Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Mang'amuzi ya kimaadili kuhusu mfumo wa uchumi na fedha duniani

Fedha inapaswa kuwa ni kipimo na kikolezo cha huduma na maendeleo endelevu ya binadamu! - AP

08/06/2018 14:36

Hivi karibuni, Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu yalichapisha Waraka wa pamoja unaojulikana kama “Oeconomicae et pecuniariae quaestiones” yaani “Mang’amuzi ya kimaadili kuhusu mfumo wa uchumi na fedha”. Fedha inapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu na wala si mtawala. Waraka huu unapembua pamoja na mambo mengine umuhimu wa kutenganisha shughuli za Benki za kibiashara na vitega uchumi hatarishi ambavyo vimepelekea mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa na waathirika wakuu ni familia.

Waraka huu, unaonya kuhusu nguvu kubwa ya kiuchumi kutoka kwenye Mashirika na Taasisi za Fedha Kimataifa, kiasi cha kutumia siasa kwa ajili ya mafao yao binafsi. Huu ni waraka ambao kimsingi unapaswa kuwa ni kiini cha tafakari na mang’amuzi ya watunga sera kiuchumi, wafanyakazi katika taasisi za fedha kitaifa na kimataifa; watunga sheria na kanuni za fedha pamoja na wale wote wanaodhibiti mzunguko wa fedha duniani. Huu ni Waraka unaogusa tema tete ya soko la fedha kimataifa! Utu na heshima ya binadamu; ustawi na maendeleo ya wengi ni mambo msingi katika kupanga na kutekeleza sera na mikakati ya uchumi endelevu unaopaswa kugusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu ya binadamu, hivi karibuni, ameuzindua Waraka huu wa“Oeconomicae et pecuniariae quaestiones” wakati wa mkutano wa 65 wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo na Biashara, UNCTAD, huko Geneva, Uswiss. Katika hotuba yake amekazia kuhusu changamoto kubwa ya utandawazi, mfumo wa fedha kimataifa sanjari na mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu. Huu ni mfumo wa uchumi huria ambao umekuwa na athari kubwa kwa familia ya binadamu. Sera na mikakati ya uchumi endelevu inajikita kwa namna ya pekee katika maendeleo ya mtu mzima!

Lakini kwa bahati mbaya sana, mfumo wa fedha kimataifa umekuwa ni mzigo mkubwa kwa familia ya binadamu kutokana na kuongezeka kwa deni kubwa katika Pato Ghafi la Taifa kiasi cha kuhatarisha uchumi na ustawi wa jamii kutokana na usimamizi mbovu wa masuala ya fedha. Matokeo yake ni kuona hata ile akiba kidogo kutoka kwa familia inayeyuka na kuwatumbukiza watu katika ugonjwa wa sonona. Hizi ni nguvu za kiuchumi zinazowatenga watu badala ya kukuza na kudumisha mshikamano unaoratibiwa na kanuni auni msingi wa ustawi na maendeleo ya wengi.

Katika mazingira kama haya anasema Kardinali Peter Turkson, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuzingatia kanuni maadili kama sehemu muhimu sana ya kupanga na kutekeleza sera na mikakati mbali mbali ya kiuchumi. Kanisa kwa upande wake, linatoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, sanjari na upendeleo kwa maskini. Lakini kwa bahati mbaya, mfumo wa fedha kimataifa umegubikwa na blanketi la uchoyo na ubinafsi pamoja na matumizi mabaya ya uongozi mambo yanayohatarisha uchumi wa dunia. Kanisa linapenda kukazia utu, uhuru na matumizi sahihi ya fursa mbali mbali zinazojitokeza, daima ustawi na maendeleo ya wengi vikipewa msukumo wa pekee.

Takwimu za kifedha zinaonesha kwamba, wawekezaji wakuu ni kutoka katika sekta binafsi na kumbe, wanahitaji kupata faida kubwa, hata kama ni kwa hasara ya watu au makampuni mengine. Hapa kuna haja ya kujikita katika uwajibikaji kwa ajili ya mafao ya wengi; haki na amani; mshikamano  na uwajibikaji. Ufanisi, mashindano, uongozi na haki stahiki ni misamihati inayopaswa kuboreshwa kwa kujikita katika kanuni maadili. Mfumo wa uchumi na fedha unakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na ukweli kwamba, faida kubwa kwa wadau ndicho kigezo msingi cha uongozi wa makampuni mbali mbali ya fedha kitaifa na kimataifa.

Kuna mabadiliko makubwa katika mfumo wa fedha ambao umeyawezesha baadhi ya makampuni makubwa kupata faida kubwa kwa hasara ya makampuni mengine. Msukumo mkubwa ni biashara bila haya ya kuwa na sera na mikakati ya kulinda akiba ya wateja wao. Kuna baadhi ya vituo vya fedha kimataifa vimechangia kuboromoka kwa kanuni maadili katika mchakato mzima wa usimamizi wa fedha. Kuna baadhi ya makampuni makubwa yamekuwa ni wakwepa kodi wa kutupwa, kwa kutotimiza kanuni maadili na hivyo kuwa ni kikwazo cha maendeleo ya wengi.

Kardinali Turkson anasema, mzunguko mkubwa wa fedha kimataifa ni ile fedha chafu inayotokana na biashara haramu ya dawa za kulevya, vitendo vya kigaidi, rushwa na ufisadi; pamoja na utumwa mamboleo. Taarifa ya mwaka 2014 inaonesha kwamba, kiasi cha dola bilioni 50 zinawekezwa Barani Afrika. Ili kuweza kukabiliana na wimbi la fedha chafu kuwekezwa sehemu mbali mbali za dunia, Kardinali Turkson anasema kuna haja ya kujikita katika kusimamia na kuratibu ubora na uhakika wa bidhaa na huduma zinazozalishwa kwenye masuala ya uchumi na fedha. Viongozi wa Serikali watoe vyeti kwa huduma na bidhaa ili kulinda afya na kuzuia vitendo vya kihalifu.

Makampuni yawe na ujasiri wa kujichunguza yenyewe, ili kuhakikisha kwamba, yanazingatia: sheria, kanuni na taratibu za fedha kitaifa na kimataifa; hatua muhimu sana katika mchakato wa maamuzi ya sera na mikakati ya makampuni mbali mbali. Umefika wakati kwa makampuni kuwadhibiti wafanyabiashara haramu kwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu zilizopo kitaifa na kimataifa. Kimsingi, Jumuiya ya Kimataifa inawajibika kufanya mageuzi ya haki katika mfumo wa uchumi na fedha kimataifa, kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema. Katika shughuli zao za kila siku, wazingatie: haki, ukweli, usawa na mshikamano. Viongozi wa serikali na Jumuiya ya Kimataifa; watunga sera na wanazuoni sehemu mbali mbali za dunia wanapaswa kushirikiana na kushikamana ili kumwilisha mageuzi haya kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

08/06/2018 14:36