Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Papa Francisko asikitishwa sana na maafa ya Volkano ya Fuego!

Papa Francisko asikitishwa sana na maafa yaliyosababishwa na mlipuko wa Volkano ya Fuego nchini Guatemala. - AP

06/06/2018 09:34

Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na taarifa za maafa makubwa yaliyotokea hivi karibuni huko nchini Guatemala baada ya Volkano ya Fuego kulipuka na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Nicolas Thevenin, Balozi wa Vatican nchini Guatemala, anasema, anapenda kutolea sala na sadaka yake kwa wale wote waliofariki dunia pamoja na kujeruhiwa kutokana na mlipuko huo.

Baba Mtakatifu anasema, yuko karibu na wale wote wanaoendelea kuomboleza kutokana na maafa haya asilia. Anaungana na wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu walioathirika! Anawaombea moyo na ari ya mshikamano; amani na utulivu wa ndani pamoja na matumaini ya Kikristo, wanapokabiliana na hali tete katika maisha yao kwa wakati huu. Mwishoni, Baba Mtakatifu anapenda kutoa baraka zake za kitume!

Mlipuko huu wa Volcano umesababisha zaidi ya watu 70 kupoteza maisha na kwamba, eneo lililoathirika zaidi ni mji wa Escuintla na Askofu Victor Hugo Palma Paul, ameiomba serikali pamoja na wasamaria wema kusaidia kuokoa maisha ya wananchi wake pamoja na kuwapatia msaada wa hali na mali. Shirika la Misaada ya Kanisa Katoliki nchini Guatemala kwa sasa linaendelea kuchakarika usiku na mchana ili kutoa huduma kwa waathirika wanaohudumiwa sasa kwenye Parokia tatu Jimboni humo.

Tarehe 10 Juni 2018 itakuwa ni Siku ya Mshikamano wa Kijimbo, ili kukusanya mchango kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa mlipuko huu wa Volkano. Caritas Guatemala inahofia kwamba, pengine zaidi ya watu 3, 000 watakuwa wameathirika pengine hata kufukiwa kwenye majivu wa Volkano hii kuwahi kutokea nchini Guatemala katika kipindi cha miaka 44 iliyopita. Caritas Guatemala inaendelea kufafanua kwamba, watu zaidi ya milioni moja na laki saba wameguswa na kutikiswa na maafa haya! Kuna uharibifu mkubwa wa makazi na miundo mbinu ya huduma ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya jamii na kwamba, miundo mingi ya barabara imeathirika kiasi kwamba, kwa sasa mawasiliano ni magumu sana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

06/06/2018 09:34