2018-06-05 14:21:00

Tarehe 5 Juni ya kila mwaka ni Maadhimisho ya Siku ya Mazingira duniani!


Kukataa matumizi ya plastiki zinazotumika mara moja na kutupwa ni changamoto duniani,na  ndiyo wito mkuu kutoka sauti kuu ya Umoja wa Mataifa katika siku ya maadhimisho ya Mazingira Duniani ambayo uhadhimishwa kila ifikapo tarehe 5 Juni ya kila mwaka. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres katika tukio la maadhimisho hayo amesema Sayari yenye afya ni muhimu kwa mustakhabali wenye mafanikio na amani. Sisi sote tuna jukumu la kutekeleza katika kulinda makazi haya tuliyo nayo. Je plastiki zitumiwazo mara moja na kutupwa zinaishia wapi? Bwana Antonio Guterres amesema, kila mwaka zaidi ya tani milioni 8 za plastiki huishia kutupwa baharini. Chembechembe za plastiki baharini hivi sasa zinazidi idadi ya nyota katika anga letu. Kuanzia visiwa vya mbali hadi Artic, hakuna mahali ambapo hapajaguswa. Kwa maana hiyo Bwana Guterres amesema, ifikapo mwaka 2050 bahari zote zitakuwa na plastiki nyingi zaidi kuliko samaki endapo hakuna jitihada za kupunguza matumizi ya plastiki. Kwa njia hiyo amesisitiza kuwa:kwa pamoja tunaweza kubadilisha njia kuelekea ulimwengu safi wenye kujali mazingira. Kataa matumizi ya plastiki zinazotumiwa mara moja  na kutupwa.

Katika siku hiyo, ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 5 June, kwa mwaka 2018 imebeba kauli mbiu, komesha uchafuzi wa mazingira utokanao na plastiki, kauli hiyo ikizitaka serikali, viwanda, jamii na watu binafsi kuungana na kutafuta njia mbadala ambayo ni endelevu  na itakayopunguza haraka uzalishaji na matumizi ya kupindukia ya mara moja ya plastiki zinazochafua mazingira ya bahari , kuathiri viumbe wa majini na kutishia afya ya binadamu. Kwa mujibu wa Mpango wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Mazingira (UNEP) India ndiyo mwenyeji wa siku ya mazingira duniani 2018. Pamoja na kuwa mstari wa mbele, nchi ya India ni mahali ambapo wanazalisha milioni 5,6 za tani ya uchafu wa plastiki  na ndiyo maana mada inajikita kuzingatia kuwa, kile Kisichofaa kutumika tena na tena achana nacho, na inawezekana kabisa kuhamasisha mapendekezo mbadala kwa ajili ya plastiki hasa kwa njia ya maendeleo mapya ya zana. Hata hivyo Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Mazingira (Unep) umekumbusha kuwa kila mwaka wanatupa uchafu wa tani milioni 8 za plastiki katika bahari na kusabisha majaribu, mateso na changamoto kubwa kwa viumbe wote hai katika  mabahari.

 Nchini India  pamoja na hayo yote ina historia ya muda mrefu ya kukumbatia maisha ya pamoja na maliasili na imejizatiti kuifanya dunia kuwa safi na yenye mazingira bora. Mkuu wa  UNEP Erik Solheim wakati wa uzinduzi wa siku hii alikuwa amesema, India ni  mwenyeji mzuri wa kimataifa wa siku hiyo kwani imeonyesha uongozi bora katika kukabili mabadiliko ya tabia nchi na haja ya kuhamia kwenye uchumi utumiao kiwango kidogo cha hewa ukaa na sasa itakuwa mstari wa mbele katika kuchagiza ukomeshaji wa matumizi ya plastiki duniani.

Siku ya mazingira duniani ilianza kuadhimishwa mwaka 1972  ambapo kwa sasa imekuwa ni maadhimisho ya kimataifa yenye lengo la kuelimisha umma kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu mazingira, hasa katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali hewa. Na ndiyo maana hata  katika tukio la kuadhimisha mwaka huu, ni kuhimiza  juhudi dhidi ya matumizi ya plastiki zitumikazo mara moja tu na kutupwa, kwa maana ulimwengu unahitaji ufumbuzi mbadala dhidi ya  matumizi ya vifaa vya plastiki vinavyotumika mara moja na kutupwa.

Katika ripoti iliyotolewa mapema mwaka huu kuhusiana na maadhimisho ya siku ya mazingira, kauli mbiu ilitolewa mjini Nairobi, Kenya na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa, (UNE), Erik Solheim, wakati wa uzinduzi wa ripoti mpya inayotathmini uwezekano wa kuachana na plastiki zinazotumika mara moja na kuibuka na njia mbadala.  Bwana Solheim alisema, kubadili mtindo wa  kutumia plastiki zinazotupwa punde baada ya kutumiwa hadi vyombo vingine mbadala, ni uwekezaji wa muda mrefu wa mazingira yetu. Ripoti hiyo ilichapishwa  kwa kila ofisi ya mazingira ya Umoja wa Mataifa ilichoita, juhudi za kuupatia ulimwengu maarifa ya kupunguza utupaji hovyo wa taka za plastiki na taka hizo kuishia baharini,kwenye mito na maziwa. Ripoti hiyo ilikuwa inasema, bahari zimezidi kuwa kama jalala la taka za plastiki hatua ambayo ina athari iliyodhihirishwa kijamii, kiuchumi na kimazingira. Kwa maana hiyo Bwana  Solheim alisisitiza kwamba, vifaa mbadala vina mchango katika kupunguza utegemezi kwa plastiki. Ripoti imekariri baadhi ya vyanzo vya plastiki mbadala kama vile karatasi, pamba, na mbao pamoja na kahawa, maganda ya mananasi pamoja na mengine. 

Mmoja wa wali tayarisha ripoti hiyo, Peter Kershaw alionesha malengo makuu hasa ya kuhamasisha jamii kujiuliuza maswali  kuhusu matumizi ya sasa ya plastiki na kufikiria matumizi mbadala, akitilia mkazo zile bidhaa ambazo zinatengenezwa kwa matumizi ya mara moja. Hata hivyo hata Mwanasayansi mkuu katika shirika hilo, Jian Liu, alisema, sayansi inaweza kusaidia jamii ya kibiashara kuwa na suluhisho mbadala ambalo haliharibu mazingira:Kuna nafasi kubwa katika nyanja za ajira na biashara katika ubunifu na uendelezaji wa bidhaa mpya za ubunifu ambazo zitachukua pahala pa plastiki za kutumia mara moja tu.

Sr Angela Rwezaula 
Vatican News

 








All the contents on this site are copyrighted ©.