2018-06-04 14:20:00

Papa: Majadiliano ya Kiekumene: Ekaristi Takatifu na Huduma ya Kanisa


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 4 Juni 2018 amekutana na kuzungumza na wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Kanisa la Kiinjili la Kiluteri nchini Ujerumani pamoja na wajumbe wa Umoja wa Makanisa ya Kiluteri nchini Ujerumani. Imekuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kukumbushia maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani, iliyofanyika kunako mwaka 2016 na kupata nafasi ya kushiriki katika tukio hili la kihistoria huko Lund, nchini Sweden, tarehe 31 Oktoba 2016, ili kujenga umoja wa kidugu, kwa kuganga na kuponya madonda ya utengano.

Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu aliyewawezesha Wakristo kuweza kukutana tena kwa pamoja baada ya “miaka 500 ya patashika nguo kuchanika”, lakini katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, kumekuwepo na maendeleo makubwa ya umoja wa Wakristo unaoendelea kukua na kupanuka. Hii ni kazi ya Roho Mtakatifu, anayewawezesha ndugu kukutana mintarafu mantiki ya Injili kuliko hata mipango ya binadamu.

Kumekuwepo na mafanikio makubwa katika majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa la Kiinjili la Kiluteri pamoja na Kanisa Katoliki; hali ambayo imesaidia sana kuvuka maamuzi mbele. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, majadiliano haya kwa siku za usoni, yataweza kuvuka vikwazo na hatimaye, kudumisha umoja miongoni mwa Wakristo! Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani yamekuwa ni fursa kwa Makanisa kuendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene katika sala, ili kuweza kumwilisha mpango wa Roho Mtakatifu anayetoa dira, mwongozo na mwanga wa kufuatilia utekelezaji wake.

Roho Mtakatifu anaendelea kuwasukuma Wakristo kujenga mshikamano wa upendo, kwa kupendana kwani wamezaliwa upya kwa njia ya Neno la Mungu. Kwa pamoja wanahamasishwa kushikamana katika huduma ya upendo kwa: maskini, watu wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Uekumene wa damu kiwe ni kikolezo cha umoja wa Wakristo unao onekana. Wakristo wanapaswa kuendeleza mshikamano wa majadiliano ya kitaalimungu kwa kutembea kwa pamoja, katika hali ya uvumilivu, daima wakimwangalia Mwenyezi Mungu. Fumbo la Ekaristi Takatifu na Huduma ya Kikanisa ni tema zinazopaswa kupewa uzito wa pekee katika majadiliano ya kiekumene, ili kuweza kufikia muafaka!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, majadiliano ya kiekumene, yawahusishe Wakristo wengi zaidi, ili kwa pamoja waweze kukua na kukomaa kama Jumuiya ya waamini wanaosali, wanaopendana, wanaotangaza na kushuhudia kwa pamoja Habari Njema ya Wokovu. Kwa njia hii, Wakristo kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu wataweza kutambua ufunuo wa Kimungu, unaoendelea kufahamika zaidi kwa kumfahamu na kumpenda kwa pamoja Kristo Yesu, ambaye ni utimilifu wa Ufunuo wa Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amemwomba Kristo Yesu, aweze kuwasindikiza, ili kwa kuwa Wakristo, waweze kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu, wajasiri katika utume, ili huduma ya shughuli za kichungaji inayotolewa ijengwe katika msingi wa moyo wa kiekumene.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.