2018-05-29 07:38:00

Changamoto za maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Bangladesh


Baraza la Maaskofu Katoliki Bangladesh chini ya uongozi wa Kardinali Patrick D’Rozario, Rais wa Baraza linaloundwa na Majimbo makuu mawili yaliyogawanyika katika majimbo saba, limehitimisha hija yake ya kitume, inayofanyika mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano. Imekuwa ni fursa ya kukutana na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na waandamizi wake; kusali na kutafakari kuhusu maisha na utume wa Kanisa nchini Bangladesh.

Baraza hili lilianzishwa kunako mwaka 1971 na Shirika la Misaada ya Kanisa Katoliki Bangladesh, ndicho chombo chake kikuu cha huduma ya huruma na upendo kwa ya familia ya Mungu nchini humo! Idadi ya waamini wa Kanisa Katoliki ni ndogo sana, ikilinganishwa na waamini wa dini ya Kiislam. Kanisa linamshukuru Mungu kwa idadi kubwa ya miito anayoendelea kulijalia Kanisa. Maaskofu wanasema, licha ya idadi ndogo ya waamini wa Kanisa Katoliki nchini Bangladesh, lakini Kanisa limekuwa mstari wa  mbele katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu nchini Bangladesh.

Caritas Bangladesh, kimekuwa ni chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa wananchi wote wa Bangladesh wakati wa majanga asilia. Ni chombo ambacho kinaendelea kupata ushirikiano kwa Mashirika mbali mbali ya Misaada ya Kanisa Katoliki, ili kuwahudumia watu wote pasi na ubaguzi, jambo la msingi ni utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi kama sehemu muhimu sana ya Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Majadiliano ya kidini ni kati ya changamoto pevu ambazo Kanisa Katoliki nchini Bangladesh inakabiliana nazo kutokana na ukweli kwamba, kuna baadhi ya waamini wa dini ya Kiislam wanayo misimamo mikali ya kidini na kiimani, hali ambayo ni hatari sana katika mchakato wa kukuza na kudumisha: haki, amani na maridhiano kati ya watu; umoja, mshikamano na mafungamano ya jamii kitaifa. Kumekuwepo na uporaji wa maeneo makubwa ya ardhi kutoka kwa maskini, hali ambayo imeendelea kudhalilisha utu na heshima ya watu nchini Bangladesh pamoja na uvunjwaji mkubwa wa haki msingi za binadamu.

Vitendo vya kigaidi, uhuru wa kidini pamoja na uhuru wa watu kujieleza kadiri ya Katiba ya nchi ni kidogo sana na matokeo yake, kumekuwepo na: mashambulizi ya mara kwa mara na hujuma kwa Kanisa na viongozi wake. Licha ya changamoto zote hizi, Kanisa Katoliki kwa kushirikiana na Makanisa mengine, linaendelea kujizatiti katika majadiliano ya kidini la Baraza la Waamini wa Dini ya Kiislam nchini Bangladesh lijulikanalo kama Bangladesh Jamiatul Ulama. Katika historia yake, Bangladesh kunako mwaka 1970 ilitembelewa na Mwenyeheri Paulo VI.

Mwaka 1973 Bangladesh ikaanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Vatican. Mwaka 1985 Baraza la Maaskofu Katoliki Bangladesh likafanya hija ya kitume mjini Vatican na kukutana na Mtakatifu Yohane Paulo II aliyekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa maisha ya kiroho kati ya Wakristo na Waislam, kwani wote wanamwamini Mungu mmoja, mwingi wa huruma na mapendo. Ni wajibu na dhamana na waamini wa dini mbali mbali nchini Bangladesh kujikita katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika: haki, amani, maridhiano; uhuru, haki jamii pamoja na tunu msingi za maisha ya kiroho. Huu ndio unapaswa kuwa ni ushuhuda wa Kikristo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya wananchi wa Bangladesh, ili kujenga amani, maridhiano na udugu na umoja wa kitaifa!

Kunako mwaka 1986 Mtakatifu Yohane Paulo II akafanya hija ya kichungaji nchini Bangladesh na kutumia fursa hii kuhimiza: ari na moyo wa upendo wa kidugu; tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili; kwa kuheshimu imani na mapokeo ya dini mbali mbali nchini Bangladesh, ili kudumisha umoja na udugu, haki, amani na maridhiano. Baba Mtakatifu Francisko mwaka 2017 akatembelea Bangladesh kwa kukazia zaidi majadiliano ya kidini kama njia muafaka ya ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki, amani na maridhiano. Akaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwajali na kuwatunza watu kutoka jamii Rohingya, waliofukuzwa kutoka nchini Myanmar, kwani hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Papa Francisko akawataka Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanawashirikisha waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kutambua na kuheshimu karama na mapaji waliyokirimiwa na Roho Mtakatifu. Akalitaka Kanisa kuendelea kuwa ni chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ndio ushuhuda wa maisha na utume wa Kanisa wenye mvuto na mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.