2018-06-05 15:06:00

Maandalizi ya mkutano wa G7,tarehe 8-9 Juni 2018 huko Quebec, Canada!


Ripoti ya Taasisi ya Maendeleo ya Nchi za Nje ya Uingereza imesema mataifa ya G7 yanatumia dola bilioni 100 kila mwaka kuendeleza utumiaji wa mafuta, gesi na makaa ya mawe, licha ya kuahidi kusita ifikapo mwaka 2025. Ripoti hiyo imetolewa Jumatatu kuelekea mkutano wa kilele wa mataifa yaliyoendelea kiviwanda duniani wa kundi la G7 utakaofanyika nchini Canada, kuanzia 8-9. Juni 2018.

Uingereza, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Japan na Marekani - mataifa yanayojulikana kama kundi la G7,  yalitoa ahadi mnamo mwaka 2016 kusitisha kuunga mkono utumiaji wa nishati za asili ifikapo mwaka 2025. Lakini utafiti uliongozwa na Taasisi ya Maendeleo ya Nchi za Nje ya Uingereza (ODI) umegundua kwamba mataifa hayo yanatumia takriban dola bilioni 100 kila mwaka kuendeleza utumiaji wa nishati asilia nchini mwao na nje ya nchi zao katika mwaka 2015 na 2016.

Licha ya kundi la G7 kuahidi kupunguza utumiaji wa nishati asilia, lakini hawana mfumo wowote wa kuhakikisha uwajibikaji wa kutimiza ahadi hiyo na hawana muongozo au miango yoyote, kwa mujibu wa Shelagh Whitley, mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo, akizungumza na vyombo vya habari. Watafiti wa ripoti hiyo wametengeneza orodha ya kila nchi na jinsi inavyoelekea kuachana na utumiaji wa nishati hizo asilia. Ufaransa inaongoza kwa kupata alama 63 kati ya 100, ikifuatiwa na Ujerumani iliyopata alama 62, Canada ni ya tatu kwa kupata alama 54 na Uingereza imepata alama 47.

Marekani ndiyo ya mwisho kwa kupata alama 42 kati ya 100, kutokana na kwamba, nchi hiyo inaunga mkono utumiaji wa nishati asilia na ilijitoa kutoka katika makubaliano ya kimataifa ya kupambana na kitisho cha mabadiliko ya tabianchi. Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza mwaka mmoja uliopita kujitoa katika makubaliano hayo yaliyoafikiwa na takriban nchi 200. Wawekezaji wahimiza mataifa ya G7 kupambana na mabadiliko ya tabianchi. Wakati huo huo, makampuni kadhaa makubwa ya uwekezaji, ikiwamo kampuni ya Ujerumani ya Allianz Global Investors, yamewahimiza viongozi wa mataifa hayo saba yaliyostawi zaidi kiviwanda (G7) kuongeza juhudi za kupambana na suala la mabadiliko ya tabianchi na kutimiza ahadi ya kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kwa kuachana kabisa na utumiaji wa makaa ya mawe. 

Kundi la wawekezaji wapatao 288 limesema katika taarifa yake, kwamba mabadiliko ya utumiaji wa nishati safi yapo njiani, lakini serikali zinahitaji kuongeza juhudi. Hata hivyo wito huo wa wawekezaji unategemewa kupuuzwa na Marekani. Rais Donald Trump amesema wazi kwamba angependa kuimarisha sekta ya nishati ya makaa ya mawe na gesi, na kuonyesha mashaka juu ya utafiti wa kisayansi wa mabadiliko ya tabia nchi.

Na Sr Angela Rwezaula 
Vatican News








All the contents on this site are copyrighted ©.