Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Kardinali Miguel O. Bravo, mtetezi wa wanyonge, amepumzika kwa amani!

Kardinali Miguel Obando Bravo enzi ya maisha yake alisimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! - REUTERS

05/06/2018 09:08

Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Kardinali Miguel Obando Bravo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Managua, nchini Nicaragua, kilichotokea, Jumapili tarehe 3 Juni 2018, wakati Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu. Amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 92. Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake za rambi rambi alizomwandikia Kardinali Leopoldo Josè Brenes Solòrzano, wa jimbo kuu la Managua, anamwomba, kuwafikishia salam zake za rambi rambi kwa: Wasalesiani wa Don Bosco, ndugu, jamaa na wale wote walioguswa na kutikiswa kwa msiba huu mzito.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Hayati Kardinali Miguel Obando Bravo, katika maisha na utume wake, amekuwa ni kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza; akajifunga kibwebwe kwa uaminifu na ujasiri mkuu kumtumikia Mwenyezi Mungu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu anamwombea Marehemu Kardinali Bravo, ili Kristo mchungaji mwema, aweze kumpokea na hatimaye, kumvisha taji la utukufu lisiloharibika kamwe!

Marehemu Kardinali Miguel Obando Bravo alizaliwa tarehe 2 Februari 1926, baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 10 Agosti 1958. Mwaka 1968 akateuliwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki la Matagalpa. Kunako mwaka 1970 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Managua, nchini Nicaragua. Mwaka 1985 akateuliwa na kusimikwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Kardinali na tarehe 1 Aprili 2005 akang’atuka kutoka madarakani na mazishi yake, yamefanyika tarehe 4 Juni 2018 kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Managua.

Kardinali Leopoldo Josè Brenes Solòrzano katika Ibada ya Misa Takatifu, amemkumbuka Marehemu Kardinali Bravo kama kiongozi aliyesimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu. Ni muasisi na msanii wa mchakato wa upatanisho kitaifa nchini Nicaragua. Alijipambanua kama kiongozi jasiri na mpenda haki, amani na maradhiano kati ya watu. Licha ya kutoka katika familia ya wakulima, lakini alibahatika kuwa na kipaji cha akili, kilichomwezesha kucharuka katika masomo ya hisabati na fizikia, kiasi hata cha wanafunzi wake, “kumvulia kofia, kila mara walipokuwa wanamwona akiingia darasani”.

Alisimama kidete kuwatetea wanyonge, huku akitekeleza moto yake ya kiaskofu inayosema kwamba, “Amekuwa yote kwa ajili ya wote”. Kamwe hakupatana na vitendo vya rushwa na ufisadi, akavikemea kwa nguvu zote, si tu kwa maneno, bali hata kwa vitendo. Ni kiongozi aliyefahamu kwamba, changamoto katika maisha zinaweza kutatuliwa kwa njia ya majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi na wala si kwa njia ya mtutu wa bunduki! Kwake, Injili ya haki, amani na upatanisho, vilipewa kipaumbele cha pekee! Marehemu Kardinali Miguel Obando Bravo “alikuwa vizuri” kwa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, kiasi hata cha kuthubutu kutekeleza kwa vitendo “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” kwa kuitisha na kuadhimisha Sinodi ya kwanza ya Jimboni mwake, ili kuwashirikisha watu wa Mungu kuhusu kweli za Kiinjili na Mafundisho ya Kanisa yanayoweza kuwasaidia waamini kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Miguel Obando Bravo ndiye Kardinali wa kwanza kabisa kuteuliwa kutoka Amerika ya Kusini. Siku aliporejea kutoka Vatican baada ya kusimikwa rasmi kuwa Kardinali, nchi nzima ya Nicaragua, ikatetema kwa furaha na shangwe. Kunako mwaka 1987 Mtakatifu Yohane Paulo II akamwalika kuandika Tafakari ya Njia ya Msalaba kuzunguka Magofu ya Coloseo wakati wa Ijumaa Kuu.

Ni kiongozi aliyesimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya haki, akataka Jamii ijengwe kwenye msingi ya amani, usawa, upendo na mshikamano ili kuondokana na tabia ya kuwa na maamuzi mbele pamoja na ubaguzi, mambo yanayovuruga umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii. Kwake, deni la nje, lilipaswa pia kuangaliwa kwa miwani ya kimaadili katika ujumla wake, kwani madhara yake ni makubwa kwa maskini na wanyonge katika jamii! Kwa ufupi hivi ndivyo Kardinali Miguel Obando Bravo anavyokumbukwa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

05/06/2018 09:08