Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Sala ya Malaika wa Bwana

Mwenyeheri Sr. Maria della Concezione: Alijisadaka kwa ajili ya vijana

Mwenyeheri Sr. Maria della Concezione alijiweka wakfu kwa Mungu na kujisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa vijana na maskini. - AP

11/06/2018 13:32

Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, Jumapili, tarehe 10 Juni 2018, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amemtangaza Mtumishi wa Mungu Sr. Maria della Concezione kuwa Mwenyeheri katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa huko Agen, nchini Ufaransa. Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amemkumbuka Mwenyeheri mpya na kuwaomba waamini kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Mwenyeheri Sr. Maria della Concezione.

Wakati ule, alikuwa anajulikana kama Adelaide de Batz de Trenquelleòn. Ni muasisi wa Shirika la Watawa wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, maarufu kama “Marianist”. Huyu ni mwanamke wa shoka  aliyejiweka wakfu mbele ya Mungu na kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa vijana wa kizazi kipya. Katika mazingira magumu ya wakati wake, alijiandaa kumshuhudia Kristo hata kwa kumwaga damu yake kama kielelezo cha sadaka ya maisha inayotolewa kwa ajili ya huduma kwa jirani, ili hatimaye, kuweza kurithi maisha ya uzima wa milele anasema Kardinali Angelo Amato katika mahojiano maalum la Vatican News.

Mwenyeheri Sr. Maria della Concezione alizaliwa kunako tarehe 10 Juni 1789, huko Agen, akabatizwa siku hiyo hiyo alipozaliwa, akakulia na kulelewa katika uwanja wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Katika maisha na utoto na ujana wake, akakumbana na athari za Mapinduzi ya Ufaransa yaliyotikisa maisha ya familia yake, kiasi hata cha kujikuta wakiwa wametupwa uhamishoni huko Uingereza.

Tarehe 6 Januari 1801, Sherehe ya Tokeo la Bwana, Mwenyeheri Sr. Maria della Concezione akapokea Ekaristi Takatifu kwa mara ya kwanza, tukio ambalo liliacha alama ya kudumu katika historia ya maisha yake ya kiroho, kiasi cha kuonesha nia ya kutaka kuwa mtawa wa Shirika la Wakarmeli. Alibahatika kupata malezi, makuzi na majiundo makini kutoka kwa mama yake mzazi, kiasi hata cha kuweza kuzama katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kawaida. Akajitoa bila ya kujibakiza kwa kujiweka wakfu kwa Kristo Yesu na Mama yake Bikira Maria, aliyekingiwa Dhambi ya Asili, kielelezo makini cha upendo kwa Mungu na jirani.

Katika ujana wake, akajitaabisha kuzisaidia familia maskini kwa hali na mali; akawawapatia elimu watoto kutoka katika familia maskini na wale wote waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi! Akawafundisha kweli za maisha na kuwapatia Katekesi makini na endelevu juu ya tunu msingi za maisha ya Kikristo; akajenga ujirani mwema na urafiki na vijana wa kizazi kipya. Ni hawa vijana waliounda kikundi cha kutoa katekesi na elimu kwa watoto mitaani, wakajitaabisha kuwatembelea na kuwahudumia wagonjwa na maskini huko vijijini, kiasi hata cha kuweza kuwamegea watu hawa huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani.

Mwenyeheri Sr. Maria della Concezione  aliwasaidia waamini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, lakini zaidi kwa kuwa na ushiriki mkamilifu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kiini cha maisha na utume wa Kanisa na kwamba, Sakramenti ya Upatanisho, iliwaonjesha huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, kwa kuwaganga na kuwaponya dhambi zao. Aliwahimiza waamini kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, ili waweze kumjifunza Kristo Yesu kwa njia ya shule ya Bikira Maria, Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili.

Kunako mwaka 1808 akabahatika kukutana na kufahamiana na Padre Guglielmo Giuseppe Chaminade (1761-1850), Mkuu wa Shirika la Watawa wa Maria huko Bordeau, aliyetangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Mwenyeheri kunako mwaka 2000. Akamwalika Mwenyeheri Maria della Concezione kujiunga na Shirika lao. Wakati huohuo, Sr. Maria della Concezione akakataa kufunga ndoa na mwanaume tajiri na kuamua kusadaka maisha yake katika maisha ya usafi kamili. Akashuhudia umaskini wa hali na kipato; kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema, kiasi cha kutaka kuwaunganisha watawa wa ndani na wale wa maisha ya kitume, ili kusaidia mchakato wa upyaisho wa maisha ya watu waliokuwa wameathirika vibaya sana kutokana na Mapinduzi ya Napoleone.

Tarehe 18 Juni 1815, Mfalme Napoleone akashindwa katika vita, utawala ukarejeshwa mikononi mwa wananchi. Mwenyeheri Sr. Maria della Concezione, akiwa ameungana na watawa wengine watano, hapo tarehe 25 Mei 1816 akaanzisha Shirika la Watawa Watoto wa Bikira Maria. Mwaka 1817 wakaweka nadhiri na kujiweka wakfu kwa Mungu na jirani. Shirika likajielekeza zaidi katika sekta ya elimu, sanaa na ufundi kwa watoto wa maskini, ili kuwajengea uwezo wa kupambana na maisha yao. Akafariki dunia huko Agen, Ufaransa tarehe 10 Januari 1828, huku akiimbiwa utenzi wa sifa na shukrani kwa matendo makuu, ambayo Mwenyezi Mungu alimjalia kutenda kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Kardinali Angelo Amato anakaza kusema, Mwenyeheri Sr. Maria della Concezione anaendelea kupamba orodha ya watakatifu wanawake ambao wamechangia utajiri na amana ya maisha yao ya kiroho kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na huduma kwa jirani zao. Hawa ni kama vile: Watakatifu: Ildegarda wa Bingen, Mt. Brigita, Mt. Theresa wa Avila, Mtakatifu Theresa wa Lisieux, Mt. Mama Theresa wa Calcutta pamoja na umati mkubwa wa wanawake wasiojulikana, lakini ambao wameacha alama ya kudumu katika maisha na utume wa Kanisa. Hawa ni watu waliojisadaka kwa ajili ya kumwilisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; wakarithisha kweli za Kiinjili katika jamii kwa njia ya huduma makini na ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

11/06/2018 13:32