2018-06-04 08:15:00

Papa Francisko: Ekaristi Takatifu ni kifungo cha upendo!


Waamini wa Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, Jumapili, tarehe 3 Juni 2018 wameadhimisha kwa: Ibada, uchaji na kishindo Sherehe ya Ekaristi Takatifu, yaani Mwili na Damu Azizi ya Kristo, “Corpus Domini” au “Corpus Christi” kwa lugha ya Kilatini. Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha Sherehe hii kwenye Parokia ya Mtakatifu Monica, huko Ostia, nje kidogo ya mji wa Roma. Baada ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ameongoza maandamano ya Ekaristi Takatifu na kuhitimishwa kwenye Parokia ya “Nostra Signora di Bonaria” kwa baraka ya Sakramenti kuu. Baba Mtakatifu katika mahubi yake amekazia umuhimu wa maandalizi, mahali na chakula ili kushibisha njaa ya watu wa Mungu kwa njia ya upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu amefafanua kwamba, Yesu aliwaandalia wafuasi wake mahali pa kushiriki Karamu ya Mwisho, kama ilivyokuwa hata baada ya ufufuko wake, alipowaandalia Mitume wake mkate na samaki wa kuchoma, huku akiwataka hata wao nao kushiriki kikamilifu katika tukio hili, lakini kwa msisitizo zaidi, Yesu aliwaambia wafuasi wake kwamba, anakwenda kuwaandalia makao. Injili ni chumba maalum kilichopambwa na Kanisa kwa ajili ya kuwashirikisha watu wote ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, ili baada ya maisha ya hapa duniani, waweze pia kushiriki furaha ya mbinguni.

Kristo Yesu, amewaandalia waja wake chakula maalum: Mwili na Damu yake Azizi. Waamini wamepewa zawadi kubwa mbili: Injili Takatifu na Chakula cha maisha ya kiroho; zawadi zinazofumbatwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Huu ni Mkate wa milele ulioshuka kutoka mbinguni unaozima matumaini ya waja wake na kuchochea ndoto na matamanio halali ya waamini. Kristo Yesu katika Ekaristi Takatifu amejitoa mwenyewe kuwa ni masurufu ya njiani kuelekea kwenye maisha ya uzima wa milele.

Katika Ekaristi Takatifu, Yesu anawaandalia waja wake chakula kinachorutubisha: miradi, mahusiano na mafungamano; matamanio halali na matumaini yasiyofifia hata kidogo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mwanadamu anayo njaa ya kutaka kupendwa zaidi, ambayo kamwe haiwezi kuzimwa kwa zawadi au maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Ekaristi Takatifu,  ni chakula cha kawaida, kina uwezo wa kuzima kiu ya upendo mkubwa kutoka kwa Kristo Yesu, aliyejisadaka mwenyewe pale Msalabani kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma na upendo wa Baba. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, waamini wanashiriki maisha, wanaonja upendo na kuendeleza Fumbo la Pasaka katika uhalisia wa maisha yao kwani Yesu aliteswa, akafa na kufufuka kwa ajili ya kila mmoja wao!

Waamini wanapoadhimisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, wanabahatika kukutana na Kristo Yesu na kumpokea Roho Mtakatifu na wanajaliwa kupata amani na furaha ya ndani. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuchagua chakula hiki cha maisha ya kiroho, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu; waendelee kugundua utajiri wa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu katika Jumuiya zao. Wamwombe Kristo Yesu, aweze kuwajalia ile njaa ya uwepo wa Mungu katika maisha yao, njaa inayoshibishwa kwa njia ya Ekaristi Takatifu.

Hata leo hii, Yesu anawataka wafuasi wake kumwandalia mahali ambapo ataweza kula Karamu pamoja nao! Pawe ni mahali pa kuwakutanisha watu wote bila ubaguzi, lakini zaidi kwa watu waliokata tamaa, ili aweze tena kuwawashia moto wa matumaini! Hawa ndio wale maskini wasiokuwa na makazi maalum, wanaoteseka na kufa kwa baa la njaa. Watu wanaoishi katika upweke hasi, wanaoteseka na kusumbuka kwa sababu mbali mbali za maisha; wote hawa anasema Baba Mtakatifu ni sawa na Tabernakulo iliyotelekezwa! Kwa wale wote wanaoshiriki Ekaristi Takatifu wanapaswa kuwa ni mkate unaomegwa kwa ajili ya “akina yakhe pangu pakavu, tafadhali tia mchuzi”. Ekaristi Takatifu iwashe moto wa mapendo duniani, wa kuondokana na ubinafsi, tayari kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii.

Baba Mtakatifu anawataka waamini wawe na ujasiri wa kumwandalia Yesu mahali pa kuadhimisha Karamu katika miji yao! “Ostia” maana yake ni “Mlango”. Hii ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumfungulia Kristo malango ya maisha yao: kwa kuvunjilia mbali kuta za utengano na hali ya kutowajali wengine; kwa kuondokana na anasa, jeuri na kiburi, ili kufungua malango ya haki, nidhamu na utawala wa sheria. Baba Mtakatifu anakaza kusema, “Ostia” ni kielelezo cha uzuri unaoitaka familia ya Mungu kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa maisha, kwa kuondokana na woga usiokuwa na mashiko pamoja na dhuluma. Ekaristi Takatifu inawaalika waamini, kujiachilia mikononi mwa Kristo Yesu, aweze kuwasomba kwa mawimbi yake ili kuonja: uhuru, ujasiri na umoja.

Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha waamini kwamba, kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu baada ya kushiriki Karamu ya Mwisho, waliondoka na hata wao, watashiriki katika maandamano makubwa ya Ekaristi Takatifu. Yesu anataka kukaa kati pamoja na waja wake. Anataka kutembelea hali mbali mbali za maisha ya familia ya Mungu; anataka kuingia katika nyumba ili awapatie huruma inayookoa; aweze kuwabariki na kuwafariji.

Baba Mtakatifu anawakumbusha wenyeji wa Ostia na vitongoji vyake kwamba, hivi karibuni wameguswa na kutikiswa na matukio ambayo yameacha kurasa chungu katika maisha yao; sasa Yesu anataka kuwa karibu nao! Kumbe, ni wajibu wao kumfungulia Yesu malango ya nyoyo zao, familia na mji wao. Ni muda wa kumshukuru Yesu kwani anawaandalia Karamu na chakula cha maisha ya uzima wa milele, anawataka kuwashirikisha katika Ufalme wake, ili hatimaye, waweze kumpeleka Yesu kwa jirani zao kwa sababu Yesu ni chemchemi ya furaha, maisha, udugu, haki na amani inayoapaswa kutawala katika barabara na mitaa yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.