Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Maandamano ya Ekaristi Takatifu yakuze: Toba, wongofu, haki na amani

Maandamano ya Ekaristi Takatifu yasaidie kukuza: Toba na wongofu wa ndani; haki, amani na utakatifu wa maisha! - REUTERS

31/05/2018 08:39

Imani ni ile hali ya kukutana na Kristo Yesu, Mungu kweli na mtu kweli, kisha kujiaminisha kwake katika maisha. Kawaida ya kila kukutana, kuna suala la kumtambua unayekutana naye, kisha kufuatia mtazamo wa uhalisia wa uliyekutana naye, unajipima kujitambua binafsi wewe ni nani, upo vipi, na unatarajia nini maishani mwako. Pengine kukutana katika tukio fulani, kwa wakati fulani, na mahala fulani ni mwanzo tu wa kufahamiana. Baada ya hapo, huwa kuna kufahamiana zaidi kadiri siku zinavyoenda. Kufahamiana huku vema kunategemea sana mahusianao ya karibu na kudumu, mahusiano ya heshima, upendo na urafiki.

Kristo alijifanya mwili ili kurudisha mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu. Mahusiano ya upendo ambayo mwanadamu aliyapoteza katika bustani ya edeni kwa kutenda kinyume na maagizo ya Mwenyezi Mungu (Rej., Mwanzo 3:24). Hivyo Kristu kwa sadaka yake msalabani anampatanisha tena mwandamu na Mungu, lakini ili abaki katika mahusiano hayo ya upendo na muumba wake, mwanadamu anapaswa adumu katika imani, kama mtume Paulo asemavyo: “Na ninyi mliokuwa hapo kwanza mmetengwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa (…) ili awalete ninyi mbele zake, watakatifu, wasio na mawaa wala lawama; mkidumu tu katika ile imani” (Rej., Wakolosai 1: 21 – 23).

Bila shaka ndugu msikilizaji katika maisha yako kuna tukio ambalo liliisha kukukutanisha na Kristo, ambapo ukajichotea hazina hiyo ya imani. Katika tafakari hii, napenda kukushirikisha namna mojawapo ya kukusaidia kudumu katika mahusiano naye kwa imani thabiti; nayo namna hiyo ni ibada kwa Ekaristi Takatifu.

Kawaida unapompenda mtu unatamani kuwa naye kila wakati, au walau kuwa naye muda mwingi zaidi. Hii ni kwa sababu ya vile vitu vizuri mnavyoshirikishana na furaha mnayoipata katika kuwa pamoja kama wapenzi, ndugu, jamaa ama marafiki. Kristu angali akijua ya kuwa saa ya kurudi kwa Baba yake imewadia, hakupenda kupoteza kabisa mahusiano ya urafiki na upendo alionao kwa wanafunzi wake, hivyo akapenda kubaki pamoja nao katika maumbo ya mkate, kwani aliwapenda upeo (Rej., Yohane 13:1).

Ni wazi kwamba Kristo anaishi katika mahusiano ya kiroho na waamini kama asemavyo mwenyewe “mtu akinipenda, atalishika Neno langu, na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake” (Yohane 14:23). Hata hivyo mbali ya uwepo huo kiroho, amependa kubaki pia katika uwepo halisi wa kifizikia, ingawa katika mafumbo ya mkate na divai.

Uwepo huu una maana kubwa kwako mwamini kwa sababu mbali ya kumtambua kuwa yeye kwako ni rafiki (Rej., Yohane 15:15), unamtambua pia kuwa ni Muumba wako, ambaye anajidhihirisha uweza wake kwa kujificha katika maumbo ya mkate na divai, lakini ni Yeye yule. Hivyo unapofika katika fumbo kubwa la namna hii, la kumtambua mwanakondoo wa agano jipya aliyejitoa sadaka kwa ajili ya wokovu wako, unapaswa umkiri kwa dhati kabisa kwamba “astahili mwanakondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na Baraka” (Ufunuo 5:12).

Huu ndio mwaliko wa ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu, kuukiri ukuu wake na uweza wake wa kukutakasa na dhambi na kukuokoa na mauti, ili uweze kuimba utenzi wa zaburi pamoja na Mfalme Daudi “Ee nafsi yangu umhimidi Bwana, wala usizisahau fadhili zake zote. Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote, aukomboa uhai wako kutoka kwa kaburi, akutia taji la fadhili na rehema” (Zaburi 103: 2- 4).

Maandamano ya Ekaristi Takatifu ni ushuhuda dhahiri wa kumtambua kuwa Kristo ndiye Mfalme wa wafalme na ana mamlaka zote duniani na mbinguni (Rej., Mathayo 28:18). Katika barabara za makazi na sehemu za shughuli za kila siku, Kristu anapita katika maandamano hayo ili kutakasa maeneo yote hayo, ili kuuthibitisha ufalme wake, ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na wa neema, ufalme wa haki, mapendo na amani.

Kumbe, maandamano ya waamini pamoja na Ekaristi Takatifu, yalenge katika maombi na juhudi binafsi za kushiriki pamoja na Kristu kuufanya ufalme wa namna hiyo ujidhihirishe kati ya watu. Ni maandamano ambayo kutoka kwayo, waamni wanachota neema za umoja na mshikamano kati yao, ndani ya Kristu Yesu. “Nasema kama na watu wenye akili, lifikirini ninyi ninenalo (…) Mkate ule tuumegao, je si ushirika wa mwili wa Kristu. Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja, kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja” (IWakorintho 10:15 – 18).

Mbali na ibada hiyo ya wazi na maandamano, yafaa sana kujifunza ibada binafsi kwa Ekaristi Takatifu. Ni fursa ya kuzungumza na Bwana, Mwalimu na Rafiki, ambaye kakupenda kiasi cha kuamua kubaki kati yetu katika fumbo hili kubwa namna hii. Unapoijongea Ibada ya Ekaristi Takatifu katika utulivu wa nafsi, Kristo anathamini sana utambuzi wako wa uwepo wake halisi katika Sakramenti kubwa hiyo.

Mwenyezi Mungu, katika Nafsi yake ya pili, anapenda kuzungumza nawe katika utulivu wa ndani kama alivyofanya kwa nabii Eliya katika mlima wa Bwana, mlima Horebu, na kukupatia utume, yaani kile ambacho angependa utende katika siku hiyo, juma hilo, mwezi, mwaka au nyakati fulani (Rej., IWafalme 19: 11-16). Katika altare ama tabernaklo alipo Kristo katika maumbo hayo ya mkate, na katika muungano na dhamiri yako, ndipo ulipo huo mlima Horebu, mlima wa Bwana. Iwapo kuna jambo lolote linakutatiza, iwapo kuna furaha yeyote ya kumshirikisha, iwapo kuna kubwa lolote ungependa libadilike, katika nia njema na kadiri ya mapenzi yake, atakuongoza ujue la kufanya ili mpango wake wa wokovu uweze kufanikiwa, wanadamu waokoke na Mwenyezi Mungu atukuzwe.

Katika Ibada hiyo ya Ekaristi, unaunganika naye Yeye aliyependa kubaki hapa duniani ili adumu katika umoja nawe. Ni katika muunganiko huo anaitakasa roho yako iliyokwishakuungama dhambi na kutimiza malipizi, kisha anakupatia nguvu yake ili unene na utende kama Yeye kiasi cha kujitambua na kukiri “si mimi tena ninayeishi, bali Kristo yu hai ndani yangu” (Rej., Wagalati 2:20).

Uwezo wako wa kunena kwa hekima na kutenda kwa mafanikio utatokana na ile neema uipatayo katika muunganiko na Ekaristi Takatifu, kama asemavyo mtakatifu Theresa wa Lisieux kwamba: kutazamana kwa macho ya ana kwa ana na Kristu ndiyo muungano na utajiri wa kina zaidi. Ndugu msikilizaji, nakualika umkaribie Yesu wa Ekaristi, umtazame naye akukazie macho, msemezane, ili akuinue katika muungano wa kina naye na kujichotea utajiri wa neema zinazobubujika kutoka kwake.

Nakutakia maadhimisho mema ya Sherehe ya Mwili na Damu ya Kristo Yesu.

Na Pd. Celestine Nyanda

Vatican News.

31/05/2018 08:39