Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Papa asema:Nyanyaso na dhuluma dhidi ya wafanyakazi ni dhambi ya mauti

Papa Francisko asema, dhuluma, nyanyaso na unyonyaji dhidi ya wafanyakazi ni dhambi ya mauti.

24/05/2018 14:43

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 24 Mei anaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria, Msaada wa Wakristo iliyoanzishwa na Papa Pio wa VII kunako mwaka 1815. Na mwaka 2001 Bikira Maria Msaada wa Wakristo akatangazwa kuwa ni Mama na msimamizi wa familia ya Mungu nchini China na kunako mwaka 2007, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akatangaza kwamba, hii ni siku maalum ya kuwaombea Wakatoliki nchini China. Kwa namna ya pekee, Wakatoliki wanamheshimu Bikira Maria Msaada wa Wakristo kwenye Madhabahu ya Sheshan, yaliyoko huko Shanghai, China.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linawaombea Wakatoliki wote ili waweze kuishi imani kwa ukarimu na utulivu wa ndani; kwa kujenga na kudumisha amani na upatanisho; huku wakiwa na umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, Alhamisi, tarehe 24 Mei 2018 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, amekazia umuhimu wa ufukara wa maisha ya kiroho kama kiini cha mahubiri ya Kristo na Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu. Yesu anatangaza wazi wasi kwamba, Roho wa Bwana yu juu yake amemtia mafuta ili kuwatangazia maskini Habari Njema ya Wokovu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumpenda Mungu na jirani zao, kama kielelezo cha Amri kuu ya upendo. Haiwezekani kuwatumikia mabwana wawili, yaani Mungu na fedha. Watu wakimezwa sana na utajiri na mali ya dunia, watajikuta wakibomoa mahusiano yao na jirani zao kwa sababu ya utajiri. Mfano wa tajiri na maskini Lazaro unafafanua kwa kina na mapana jinsi ambavyo utajiri unaweza kumhadaa mtu kiasi hata cha kuweza kumezwa na malimwengu. Unaweza kuharibu mafungamano na mshikamano wa kijamii na matokeo yake ni watu kutumbukia katika ubinafsi na uchoyo.

Mtume Yakobo anakazia umuhimu wa maskini kupatiwa ujira wanaostahili badala ya kutafuta faida kubwa na matokeo yake ni ukosefu wa fursa za ajira kama inavyojionesha hata nchini Italia. Baba Mtakatifu anakaza kusema, “Ole wenu msiowalipa wafanyakazi wenu pensheni; Ole wenu mnaowanyima wafanyakazi wenu muda wa mapumziko; Ole wenu ninyi mnaowadhulumu na kuwapunja wafanyakazi wenu mishahara na haki zao msingi!” Kumbukeni kwamba, hii ni dhambi ya mauti na wala haijalishi ikiwa kama kila siku unakwenda Kanisani na kwamba, umeshiriki kikamilifu katika Novena kwa Roho Mtakatifu. Utajiri na mali ya dunia, vitumike kwa ajili ya kujenga na kudumisha Injili ya upendo na mshikamano na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali na kuwaombea matajiri, ili waweze walau kutubu na kumwongokea Mungu; atakayewawezesha kuwa huru na kujinasua na utumwa wa fedha na mali. Mali na utajiri wa dunia hii viwasaidie waamini kuona njia inayowapeleka mbinguni badala ya kuwa ni kikwazo kinachowatumbukiza katika utumwa wa fedha na mali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

24/05/2018 14:43