni mtoza ushuru, lakini akabahatika kukutana na Lango la huruma ya Mungu, Kristo Yesu, aliyemwita na akaamua kuacha yote na kumfuasa na huo ukawa ni mwanzo wa toba na wongofu wa Mathayo mtoza ushuru. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba ufunuo wa huruma ya Baba wa milele iligeuka kuwa ni sherehe kubwa ya huruma ya Mungu katika maisha yake, kwani hatimaye, akaamua kufuata wito na maisha ya kipadre kwa kuacha kazi aliyokuwa anaifanya kwenye kiwanda cha kemikali, ili kujibu kilio na kukata kiu ya hamu ya ndani kabisa katika maisha yake.

Watoto pia wamebahatika kusimulia historia, changamoto na shida mbali mbali wanazokumbana nazo kwa njia ya michoro, nyimbo na kazi ya mikono yao, waliyompatia Baba Mtakatifu kama zawadi na kumbu kumbu endelevu ya mkutano wao. Baba Mtakatifu amechukua fursa hii kuwapongeza walimu na walezi kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wanafunzi hawa, ili kuwajengea leo na kesho yenye matumaini makubwa zaidi. Amewataka wanafunzi kujibidisha katika masomo kwa kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema akili zao, mikono na nyoyo zao ili kujichotea ujuzi, hekima na maarifa. Haya ni mambo makuu matatu yanayopaswa kuambatana na kukamilishana.

Baba Mtakatifu amewapatia watoto wote hawa Rozari Takatifu, muhtasari wa historia ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Watoto wameelezea mchakato mzima wa malezi na majiundo yao; wametambua changamoto, matatizo na fursa mbali mbali zinazopatikana katika vitongoji vyao, ili kuweza kuboresha hali ya maisha na kuwajengea matumaini zaidi. Wamejitaabisha kufahamu hali na mazingira ya wazazi na walezi wao miaka iliyopita; wamekutana na viongozi wa serikali na mitaa ili kupata ufafanuzi wa changamoto za kijamii, kiuchumi na kitamaduni zinazowakabili.

Watoto pia wametoa maoni yao jinsi ya kuboresha mazingira ya miji yao kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; kwa kushiriki Ibada na matukio mbali mbali ili kujenga utamaduni wa kukutana na jirani pamoja na kukazia umuhimu wa masomo kama njia muafaka ya kuondokana na umaskini wa hali na kipato! Waalimu na walezi wameelezea hali halisi ya maisha na mazingira wanamoishi wanafunzi hawa na kwamba, kwa sasa kipaumbele cha kwanza ni kujenga utamaduni wa ukarimu, mafungamano ya kijamii pamoja na kukuza kipaji cha ubunifu.

Baba Mtakatifu amewataka waalimu na walezi kuhakikisha kwamba, shule panakuwa ni mahali pa upendo na mshikamano; mahali pa malezi na makuzi ya watoto katika hatua mbali mbali za maisha: kiakili, kimaadili, kiutu, kiroho, kitamaduni na kijamii, ili kukuza na kudumisha ukweli na uwazi badala ya shule kuwa kama pango la wateule wachache wanaotaka kulinda na kudumisha ubinafsi na uchoyo!

Kwa upande wake Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni amesema “Cortile dei gentili” yaani “Ukumbi wa Wastaarabu”  ni fursa kwa watoto wanaotoka katika mazingira magumu na hatarishi, kuweza kutekeleza ndoto ya kuwa na mahali bora zaidi pa kuishi, kwa kuangalia matatizo, changamoto na fursa wanazopambana nazo katika mazingira yao ya kila siku. Ni mchakato wa kutaka kuwajengea wanafunzi ari na mwamko wa kujibidisha kufanya maboresho katika mazingira yao, ili yaweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Kumbe, imekuwa ni nafasi kwa wanafunzi hawa kupanua wigo wa mawazo yao! Hawa ni wanafunzi wanaotoka katika dini, tamaduni na mapokeo mbali mbali, nafasi ya kuheshimiana katika umoja na tofauti zao kama utajiri na amana ya maisha. Wazazi na walezi mbali mbali wamefurahia sana tukio hili la pekee kwa watoto wao ambao wamebahatika kukutana na kuzungumza mubashara na Baba Mtakatifu Francisko. Kardinali Gianfranco Ravasi, amemshukuru Baba Mtakatifu pamoja na viongozi wa Shirika la Reli Italia kwa kuwezesha “Ukumbi wa wastaarabu” kukutana na kuendesha shughuli zake kwa amani na utulivu. Hii ni awamu ya sita kwa wanafunzi wanaotoka katika familia maskini,  mazingira magumu na hatarishi; watoto kutoka  kwa wazazi na walezi walioko magerezani bila kuwasahau watoto walioathirika kwa tetemeko la ardhi kutoka kati kati ya Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

11/06/2018 13:50