2018-05-23 15:44:00

Papa Francisko: Siku ya Familia Duniani, 2018: Rehema kamili kutolewa


Rehema hupatikana kwa njia ya Kanisa, ambalo, kwa nguvu ya uweza wa kufunga na kufungua, lililopewa na Kristo Yesu, huingia kati kwa manufaa ya Mkristo na hufungua hazina ya mastahili ya Kristo na watakatifu ili kupata kwa Baba wa huruma msamaha wa adhabu za muda zinazotokana na dhambi zao. Hivi Mama Kanisa hataki tu kutoa msaada kwa watoto wake hawa, bali pia kuwachochea kwa kazi za uchaji, toba na mapendo. Katekisimu ya Kanisa Katoliki (n.1471), mintarafu rehema kamili inatuelewesha kwamba: Rehema ni msamaha mbele ya Mungu ambao kosa lake lilikwishwafutwa, msamaha ambao Mkristo mwamini aliyejiweka vizuri huupata  kutoka katika hazina ya malipizi ya Kristo na ya Watakatifu. Rehema inaweza kuwa ya muda au Kamili. Rehema ya muda huondoa sehemu ya adhabu ya adhabu za dhambi na rehema kamili huondoa adhabu zote (Rej. KKK, n.1472).

Mkristo huweza kupata rehema kamili kwa ajili yake yeye mwenyewe au kwa ajili ya marehemu kama atatimiza yafuatayo. Mosi, awe na nia thabiti ya kupata rehema katika kipindi kilichopangwa, pili akokee sakramenti ya Upatanisho (Kitubio), tatu, Apokee Ekaristi Takatifu siku hiyo ya kutolewa rehema kamili, nne; asali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu na tano atembelee Kanisa au Kituo maalumu kilichotengwa kwa ajili ya kupatiwa rehema Kamili.

 Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Dublin, nchini Ireland, kuanzia tarehe 22- 26 Agosti 2018 ametoa rehema kamili kwa waamini watakaoshiriki kikamilifu katika maandalizi na maadhimisho ya Siku ya Familia Duniani inayoongozwa na kauli mbiu “Injili ya familia: furaha ya ulimwengu”. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutubu na kumwongokea Mungu; kwa kushuhudia imani yao inayomwilishwa katika upendo, daima wakijitahidi kuzitakatifuza familia zao, kwa kufuata mfano bora wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya IX ya Familia Duniani yanaongozwa kwa namna ya pekee kabisa na Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi.

Taarifa kutoka Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha zinaonesha kwamba, hadi kufikia wakati huu kuna zaidi ya washiriki 22, 000 kutoka katika mataifa 103 ambao tayari wamekwisha kujiandisha. Rehema kamili inatolewa hata kwa wale ambao hawatapata fursa ya kushiriki mubashara katika maadhimisho haya, lakini wakitimiza masharti yaliyowekwa wanaweza pia kujipatia rehema ya muda. Hii ni pamoja na kusali Baba Yetu, Kanuni ya Imani; kwa kufanya toba na matendo ya huruma.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, familia bado inaendelea kuwa ni kitovu cha Habari Njema ya Wokovu kwa walimwengu, kumbe, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanahamasishwa na Mama Kanisa, kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo ambao umegeuka kuwa kama tambara bovu! Ni wajibu wa wanandoa kutangaza na kushuhudia uzuri, utakatifu na heshima ya maisha ya ndoa na familia kama njia muafaka ya kuyatakatifuza malimwengu! Familia kadiri ya mpango wa Mungu kama ilivyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu na familia jinsi ilivyo katika ulimwengu mamboleo ni changamoto pevu katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu Injili ya familia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.