2018-05-24 15:01:00

Masalia ya Mtakatifu Yohane XXIII yapelekwa Bergamo


Kardinali Angelo Comastri, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Alhamisi, tarehe 24 Mei 2018, ameongoza Ibada kwa ajili ya kusindikiza masalia ya Mtakatifu Yohane XXIII yanayopelekwa nyumbani kwao, alikozaliwa, yaani mjini Bergamo, Kaskazini mwa Italia. Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1959 masalia ya Mtakatifu yanatoka kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwenda mahali alikozaliwa. Haya yalikuwa ni masalia ya Mtakatifu Pio X aliyekuwa amewahakikishia waamini wake kwamba, angerejea tena Jimboni mwake, akiwa hai au amekufa. Mtakatifu Yohane XXIII alitamani hata yeye kurejea tena Jimboni mwake Venezia, lakini hakufaulu kwani alichaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, ndiyo maana, sasa wanafanya hija ya kurejesha tena masalia yake, ili kutoa nafasi kwa familia ya Mungu mahali alikozaliwa kuweza kutoa heshima zake.

Bergamo huko ndiko mahali ambapo Papa Yohane wa XXIII alikozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu; akabahatika kupata wito na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mtakatifu Yohane XXIII alikuwa anasema daima kwamba, urithi mkubwa ambao kamwe hawezi kusahau katika maisha yake ni mambo msingi aliyofundishwa nyumbani kwao; kwa njia ya mifano bora ya wazazi, ndugu, jamaa na majirani zake. Ndiyo maana daima alitamani kurejea nyumbani kwao kwa mapumziko, ili kujichotea utajiri na ushuhuda wa maisha ya  na mifano bora ya waamini.

Tangu mwanzo wa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, watu mbali mbali waliweza kushuhudia utakatifu wa maisha kama kielelezo cha uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Ni kiongozi aliyefundisha kwa mifano na maisha yake wema, uzuri na utakatifu wa maisha ya kifamilia; akapandikiza mbegu ya Injili ya matumaini kwa wale waliokata tamaa ya maisha, ili kujikita katika uzuri na wema . Aliwataka waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya amani, upendo na mshikamano wa dhati na kwamba, watoto walikuwa ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, walipaswa kulindwa, kuendelezwa na kufarijiwa katika shida na mhangaiko yao mbali mbali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.