2018-05-25 16:49:00

Miaka 25 ya Mfuko wa "Centesimus Annus" na changamoto mamboleo!


Mfuko wa “Centesimus Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, CAPP, ulioanzishwa Mtakatifu Yohane Paulo II, mwaka 2018 unaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake. Hii ni kumbu kumbu endelevu tangu Papa Leo XIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Rerum Novarum” yaani “Mambo Mapya” msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Lengo la mfuko huu ni kufafanua na kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa katika uhalisia wa maisha ya watu, kwa kuwasaidia: wafanyabiashara na wataalam katika medani mbali mbali za maisha; kufahamu shughuli zinazotekelezwa na Vatican katika kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu.

 

Mfuko unapenda kukazia zaidi: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mfuko huu umeendelea kuwa nyenzo muhimu sana ya ushuhuda wa Kanisa katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Mfuko wa “Centesimus Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro kati ya tarehe 24-26 Mei 2018 kunafanyika Kongamano la Kimataifa linaongozwa na kauli mbiu “Sera na mtindo mpya wa maisha katika kipindi cha digitali”.

Wajumbe wameendelea kudadavua kuhusu mambo mapya katika masuala ya kiuchumi na jamii yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza; Ukosefu wa fursa za ajira na athari zake katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia bila kusahau mageuzi makubwa ya kitamaduni; Umuhimu wa mshikamano wa uhakika wa chakula duniani, dhidi ya utamaduni wa kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Utu na heshima ya kazi pamoja na fursa za ajira ambazo ni shirikishi; Mafundisho Jamii ya Kanisa kama chombo madhubuti cha uinjilishaji; Umuhimu wa majadiliano katika maeneo ya vita.

Bwana Domingo Sugranyes Bickel, Rais wa Mfuko wa “Centesimus Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, CAPP, katika hotuba yake ya ufunguzi, amekazia umuhimu wa Jubilei ya Miaka 25 ya Mfuko huu kama chachu ya kuhamasisha ufahamu mpana zaidi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa, kwa kuwashirikisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi memsa kwa wingi zaidi; ili yaweze kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kama njia ya kukabiliana na changamoto mamboleo.

Mabingwa na wataalamu wa masuala ya kiuchumi, wasomi, wafanyakazi katika sekta ya umma, wawakilishi wa vyama na mashirikisho ya wafanyakazi sehemu mbali mbali za dunia, watalaam na wana sayansi wanashririkishwa ili kusaidia kung’amua mapya katika uchumi na teknolojia; Ufahamu makini wa kanuni maadili na utu wema zinazopaswa kutumiwa ili kukabiliana na changamoto zote hizi. Mabingwa na wataalam hawa wamegusia mapambano dhidi ya umaskini duniani; uksoefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana na madhara yake; mwelekeo mpya wa mfumo wa kazi zinazoendeshwa kwa njia ya kidigitali na madhara yake katika jamii; kanuni maadili na sheria zinazobubujika kutoka katika Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Wajumbe wameangalia: umuhimu wa Mfuko wa Mshikamano kama njia ya kupambana na ukosefu wa fursa za ajira kwa kuwekeza zaidi katika rasilimali watu kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko. Pamoja na mambo mengine, Mfuko huu unapania kufanya maboresho makubwa ya mfumo wa kazi duniani kwa kuyahusisha makundi makuu matatu: Jumuiya zinazosukumizwa pembezoni mwa jamii; elimu pamoja na ruzuku ya elimu; mikopo nafuu pamoja na malezi kwa wafanyabiashara. Jumamosi, tarehe 26 Mei 2018, wajumbe wa mkutano huu wa kimataifa, watasikiliza changamoto kutoka kwa Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican pamoja na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol anayedadavua kuhusu “Agenda ya pamoja kwa ajili ya mafao ya wengi” na baadaye, wanakutana na Papa Francisko kwa faragha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.