2018-05-26 15:23:00

Papa: Kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema ni chanzo cha majanga


Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Mfuko wa “Centesimus Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, CAPP, yanaongozwa na kauli mbiu “Sera na mtindo mpya wa maisha katika kipindi cha digitali”. Hii ni kumbu kumbu endelevu tangu Papa Leo XIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Rerum Novarum” yaani “Mambo Mapya” msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II, alitamani sana kuona kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapata hekima inayofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuboresha sera na mikakati ya kiuchumi, biashara na huduma za kijamii. Hii ni changamoto endelevu inayopaswa kuvaliwa njuga na Mama Kanisa katika jukwaa la Jumuiya ya Kimataifa ambamo kuna changamoto changamani zinazoingiliana.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 26 Mei 2018 amekutana na kuzungumza na washiriki wa mkutano wa Kimataifa kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Mfuko wa “Centesimus Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, CAPP. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol amekuwepo na ameshiriki katika kuchangia mada. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amesema, changamoto kubwa inayoendelea kuathiri mfumo mzima wa uchumi ni kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema na matokeo yake ni kushamiri kwa ubinafsi na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine; hali inayoathiri utu na heshima ya familia ya binadamu.

Changamoto changamani za mapambano ya umaskini na mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu zinakwama kutokana na ubinafsi, hali ambayo imejitokeza kwa kiasi kikubwa katika wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Mfuko wa “Centesimus Annus” anasema Baba Mtakatifu Francisko una dhamana na wajibu mkubwa wa kutangaza na kushuhudia ujumbe wa Injili ili kukabiliana na changamoto hizi, ili hatimaye, kulisaidia Kanisa kutekeleza utume wake kiaminifu. Ushirikiano wa karibu na wadau katika sekta ya uchumi na fedha, viongozi wa vyama na mashirikisho ya wafanyakazi pamoja na wafanyakazi wa umma ni muhimu sana ili kuweza kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika maeneo haya.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, kuna mpasuko mkubwa kati ya sayansi na imani, kiasi kwamba, kanuni maadili na utu wema, havina nafasi tena katika masuala ya uchumi na fedha. Matokeo yake ni watu kutafuta faida kubwa zaidi bila ya uwajibikaji wa kijamii. Kuna haja ya kuhakikisha kwamba, sera na mikakati ya kiuchumi inajikita katika kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu pamoja na mafao ya wengi. Haya ni mambo ambayo yanapaswa kumwilishwa katika maisha ya kijamii na wala si mambo yanayotoka nje. Hili ni lengo la muda mrefu linalopaswa kufanyiwa kazi kwa kuwashirikisha watu binafsi na taasisi mbali mbali katika “tumbo” la maisha ya kijamii.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, mkutano huu umeongozwa na kauli mbiu “Sera na mtindo mpya wa maisha katika kipindi cha digitali”. Moja ya changamoto kubwa katika ulimwengu wa digitali ni athari kubwa katika familia, kwani watu wengi wanajikuta hawana tena fursa za ajira. Kanisa kwa kuguswa na mahangaiko ya vijana wa kizazi kipya kutokana ukosefu wa fursa za ajira, ameamua kuitisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana ili kuonesha mshikamano wa Kanisa katika maisha na utume wa vijana wa kizazi kipya. Mchango wa Mafundisho Jamii ya Kanisa hauna budi kuwajengea vijana na familia matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Baba Mtakatifu anasema, changamoto hizi hazina budi kukabiliwa kwa kujenga umoja na mshikamano wa kiekumene, kama inavyojionesha kwa uwepo na ushiriki wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza. Hii imekuwa ni fursa ya kuweza kutambua kwa mara nyingine tena uzoefu na utajiri wa Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kuweza kufunda dhamiri nyofu za viongozi katika medani za kisiasa, kijamii na kiuchumi, mwaliko ni kuendeleza dhamana hii bila kuchoka hata kidogo, ili kujenga utamaduni wa utandawazi wa haki uchumi, usawa na ushirikishwaji wa watu. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru wote kwa mchango wao na kuwaweka chini ya huruma na neema ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.