Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Dhambi na matokeo ya ufunuo wa mpango wa ukombozi wa mwanadamu

Mwanadamu ana lazima ya kufuata sheria ya maadili inayomsukuma kutenda jema na kuepuka ovu. Sheria hii yaongea ndani kabisa ya dhamiri ya mwanadamu! - REUTERS

09/06/2018 16:39

Utangulizi: Mungu alipomuumba mwanadamu alikusudia kuanzisha naye mahusiano ya pekee. Alimweka juu ya viumbe vyote avitawale akimjalia tunu na zawadi nyingi ikiwemo kuumbwa kwa sura na mfano wa Mungu mwenyewe. Maandiko Matakatifu katika dominika hii ya 10 ya mwaka B, yanaonesha matokeo ya dhambi katika mpango huu wa Mungu kwa mwanadamu, dhambi iliyoingia kwa uasi wa mwanadamu na kuwa maangamizi kwa mwanadamu mwenyewe. Lakini ili dhambi isiwe na kauli ya mwisho katika mpango wa Mungu kwa mwanadamu, Mungu anaufunua mpango wa ukombozi na kumwalika mwanadamu kuufuata. Tunatafakari leo juu ya uhalisia wa dhambi katika maisha ya mwanadamu na nafasi aliyonayo mwanadamu katika kuishinda dhambi kwa neema ya Mungu.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza: (Mwa. 3:9-15) linaeleza tukio la kuingia kwa dhambi ulimwenguni. Kisha kutenda dhambi, Adamu anajificha. Ndipo Mungu anamwita na kumuuliza, “uko wapi?” Ndiyo kusema “nini kimekutokea wewe uliyekuwa rafiki yangu wa karibu, wewe niliyekutendea mema mengi na mengi bado yalikuwa yanakusubiri? Uko wapi... mbona umeniasi na kujiangamiza mwenyewe” Na tena swali hilo “uko wapi” halikuwa sana katika kuulizia mahali, bali ni katika kuulizia hali.  Ndiyo kumwambia Adamu “hali yako ikoje baada ya dhambi?, bado una uhuru uliokuwa nao au uko mateka, bado una wema uliokuwa nao au umefumbwa na uovu?” Na jibu la Adamu likawa “nilisikia sauti yakoikaogopa kwa maana mimi ni uchi, nikajificha”

Katika hatua inayofuata baada ya Adamu kukiri kuwa yu uchi, yu mtupu na hana chochote tena badala sasa ya kukiri kosa alilolifanya anatupa lawama kwa mkewe Eva. Hata Eva naye anapoulizwa anatupa lawama kwa nyoka! Naye Mungu katika kuadhibu anaanza na nyoka. Hamuulizi kwa sababu alikwisha hukumiwa. Ndivyo inavyowaka hasira ya Mungu juu ya dhambi na juu ya wale wanaowaingiza wengine katika dhambi. Katika maneno “nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa na wewe utamponda kisigino” Kanisa linaona Habari Njema ya kwanza, ndiyo ahadi ya ukombozi. Kwamba katika vita vilivyoanza sasa kati ya uzao wa Ibilisi na uzao wa Eva, ni mwana wa uzao wa Eva atakayemponda kichwa Ibilisi. Na hii ndiyo ahadi ya kwanza ya Mungu kumkomboa mwanadamu mara tu dhambi ilipoingia ulimwenguni (rej. KKK 410).

Somo la pili (2Kor. 4:13-5:1) ni katika mazingira ambayo Mtume Paulo anaelezea magumu ambayo yeye na mitume wengine wanayapata katika kumhubiri Kristo licha ya kuwa wamejitoa kikamilifu katika huduma hiyo. Wanapata misukosuko kutoka nje lakini pia wanapata kutoka ndani yao wenyewe kama alivyosema hapo awali (4:7) “ ..tuna hazina hii katika vyombo vya udongo” kuonesha udhaifu wao binafsi. Somo la pili katika dominika hii linaanza kwa kueleza kuwa pamoja na magumu hayo waliyonayo, wanakitu kinachowafanya wazidi kusonga mbele na wasirudi nyuma wala kukata tamaa. Kitu hicho ni IMANI, “lakini tuna roho ile ile ya imani”. Ndiyo kusema kuwa Imani ni zaidi ya kupokea tu mafundisho, kuyakubali na kuyaishi. Imani inayo nguvu kama ya kumvusha mtu kupita hali mbalimbali za maisha. Ananukuu Zaburi ya 116:10 ambapo mzaburi anakiri kuwa “nalizidi kuamini hata niliposema mimi naangamia”. Ndiyo nguvu ya imani, ndiyo roho ya imani inayoweza kumvusha mtu hata katikati ya giza na hofu katika maisha.

Injili (Mk.3:20-35) Yesu anarudi nyumbani na anapata umati mkubwa sana. Katika ule umati ambao hadi unamzuia Yesu na wanafunzi wake hata kula chakula, Mwinjili Marko anaonesha makundi mawili ya watu. Lipo kundi lililo upande wa Yesu na lipo kundi ambalo lipo kinyume naye. Kundi lililo upande wa Yesu ndilo kundi la ndugu zake. Hawa wanamwona na wanashikwa hofu juu yake kuwa huenda amerukwa na akili. Ni hofu yenye sintofahamu kwa upande wao. Wanamsikitikia Yesu na wanataka kufanya kitu wamsaidie. Kundi la pili ni lile la Waandishi. Hawaamini anachokifanya Yesu na kwa chuki waliyonayo kwake wanasema Yesu mwenyewe ana pepo na anatoa pepo kwa jina la Beelzebuli mkuu wa pepo. Ni shutuma kubwa kabisa kwa Yesu. Katika makundi yote haya mawili, Yesu anawaalika kutambua kuwa walio upande wake, walio ndugu zake hasa ni wale wanaoyafanya mapenzi ya Mungu. Bila kuvunja umuhimu wa undugu wa kibinadamu na nafasi yake, Yesu anataka kuonesha kuwa  kutimiza mapenzi ya Mungu kunapaswa kupewa nafasi ya kwanza katika yote.

Tafakari: Maandiko Matakatifu katika dominika ya leo yanatualika tutafakari juu uhalisia wa dhambi katika maisha yetu. Yanatuonesha kwanza mapato ya dhambi au hali ya mwanadamu baada ya dhambi: mwanadamu anakuwa mtupu mbele ya Mungu, anapoteza neema ya utakaso, anajitenga na Mungu na kujiweka mateka wa shetani. Dhambi inawagawa wafuasi wa Kristo, inawafanya washindwe kumshuhudia, washindwe kuona nguvu ya kuokoa katika yale ambayo Kristo anayafanya daima ulimwenguni. Mungu hamwachi kamwe mwanadamu katika maisha ya dhambi, kama alivyomtafuta Adamu na kutangaza mpango wa ukombozi hata leo Mungu haachi kunyoosha mkono wake kumwinua mwanadamu kutoka udhaifu na kumrudishia hadhi ya mwana wa Mungu. Humwita daima “uko wapi” na ndani ya dhamiri yake humwitia wongofu.

Tunaona pia kuwa kukubali udhaifu, kukubali makosa ni hatua muhimu sana katika kuelekea wongofu. Lakini kutafuta visingizio au kujaribu kuhalalisha udhaifu au mabaya kwa namna moja au nyingine kama Adamu na Eva walivyofanya, hakumsaidii mwanadamu kufikia wongofu. Mtume Yohane anatuandikia kuwa “tukisema hatuna dhambi tunajidanganya wenyewe na kweli haimo ndani yetu bali tukiziungama dhambi zetu Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu na kutusafisha na udhalimu wote” (rej 1Yoh. 1:8-9). Dhambi zote mwanadamu anapoziungama kwa majuto kamili zinapata maondoleo isipokuwa tu kama mtu amejitenga na nguvu ya maondoleo ya dhambi, Roho Mtakatifu. Ndicho anachokisema Kristo kuwa ndiyo dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu.

Padre William Bahitwa.

Vatican News.

09/06/2018 16:39