2018-06-04 09:27:00

Hija ya Masalia ya Mtakatifu Yohane XXIII yasaidie kuamsha mambo mema


Baba Mtakatifu Francisko baada ya sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 3 Juni 2018, alipenda kuungana na familia ya Mungu Jimbo Katoliki la Bergamo chini ya Askofu Francesco Beschi. Jumapili, tarehe 3 Juni 2018 wakiwa Parokiani “Sotto il Monte” wamekumbuka na kuadhimisha siku ambayo Mtakatifu Yohane XXIII alipofariki dunia. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, hija ya masalia ya Mtakatifu Yohane XXIII huko Bergamo yatasaidia kuamsha tena moyo wa ukarimu na matendo mema!

Itakumbukwa kwamba, Bergamo huko ndiko mahali ambapo Papa Yohane wa XXIII alikozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu; akabahatika kupata wito na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mtakatifu Yohane XXIII alikuwa anasema daima kwamba, urithi mkubwa ambao kamwe hawezi kusahau katika maisha yake ni mambo msingi aliyofundishwa nyumbani kwao; kwa njia ya mifano bora ya wazazi, ndugu, jamaa na majirani zake. Ndiyo maana daima alitamani kurejea nyumbani kwao kwa mapumziko, ili kujichotea utajiri na ushuhuda wa maisha ya  na mifano bora ya waamini.

Tangu mwanzo wa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, watu mbali mbali waliweza kushuhudia utakatifu wa maisha kama kielelezo cha uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Ni kiongozi aliyefundisha kwa mifano na maisha yake wema, uzuri na utakatifu wa maisha ya kifamilia; akapandikiza mbegu ya Injili ya matumaini kwa wale waliokata tamaa ya maisha, ili kujikita katika uzuri na wema . Aliwataka waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya amani, upendo na mshikamano wa dhati na kwamba, watoto walikuwa ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, walipaswa kulindwa, kuendelezwa na kufarijiwa katika shida na mhangaiko yao mbali mbali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.