Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Sala ya Malaika wa Bwana

Mwenyeheri Sr. Maria Crocifisa wa Upendo wa Mungu, Mwanamke wa shoka

Mwenyeheri Sr. Maria Crofisa wa upendo wa Mungu ni mwamke aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya elimu kwa watoto maskini! - RV

04/06/2018 08:48

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 3 Juni 2018, amemkumbuka Mwenyeheri Sr. Maria Crocifisa wa Upendo wa Mungu, aliyekuwa anajulikana kama Maria Gargani, Muasisi wa Shirika la Watawa Mitume wa Moyo Mtakatifu wa Yesu aliyetangazwa kuwa Mwenyeheri, Jumamosi, tarehe 2 Juni 2018 huko Napoli, Kusini mwa Italia, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu.

Baba Mtakatifu amekazia kwamba, Mwenyeheri Sr. Maria Crocifisa alikuwa ni binti wa kiroho wa Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina. Ni Mama wa shoka na mtume hodari aliyejisadaka bila  ya kujibakiza katika sekta ya elimu na huduma ya maisha ya kiroho parokiani. Kwa maombezi na mfano wa maisha yake, awasaidie na kuwatia shime mabinti wake wa kiroho pamoja na wadau mbali mbali katika sekta ya elimu. Tangu mwanzo wa maisha yake, alionesha Ibada maalum kwa Ekaristi Takatifu na Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya huruma na upendo wa Kimungu!

Kardinali Angelo Amato anasema, Mwenyeheri Sr. Maria Crocifisa alibahatika kuzaliwa na kulelewa kwenye familia iliyokuwa na uwezo mkubwa kielimu, kiasi kwamba, katika maisha yake, akajikita zaidi katika kufundisha Katekesi na elimu dunia kwa watoto waliokuwa wanatoka kwenye familia maskini! Daima alimwomba Kristo Yesu, aweze kutekeleza mapenzi yake katika maisha ya huduma kwa watoto! Ili kuweza kutekeleza hamu ya moyo wake, akajiweka wakfu kwa Kristo Yesu na kujiunga na Chama cha Vijana Wakatoliki na Mtawa katika Utawa wa Tatu wa Mtakatifu Francisko.

Katika maisha na utume wake, akawa ni shuhuda wa imani iliyomwilishwa katika medani mbali mbali za maisha, lakini zaidi katika sekta ya elimu na huduma makini ya elimu kwa watoto vijijini. Akabahatika kuwa ni msanii mzuri aliyeweza kuunganisha sala na tafakari iliyomwilishwa katika huduma. Kwa njia ya ushuhuda wa maisha ya sala iliyomwilishwa katika huduma, akawa ni mfano bora wa kuigwa na jirani zake. Kunako mwaka 1916 akabahatika kukutana na Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina na huo ukawa ni mwanzo wa mawasiliano na mahali pa kujichotea hekima, neema na utajiri wa maisha ya kiroho.

Mwenyeheri Sr. Maria Crocifisa, katika safari ya maisha yake, alipambwa kwa namna ya pekee na fadhila ya upendo; akateseka sana ili kuanzisha Shirika ambalo lingesaidia kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya Kikristo. Kunako mwaka 1936 akaanzisha Shirika lililojikita katika elimu ya awali na sekondari; ufundi kwa wasichana na wanawake na baadaye, akaanzisha taasisi ya elimu kwa ajili ya kuwaandaa waalimu, wafanyakazi parokiani, waimbaji na wahudumu wa maskini, wagonjwa na wale wote waliokuwa kufani! Kunako mwakqa 1945 Maria Gargani akakubaliwa kuwa Mtawa na kupewa jina la Sr. Maria Crocifisa wa Upendo wa Mungu.

Baada ya miaka mingi ya taabu na mahangaiko ya ndani kunako mwaka 1956 Shirika likaidhinishwa na Sr. Maria Crocifisa wa Upendo wa Mungu akawa ni muasisi na Mama mkuu wa Shirika hadi mwaka 1971 na kunako mwaka 1973 akafariki dunia. Urithi, amana na utajiri wake wa maisha ya kiroho, umefumbatwa katika Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

04/06/2018 08:48