Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Habari \ Habari za Kimataifa

UNICEF: Vita ni chanzo kikuu cha maafa na majanga kwa watoto duniani

UNICEF: Vita, vurugu na kinzani za kijamii ni vyanzo vikuu vya maafa na majanga yanayowapata watoto wengi duniani kiasi cha kurudisha nyuma maendeleo ya elimu, afya na ustawi wa wananchi wengi. - REUTERS

05/06/2018 11:55

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres, hivi karibuni amehitimisha ziara yake ya kikazi nchini Mali ambako ameshuhudia mateso na mahangaiko ya watoto kutokana na vita inayoendelea huko; lakini vita ambayo kwa sasa inaonekana kana kwamba, imesahaulika! Zaidi ya watoto 850, 000 wenye umri chini ya miaka mitano wako hatarini kukumbwa na utapiamlo na kati yao, watoto 274, 000 wanaweza kupatwa na utapiamlo wa kutisha. Kuna zaidi ya watoto milioni moja ambao hawana nafasi ya kwenda shule ya msingi, kiasi hata cha kuhatarisha: ustawi na maendeleo yao kwa siku za usoni.

Idadi ya watoto ambao hawakubahatika kuendelea na shule ya sekondari nchini Mali, imefikia kiasi cha watoto milioni moja. Taarifa zinaonesha kwamba, shule za msingi 750 zimefungwa kutokana na vita. Idadi ya vifo vya watoto wachanga inaendelea kuongezeka maradufu na kwamba, wanawake wajawazito nao wako hatarini kupoteza maisha yao kutokana na kushindwa kupata huduma makini. Kwa muhtasari, hii ni taarifa iliyotolewa na Bi Henrietta H. Fore, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF. Mali ni kati ya nchi 10 duniani ambazo watoto wake wanateseka kutokana na vita, kinzani na migogoro ya kijamii.

UNICEF inasema, nchi nyingine ni: Yemen, Siria, DRC na kwamba, idadi ya watoto wanaoteseka kutoka na vita inazidi kuongezeka maradufu. Nchi Sudan ya Kusini, zaidi ya watoto 19, 000 wanaendelea kutumiwa kama chambo cha vita, wabeba mizigo, wapishi na hata wakati mwingine wanadhalilishwa kijinsia. Vita sehemu mbali mbali za dunia inaendelea kusababisha majanga na maafa makubwa hasa kwa watoto na wanawake. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa, kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, amani inapatikana, ili watu waweze kujikita katika mapambano dhidi ya baa la njaa, ujinga na umaskini wa hali na kipato! Watoto wanahitaji mazingira ya haki, amani na utulivu ili waweze kwenda shule. Mashambulizi dhidi ya shule, hospitali, vituo vya afya na zahanati ni hatari sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

05/06/2018 11:55