Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Moyo Mtakatifu wa Yesu: Chemchemi ya huruma, upendo na imani ya Kanisa

Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya huruma na mapendo yanayomwilishwa katika matendo ya Huruma: kiroho na kimwili.

08/06/2018 14:14

Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu inapata chimbuko lake pale juu Msalabani, askari alipomchoma Yesu kwa mkuki ubavuni, mara ikatoka damu na maji, alama za Sakramenti za Kanisa. Kunako mwaka 1673 Mtakatifu Margherita Maria Alacoque akatokewa na Kristo Yesu na kumpatia dhamana ya kutangaza na kueneza Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu, lakini zaidi kwa wadhambi wanaothubutu kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata utakatifu wa maisha. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2002 akatenga Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu kuwa ni Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa kufunga Mwaka wa Mapadre Duniani, tarehe 3 Juni 2016 aliwataka Wakleri kujichotea utajiri wa maisha ya kiroho unaofumbatwa katika Waraka wa Kitume wa Papa Pio XII, “Haurietis acqua” wa Mwaka 1956 kuhusu “Moyo Mtakatifu wa Yesu kiini cha huruma ya Mungu”. Ni chemchemi ya: imani, upendo, huruma, msamaha, uvumilivu na uaminifu na unyenyekevu wa Mungu, aliyejifanya kuwa mdogo ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Ijumaa, tarehe 8 Juni 2018 amekaza kusema, Mwenyezi Mungu ni asili na chemchemi ya upendo usiokuwa na kifani. Amejifunua kwa njia upendo pasi na makuu! Neno wa Mungu akafanyika mwili na kukaa kati ya watu wake. Upendo wa Mungu unamwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama mwendelezo wa ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu!

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye alimpenda binadamu tangu awali na akaamua kumsindikiza na kumsaidia katika hija ya maisha yake. Si rahisi sana kwa mwanadamu kutambua upendo wa Mungu katika maisha yake, kwani huu ni upendo unaovuka mipaka ya uelewa na ufahamu wa binadamu ni sawa na bahari ambayo haina mwisho. Upendo wa Mungu unafahamika kwa kuupokea na kuumwilisha kwa wengine. Mwenyezi Mungu amewafundisha waja wake upendo kwa kuambatana nao bega kwa bega, siku kwa siku; kwa kuwalinda na kuwatunza.

Mwenyezi Mungu ameufunua upendo wake kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu akatwaa mwili na kukaa kati ya watu wake. Ni upendo ambao umeweza kufahamika kwa njia ya matukio ya kawaida kabisa katika maisha ya mwanadamu. Matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni muhtasari wa upendo na huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu hadi wakati huu. Upendo wa Mungu unamwilishwa katika matendo kwani maneno matupu hayawezi kuvunja mfupa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

08/06/2018 14:14