Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Changamoto ya maendeleo ya sayansi katika sekta ya kazi na ajira!

Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika ulimwengu wa utandawazi yamekuwa na athari kubwa sana katika maisha ya kijamii hususan katika soko la ajira duniani na waathirika wakuu ni vijana wa kizazi kipya! - REUTERS

06/06/2018 08:58

Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, changamoto ya ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya; mazingira bora zaidi ya kazi na elimu kwa wanawake kama sehemu ya mchakato wa kupambana na umaskini pamoja na kuhakikisha kwamba, utumwa mamboleo unaoendelea kunyanyasa utu na heshima ya binadamu unang’olewa kutoka katika uso wa dunia! Kwa muhtasari huu ndio mchango wa mawazo mazito yaliyotolewa na Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, wakati alipokuwa anashiriki katika kikao cha 107 cha Shirika la Kazi Duniani, ILO hivi karibuni!

Askofu mkuu Jurkovic anasema,  kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika sekta ya uchumi na katika mchakato mzima wa kutunga sera za maendeleo. Lakini kutokana na kukua kwa uchumi wa dunia, kuyumba kwa nguvu za kisiasa na kijeshi; ongezeko kubwa la idadi ya watu; changamoto za kijamii na kimazingira pamoja na  kuendelea kuwepo kwa athari za myumbo wa uchumi kimataifa; ni mambo ambayo yanahitaji mjadala endelevu kati ya watunga sera, lakini zaidi umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuendeleza na kutekeleza sera zinazotungwa!

Ujumbe wa Vatican katika mkutano huu unakaza kusema, kazi ni utimilifu wa utu na heshima ya binadamu, kumbe, inapaswa kuwa ni shirikishi na inayowaunganisha watu wote katika jamii, kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu. Kumbe, kazi haina budi kujikita katika mambo makuu matatu: maendeleo ya kiuchumi, mafungamano ya kijamii na mazingira endelevu, daima; mahitaji msingi, utu na heshima ya binadamu vikipewa msukumo wa pekee. Mazingira bora ya kazi yanafumbatwa pia katika ujira wa haki na usawa, unaowawezesha wananchi kuishi kama binadamu; kwa watu kutambua maana ya maisha, hatima yao, kwa kuwa na maisha bora yanayosimikwa katika utu, kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Askofu mkuu Jurkovic anaendelea kufafanua kwamba, maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia na utandawazi yamekuwa na athari kubwa sana katika maisha ya kijamii na katika soko la ajira, hasa kutokana na ukweli kwamba, nchi nyingi bado zimeathirika sana kutokana na mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa. Fursa za ajira zimepungua sana na kiasi kikubwa cha kazi zinafanywa na mashine, ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza faida katika vitega uchumi. Matokeo yake ni changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ufanisi wa kiuchumi na uzalishaji dhidi ya utu na heshima ya binadamu, bila kusahau kanuni maadili na utu wema!

Kimsingi, teknolojia inapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kuna watu wana fursa za ajira, lakini bado wanaendelea kuogelea katika umaskini wa hali na kipato! Kumbe, ajira inapaswa kuwawezesha watu kuwa huru zaidi, kukuza na kudumisha kipaji cha ubunifu; kwa kukuza na kudumisha ushirikishwaji na mafungamano ya kijamii, ili kudumisha utu na heshima ya binadamu anasema Baba Mtakatifu Francisko.

Uchumi wa dunia unaendelea kucharuka kwa kasi kubwa, lakini kwa bahati mbaya, hautengenezi fursa mpya za ajira kwa vijana wa kizazi kipya, changamoto ni kuhakikisha kwamba, vijana wanapewa kipaumbele katika sera na mikakati ya kazi duniani. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja ya kuwekeza katika elimu, taaluma na ujuzi kwa vijana, ili kuwajengea uwezo wa kutumia karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vijana washirikishwe kikamilifu katika maendeleo ya teknolojia, mitandao ya kijamii, tafiti na ugunduzi. Vijana washirikishwe katika mchakato wa demokrasia, upyaisho wa kimaadili na maendeleo ya mtu binafsi, ili kweli vijana waweze kuwa ni kikolezo cha maendeleo endelevu ya binadamu na kwa jinsi hii, kazi inakuwa ni fungamanishi!

Askofu mkuu Jurkovic anaendelea kufafanua kwamba, kuna haja ya kufanya maboresho makubwa katika masuala ya kazi kwa kuwajengea wanawake mazingira bora ya kazi; kwa kuwapatia haki sawa katika soko la ajira; kwa kuheshimu haki zao msingi na majukumu yao ya kimama, ili kukuza na kudumisha haki jamii! Wanawake wawezeshwe kushiriki katika ajira na kutekeleza dhamana na majukumu yao ya kifamilia, kwani wao ni kiungo muhimu sana katika familia; katika malezi na makuzi ya watoto wao. Kwa kutambua majukumu haya, utu na heshima ya wanawake vitakuzwa na hatimaye, ubaguzi dhidi ya wanawake, utaweza kupewa kisogo katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu.

Ili kweli wanawake waweze kupata fursa za ajira na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo endelevu ya jamii, kuna haja ya kuwawezesha kielimu, kiuchumi, kijamii na kisiasa. Elimu itawasaidia kupambana na umaskini na mifumo yote ya ubaguzi; itawasaidia kusimamia haki zao msingi, kuwajibika na kupata ujira stahiki. Wanawake na wasichana wengi kutoka katika Nchi zinazoendelea duniani, bado wanabaguliwa katika masuala ya elimu.

Matokeo yake, ni wanawake kutumbukizwa katika mifumo ya utumwa mamboleo, unaonyanyasa na kudhalilisha utu na heshima yao kama binadamu. Ujumbe wa Vatican kwenye mkutano huu, unalaani vitendo vyote vya nguvu na nyanyaso dhidi ya wanawake sehemu mbali mbali za dunia. Lakini, pia unatoa angalisho kuhusu dhana ya “Ukoloni wa kisera”. Ni matumaini ya Askofu mkuu Ivan Jurkovic kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaendelea kujizatiti katika maboresho ya kazi kama kiini cha haki jamii; ili kukuza na kudumisha mshikamano na mgawanyo bora wa rasilimali za dunia pamoja na wafanyakazi kupata ujira stahiki. Wanawake wanao mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kumbe, waheshimiwe na kutendewa haki; waendelezwe na kuthaminiwa utu na heshima yao kama binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

06/06/2018 08:58