Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Kardinali Bassetti asema, machafuko ya kisiasa Italia yalikuwa hatari

Machafuko ya kisiasa nchini Italia yalichochewa zaidi na matumizi haramu ya mitandao ya kijamii. - REUTERS

08/06/2018 15:03

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Alhamisi jioni 7 Juni 2018 imeadhimisha mkesha wa sala kwa ajili ya kuiombea Italia ambayo tangu baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika hapo tarehe 4 Machi 2018 imepitia kipindi kigumu cha machafuko ya hali ya kisiasa, kiasi hata cha kupoteza dira, mwelekeo na lengo la siasa ambalo kimsingi ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, hasa kwa kulinda maskini na wale wasiokuwa na sauti katika jamii!

Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika tafakari yake anagusia kuhusu: umuhimu wa wananchi wa Italia kujenga na kudumisha uzalendo utakaowawezesha kutumia vyema karama zao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na wala si kwa ajili ya uchu wa mali na madaraka. Familia ya Mungu nchini Italia iendelee kuonesha huruma na mapendo kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi.

Baada ya hali tete kisiasa nchini Italia kupewa kisogo hivi karibuni kwa kuundwa serikali mpya chini ya Professa Giuseppe Conte kama Waziri mkuu, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, linapenda kutoa pongezi zake za dhati kwa Baraza jipya la Mawaziri na kwamba, Serikali mpya inapaswa sasa kuanza kujielekeza zaidi katika huduma kwa familia ya Mungu nchini Italia, kwa kujikita zaidi katika: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kardinali Bassetti anasikitika kusema kwamba, machafuko ya kisiasa nchini Italia hivi karibuni, yalichochewa zaidi na matumizi haramu ya mitandao ya kijamii, hata dhidi ya Rais Sergio Mattarella wa Italia, ambaye kadiri ya Katiba ya nchi, alitakiwa kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi. Kuna haja ya kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano unaosimikwa katika kanuni maadili na utu wema; kwa upendo na mshikamano ili kuboresha maisha ya wananchi wengi wanaoteseka kutokana na hali ngumu ya uchumi. Ni wakati wa ujenzi wa Italia mpya kwa kujikita zaidi katika hekima, uvumilivu na ukarimu, ili kujenga na kudumisha: Injili ya amani; kazi, utamaduni na maendeleo endelevu ya binadamu.

Ni muda muafaka wa kuondokana na chachu ya ubaguzi wa aina mbali mbali sumu kali inayopekenya utu na heshima ya binadamu; maamuzi mbele na woga usiokuwa na mvuto wala mashiko. Ni wakati wa kuondokana na ubinafsi unaofumbatwa katika uchu wa mali na madaraka, ili kuanza kutumia karama na mapaji ambayo kila mtu amekirimiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Italia. Viongozi wa kisiasa watambue kwamba, uongozi ni huduma kwa ajili ya Italia na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake. Waamini wa Kanisa Katoliki waendelee kushiriki kikamilifu katika shughuli za kisiasa kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu kwa uwepo na ushuhuda wao wenye mvuto na mashiko!

Hii ni huduma inayopania kukuza na kudumisha demokrasia, ustawi na maendeleo ya wengi; daima waamini watambue kwamba, wanapaswa kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa. Umefika wakati wa kuanza mchakato wa sera na mikakati mpya katika medani mbali mbali za maisha, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa vijana, ili waweze kushirikisha karama na mapaji yao; kwa kukuza na kudumisha kanuni maadili na utu wema. Kimsingi, Italia inataka kutekeleza wito na dhamana yake kwa kuwajibika zaidi katika ujenzi wa amani, ustawi na maendeleo ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

08/06/2018 15:03