2018-05-24 15:26:00

Askofu mkuu Alfred Xuereb "atia timu" Korea kwa imani na matumaini!


Askofu mkuu Alfred Xuereb, Balozi wa Vatican nchini Korea na Mongolia katika mahojiano maalum na Vatican News kabla ya kuondoka kuelekea kwenye utume wake mpya anasema, changamoto kubwa iliyoko mbele yake ni: Umoja na mshikamano wa kitaifa nchini Korea; haki na amani; huduma ya Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa watu wa Mungu katika maeneo ya uwakilishi wake! Askofu mkuu Xuereb, tarehe 26 Mei 2018 “anatia timu” huko Seoul, Korea ya Kusini, tayari kuanza kutekeleza dhamana na utume wake kwa kutambua na kuthamini mchango mkubwa unaoendelea kutolewa na Makanisa mahalia katika mchakato mzima wa upatanisho, haki na amani.

Askofu mkuu Alfred Xuereb anasema, tarehe 26 Mei ina umuhimu wa pekee katika maisha na utume wake kama Padre, kwani hii ndiyo siku aliyopewa Daraja Takatifu ya Upadre, miaka 34 iliyopita na huo ukawa ni mwanzo wa safari yake ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Anaenda nchini Korea ya Kusini, kama sehemu ya utekelezaji wa wito na maisha yake ya Kikasisi, daima akitumainia neema na baraka ya Mwenyezi Mungu ambayo imemwongoza wakati wote wa maisha na utume wake. Ni matumaini yake kwamba, Mwenyezi Mungu ataweza kumtumia kama chombo chake cha amani, upatanisho na huduma makini kwa watu wa Mungu Korea na Mongolia.

Askofu mkuu Xuereb anasema, anaanza utume wake katika kipindi muhimu sana cha historia ya maisha ya familia ya Mungu nchini Korea, inayoonesha ile hamu ya kutaka kuungana pamoja kama taifa moja, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa, nyenzo muhimu sana ya ujenzi wa amani, ustawi na maendeleo ya wengi! Mchakato wa umoja na upatanisho wa kitaifa nchini Korea ulianza rasmi tarehe 27 Aprili 2018 kwa kuwakutanisha Marais wa Korea ya Kusini na Kaskazini!

Baba Mtakatifu Francisko akatumia fursa hii kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuunga mkono juhudi hizi ili ziweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani amani na utulivu; upendo na mshikamano wa kidugu. Kwa muda wa miaka 23 familia ya Mungu Korea ya Kusini, kila siku ya Jumanne, ilikuwa inakutana kusali na kumwomba Bikira Maria, Mama wa neema aweze kusaidia kuombea mchakato wa umoja na mshikamano wa kitaifa anasema Askofu mkuu Xuereb.

Hivi karibuni, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican alisikika akisema, matukio ya hivi karibuni huko Korea yamewasha kwa mara nyingine tena, moto wa matumaini ya umoja na mshikamano wa kitaifa. Kanisa linayo nafasi ya pekee sana katika mchakato mzima wa upatanisho, umoja na mshikamano wa familia ya Mungu nchini Korea. Kanisa litaendelea kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili bila kusahau mchango wake katika diplomasia ya kimataifa, ili kuweza kuzima kiu ya amani, ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu nchini Korea. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Xuereb amebahatika kufanya kazi na Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI pamoja na Papa Francisko!

Kumbe, ni kiongozi ambaye ana uzoefu mkubwa katika masuala ya diplomasia ya kimataifa. Anasema, kati ya mambo makubwa ambayo amejifunza kutoka kwa Mababa hawa wa Kanisa ni sadaka na majitoleo kwa Kristo na Kanisa lake; kwa kujikita katika unyenyekevu na ukarimu! Hakuna utukufu pasi na Fumbo la Msalaba; wala hakuna unyenyekevu pasi na kunyenyekeshwa. Anakwenda kuuanza utume wake Korea na Mongolia, akiwa na matumaini ya kupata msaada wa sala kutoka kwa watu mbali mbali ambao amebahatika kufahamiana nao na kumtajirisha katika maisha na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokuwa anamweka wakfu kuwa Askofu mkuu alisema, wajibu wa kwanza wa Askofu ni kusali, ili aweze kutekeleza vyema dhamana ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, daima akionesha umoja wa urika na Maaskofu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro! Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Alfred Xuereb alizaliwa kunako mwaka 1958 huko Malta; akapata Daraja Takatifu ya Upadre mwaka 1984 na kujiunga na huduma ya kidiplomasia mjini Vatican kunako mwaka 1991 na mapema mwaka huu Baba Mtakatifu Francisko amemteua kuwa Askofu mkuu na Balozi mpya wa Vatican Korea na Mongolia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.