2018-05-26 16:22:00

Kardinali mteule Becciu, kuongoza Baraza la Kipapa la Watakatifu


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali mteule Giovanni Angelo Becciu, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican, kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu; dhamana ambayo ataanza kuitekeleza mwezi Agosti 2018. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kardinali mteule Becciu ataendelea na utume wake wa sasa hadi tarehe 29 Juni 2018, Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Miamba wa imani.

Hii ni Sherehe ambayo pia Baba Mtakatifu atawasimika rasmi Makardinali 14 walioteuliwa wakati wa Sherehe ya Pentekoste kwa mwaka huu kama alama ya Kanisa la Kiulimwengu. Kardinali mteule Giovanni Angelo Becciu ataendelea pia kuwa Mwakilishi maalum wa Papa katika Shirika la Kijeshi la Malta ambalo kwa miaka ya hivi karibuni limeguswa na kutikiswa katika misingi ya uongozi wake.

Kardinali mteule Giovanni Angelo Becciu, alizaliwa tarehe 2 Juni 1948 huko Pattada, Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 27 Agosti 1972 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 5 Oktoba 2001 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu mkuu na hatimaye kuwekwa wakfu na Kardinali Angelo Sodano, aliyekuwa Katibu mkuu wa Vatican kwa wakati ule. Akateuliwa kuwa Balozi wa Angola, Sao Tome na Principe kati ya mwaka 2001 hadi mwaka 2009. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamhamishia Cuba kama kituo kipya cha kazi kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2011. Akateuliwa kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Vatican kati ya mwaka 2011 hadi mwaka 2018. Tarehe 20 Mei 2018 katika Maadhimisho ya Sherehe ya Pentekoste, kuzaliwa kwa Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko akateuwa Askofu mkuu Giovanni Angelo Becciu kuwa ni kati ya Makardinali 14 kutoka sehemu mbali mbali za dunia, watakaosimikwa rasmi hapo tarehe 29 Juni 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.