2018-05-24 14:23:00

Amana, utajiri na urithi wa Mtakatifu Yohane XXIII katika Kanisa!


Mtakatifu Yohane XXIII anakumbukwa na watu wengi duniani kutokana na ucheshi wake; mchango wake katika kukuza na kudumisha utamaduni wa amani duniani unaofumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Ni kiongozi aliyependa kuona tasnia ya mawasiliano ya jamii inajikita katika: ukweli, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Alipenda kuhakikisha kwamba, vijana wa kizazi kipya wanawezeshwa kimaadili, kiutu na kiuchumi ili kuweza kupambana na hali pamoja na mazingira yao.

Mtakatifu Yohane XXIII alikazia kwamba, Kanisa kwa asili ni la kimisionari, linatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na kwamba, ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa, mambo yanayopaswa kuendelezwa na kudumishwa kwa vijana wa kizazi kipya! Haya ni kati ya mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum na Jarida la “Eco” linalochapishwa huko mjini Bergamo, mahali alipozaliwa Mtakatifu Yohane XXIII.

Masalia ya Mtakatifu Yohane XXIII yanafanya hija huko Bergamo kama chachu ya upyaishaji wa maisha ya kiroho miongoni mwa waamini ndani na nje ya Italia, kwani huyu ni kiongozi aliyefahamika sana kati ya watu wa Mataifa kutokana na mchango wake katika medani mbali mbali za maisha ya watu. Hii ni nafasi kwa wagonjwa, maskini na waamini wenye mapenzi mema ambao kutokana na sababu mbali mbali hawakupata fursa ya kutembelea kaburi la Mtakatifu Yohane XXIII mjini Roma. Ni mwaliko wa kumwangalia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, chemchemi ya furaha ya Injili kwa waja wake.

Mtakatifu Yohane XXIII, alipenda kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukimbilia huruma, upendo na hifadhi katika Madonda Matakatifu ya Yesu; kwa njia ya huduma makini kwa maskini, wagonjwa na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, maskini ni amana na utajiri wa maisha na utume wa Kanisa. Ni kiongozi aliyeshuhudia mateso na mahangaiko ya watu wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Daima Msalaba wa Kristo ulikuwa ni kielelezo cha mateso na mahangaiko ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa.

Mtakatifu Yohane XXIII katika maisha na utume wake, alipenda kuona wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii wanajikita katika tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii; kwa kutafuta, kulinda na kudumisha ukweli, utu na heshima ya binadamu. Aliwataka wadau katika tasnia ya habari kuwajibika barabara katika kazi na dhamana yao katika jamii, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa haki, amani na maridhiano kati ya watu. Vyombo vya habari kamwe visiwe ni chanzo cha kuchochea uchu wa mali na madaraka kwani matokeo yake ni vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ukweli wa habari upewe kipaumbele cha kwanza, kwani ukweli daima utawaweka huru na kwamba, waandishi wa habari wajiepushe na habari za kughushi na badala yake wajikite katika uandishi wa habari unaojikita katika Injili ya amani, umoja, upendo na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, anapenda kuivalia njuga changamoto hii, kama shuhuda na chombo cha Habari Njema ya Wokovu.

Mtakatifu Yohane XXIII ni kiongozi aliyemwilisha katika maisha na utume wa Kanisa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Akajikita katika kutafuta, kusimamia na kudumisha amani inayojikita katika: ukweli, haki, upendo na uhuru kama; mambo msingi yanayofumbatwa katika Waraka wake wa kitume, “Pacem in Terris wa Mwaka 1964. Lengo ni kuiwezesha familia ya binadamu kujenga jamii inayosimikwa katika umoja, upendo, udugu, haki na mshikamano wa dhati. Alipenda kuona vijana wa kizazi kipya wanajengewa uwezo kiuchumi ili kupambana na hali pamoja na mazingira yao. Kila kijana anasema Baba Mtakatifu Francisko ana historia, karama na changamoto zake katika maisha. Mama Kanisa anapenda kuwekeza miongoni mwa vijana ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili. Papa Yohane XXIII alikuwa na upendo mkubwa kwa vijana wa kizazi kipya.

Kanisa kwa asili ni la kimisionari kwani limezaliwa na linatumwa ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, dhamana iliyotekelezwa kwa kiasi kikubwa na Mtakatifu Yohane XXIII kwa kutuma wamisionari sehemu mbali mbali za dunia ili kutangaza Injili ya Kristo. Kutoyafahamu Maandiko Matakatifu wanasema Mababa wa Kanisa ni kutomfahamu Kristo. Kanisa linaendelea kuinjilisha kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko na wala hakuna sababu ya msingi ya kufanya wongofu wa shuruti, dhana ambayo imepitwa na wakati.

Urithi wa utajiri wa familia yake unaendelea kutumiwa na Kanisa kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji huko Bergamo, ni jambo la kumshukuru Mungu. Hili ni eneo ambalo kazi ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa watu wake! Kumbe, rasilimali na utajiri wa nchi unapaswa kutumiwa vyema kama kielelezo cha upendo na mshikamano na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Jamii inahitaji uchumi shirikishi na shikamanishi, ili kupambana na ukosefu wa fursa za ajira na umaskini wa hali na kipato, ili hatimaye kudumisha utamaduni wa mshikamano kati ya watu! Kuna haja ya kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene, kwa kukataa kishawishi cha kutumbukia kwenye misimamo mikali ya kidini na kiimani ambayo imekuwa ni chanzo kikuu cha vitendo vya kigaidi vinavyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Huu ndio urithi wa Mtakatifu Yohane XXIII katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News








All the contents on this site are copyrighted ©.