2018-05-28 08:55:00

Papa Francisko kutembelea Sicilia, Kusini mwa Italia, 15 Septemba 2018


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa kufungua mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, Jumatatu, tarehe 21 Mei 2018 amesema, kwa hakika, Bikira Maria ni Mama wa Kanisa, anayewafanya viongozi wa Kanisa kusikia na kutambua uwepo wake kati yao, wanapokutana kujadiliana masuala msingi katika maisha na utume wa Kanisa. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, waamini wataendelea kutambua na kuthamini: Ibada kwa Bikira Maria na Umama wa Kanisa.

Katika mkutano huu, Baba Mtakatifu amewaambia Maaskofu kwamba, kuna mambo makuu matatu yanayomkera sana moyoni mwake. Mosi: ni kuteteleka kwa miito mitakatifu ndani ya Kanisa;  Pili, ni ukosefu wa ufukara wa kiinjili na uwazi katika matumizi ya rasilimali ya Kanisa inayopaswa kutumika kama kikolezo cha mchakato wa uinjilishaji na tatu ni kupunguza utitili wa majimbo kwa kuunganisha baadhi yao!

Baba Mtakatifu kwa kutambua na kuthamini ushuhuda wa Kiinjili uliotolewa na Mwenyeheri Pino Puglisi katika, Jubilei ya Miaka 25 tangu alipouwawa kikatili, tarehe 15 Septemba 2018 atafanya hija ya kichungaji katika Majimbo ya Piazza Armerina na Palermo, yaliyoko Kusini mwa Italia. Mwenyeheri Giuseppe Puglisi, aliyekuwa Paroko wa Parokia ya Brancaccio, Jimboni Palermo aliuwawa na kikundi cha kigaidi cha Mafia, wakati wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 56 ya kuzaliwa kwake. Mwenyeri Pino Puglisi, alisimama kidete kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kiinjili, kwa kujisadaka katika huduma ya kuwaokoa vijana na watoto waliokuwa wanatumbukizwa katika vitendo vya kigaidi, biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ili kuwapatia matumaini mapya katika maisha.

Hawa ni watoto waliokuwa wanalelewa katika mazingira magumu na hatarishi, kiasi cha kuwa ni hatari kwa jamii kutokana na vitendo vya kinyama walivyokuwa wanafundishwa kutenda. Viongozi wa kikundi cha Mafia wakamwona Padre Pino Puglisi kuwa ni kikwazo katika shughuli zao na hivyo wakaamua kumfutilia mbali, kwanza kabisa kwa kumtishia maisha, lakini baadaye kwa kumtwanga risasi kichwani akiwa mlangoni pa makazi yake. Mwenyeheri Pino aliwaona uso kwa uso watesi wake, kabla hajapigwa risasi akawaambia, “nilitegemea jambo kama hili”! Hii ilikuwa ni chuki dhidi ya imani, “Odium fidei” ndiyo maana Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, tarehe 29Juni 2012 akatangazwa kuwa Mtumishi wa Mungu na tarehe 25 Mei 2013 akatangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Mwenyeheri.

Askofu mkuu Corrado Lorefice wa Jimbo kuu la Palermo anasema, ziara ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko huko Palermo, itawasaidia watu wa Mungu kukuza ari na moyo kimisionari, tayari kutoka ili kutangaza tunu msingi za Kiinjili na kwamba, huu ni ushuhuda kuwa Baba Mtakatifu anathamini mchango wa watoto wa Kanisa wanaojisadaka bila kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili hata katika mazingira magumu na hatarishi. Huu ni mwaliko kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Palermo, kuchuchumilia mambo msingi katika maisha, kwa kusimama kidete kulinda, kutangaza na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kupiga moyo konde na kusonga mbele katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu yuko pamoja na kati yao, akiwatia shime.

Kwa upande wake, Askofu Rosario Gisana wa Jimbo Katoliki Piazza Armerina anapenda kutoa shukrani zake za dhati kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa uamuzi wake wa kutembelea Jimboni mwao ili kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo, hasa katika kipindi hiki kigumu cha athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa. Wananchi wengi wanakabiliwa na hali ngumu ya uchumi.

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, ameendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kutokana na ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaotolewa na watu wa Mungu ndani nje ya Italia. Kati ya mashuhuda hawa wa imani, matumaini na mapendo, wamo; Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina, Mtumishi wa Mungu Askofu Tonino Bello, Don Zeno Saltini, muasisi wa Jumuiya ya Nomadelfia pamoja na Mama Chiara Lubich, muasisi wa Jumuiya ya Wafokolari. Itakumbukwa pia kwamba, mwaka 2017, Baba Mtakatifu Francisko ametembelea na kusali kwenye makaburi ya Don Lorenzo Milani na Don Primo Mazzolari. Hawa ni mashuhuda wa miito mitakatifu, Ufukara wa Kiinjili na watu ambao wametumia karama na mapaji yao kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani, Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.