Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Mapambano dhidi ya utumwa mamboleo yanahitaji ushirikiano wa dhati!

Papa Francisko: Biashara ya binadamu na utumwa mamboleo ni uhalifu dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. - AP

05/06/2018 10:10

Kikundi cha Mtakatifu Martha ni taasisi ya kimataifa dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo kilichozinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2014, ili kupambana na donda hili la kijamii, linalodhalilisha utu na heshima ya binadamu kwa kuwatumbukiza watoto, wasichana na wanawake katika utumwa mamboleo. Biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni uhalifu mkubwa dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu; mambo ambayo wakati mwingine yanafumbiwa macho na jamii, lakini umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inatokomeza kabisa biashara ya binadamu na athari zake.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, wakimbizi na wahamiaji ni wahanga wakubwa wa biashara ya haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, unaoendeshwa na magenge makubwa ya uhalifu kimataifa, donda ndugu katika ulimwengu mamboleo dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Huu ni uhalifu dhidi ya binadamu, pamoja na mambo yote yanayoweza kutekelezwa kwa njia ya ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa, lakini tiba muafaka ni toba na wongofu wa ndani ili kuachana na tabia na utamaduni wa kifo!

Uongozi bora na makini katika vikosi vya ulinzi na usalama; umoja na ushirikiano miongoni mwa wanasiasa pamoja na mihimili ya uinjilishaji, ni muhimu sana katika kupambana na janga la biashara ya binadamu na utumwa mamboleo unaofumbatwa katika; utalii na biashara ya ngono na kazi za suluba! Hivi karibuni, Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa akichangia mada kuhusu umuhimu wa Kikundi cha Mtakatifu Martha, anasema, Taasisi hii ya Kimataifa kwa kushirikiana na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa Kanisa pamoja na viongozi mbali mbali wa umma, imeamua kujizatiti kikamilifu katika kupambana na utumwa mamboleo kwa kujenga na kudumisha imani kwa viongozi; kwa kuibua mbinu mkakati wa huduma kwa waathirika pamoja na kuwajibika kutekeleza yale yaliyoamriwa.

Huu ni mshikamano wa dhati unaoweza kuleta mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya biashara ya binadamu na utumwa mamboleo. Hapa kuna haja ya kuwa na sera pamoja na mbinu mkakati zinazotekelezeka, ili kufutilia mbali biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; biashara na utalii wa ngono pamoja na kazi za suluba, madonda yanayoathiri utu na heshima ya binadamu. Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kuweka sera na mikakati ya kuzuia na kuwaadhibu wahusika kama ilivyoamriwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2000 na baadaye kufanyiwa marekebisho kwa kukazia: umuhimu wa kuzuia, kuwalinda waathirika, kuwashtaki wahusika pamoja na kujenga ushirikiano kati ya wadau mbali mbali ili vitendo hivi vya kinyama viweze kupewa kisogo!

Askofu mkuu Bernardito Auza anasema, Mpango wa Maendeleo Endelevu wa mwaka 2015 hadi mwaka 2030, Jumuiya ya Kimataifa inapania kufutilia mbali mifumo yote ya: biashara ya binadamu, utumwa mamboleo na unyonyaji; pamoja na nyanyaso dhidi ya watoto wadogo ifikapo mwaka 2030. Ili kuweza kufikia maamuzi haya kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa: kuaminiana, kutekeleza sera na mikakati iliyokwisha kuibuliwa pamoja na kuwajibika kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu.

Kikundi cha Mtakatifu Martha ni taasisi ya kimataifa inayopaswa kuigwa katika mapambano dhidi ya biashara ya binadamu, utumwa mamboleo na mifumo yote ya unyonyaji, ili kuwahudumia waathirika, kwa kulinda na kuheshimu utu wao pamoja na kuwarejeshewa uhuru ambao walikuwa wamepokwa na watesi wao kwa kuwageuza kuwa watumwa. Ni taasisi ambayo imeweza kwa mwanga wa Injili kufunua kashfa na madonda yanayodhalilisha utu wa binadamu; ili kuanza kuyaganga na kuyaponya, tayari kuanza kuandika historia mpya ya maisha katika utu na heshima ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!

05/06/2018 10:10