2018-05-23 06:58:00

Papa Francisko asema: Vijana hakuna kulala hadi kieleweke!


Baba Mtakatifu Francisko anasema, shule ni mahali pa kuwafunda vijana wa kizazi kipya maana na umuhimu wa tunu ya maisha; kwa kujiweka wazi kwa wale wasiowafahamu, ili kuchanganyika na hatimaye, kufutilia mbali kabisa maamuzi mbele ambayo ni chanzo cha kinzani, mipasuko ya kijamii na hatimaye vita! Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurentes" ilianzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2013 baada ya uzoefu na mang'amuzi yake huko nchini Argentina, kwa sasa taasisi hii, inapania kuendelea kuwapa vijana uzoefu na mang’amuzi ya kutambua na kushuhudia Injili ya maisha sanjari na kukuza elimu na malezi bora kwa vijana wa kizazi kipya.

Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurentes" imeasisiwa katika mazingira ya umaskini, kwa ajili ya watoto waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi ili kuwajengea matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi, daima mwanadamu na mahitaji yake msingi akipewa kipaumbele cha kwanza. Juhudi hizi zinafanywa kwa njia ya elimu, sanaa, michezo, pamoja na kujenga utamaduni wa kuwakutanisha vijana ili hatimaye, kuchangia katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika udugu, haki, amani na mapendo ya dhati.

Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko amezindua tawi la Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurentes" katika kitongoji maskini huko Barrio, kati kati ya mji wa Buenos Aires, nchini Argentina. Baba Mtakatifu akiwa ameungana na magwiji na vinara wa michezo kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ameweza kutoa ujumbe wake wa matumaini kwa vijana hawa na kusikiliza muziki ulioporomoshwa kwa niaba yake, kama alama ya shukrani kwa jitihada zake za kuwajengea vijana uwezo wa kupambana na mazingira yao kwa njia ya elimu na malezi makini.

Tukio hili la aina yake limehudhuriwa pia na Josè Maria Del Corral, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurentes" pamoja na Katibu wake mkuu Enrique Palmeyro. Ujumbe wa Baba Mtakatifu uliweza kuwafikia pia vijana wengine waliokuwa wamejiunga na Baba Mtakatifu kwa njia ya video kutoka: Argentina, Paraguay, Colombia, Mexico, Perù, Brazil, Haiti, Msumbiji, Italia na Hispania. Katika uzinduzi huu, Baba Mtakatifu Francisko amewaambia vijana “hakuna kulala hadi kieleweke; wala hakuna sababu ya msingi ya kukata wala kukatishwa tamaa, bali waendelee kuwa na ndoto inayoweza kumwilishwa katika uhalisia wa maisha.”

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa na ujasiri kiasi hata cha kuthubutu kupambana na hali pamoja na mazingira yao, kwa kuondokana na mazoea ya kuzama katika mawazo ya kufikirika tu, kiasi hata cha kujikuta wakiwa wanakula “pensheni katika umri wa miaka kumi na mitano”. Hali hii anasema Baba Mtakatifu, inasikitisha na kukatisha tamaa, kuwaona vijana wanazeeka katika umri mdogo kabisa. Hii inatokana na kasumba ya kijana kujikatia tamaa na kuacha kuchakarika ili kujitafutia riziki halali kwa njia ya kazi halali; kwa maneno machache anasema Baba Mtakatifu, vijana wa aina hii wanakosa ari na mwamko wa kuthubutu katika maisha kwa kusahau kwamba, maisha ni mapambano.

Vijana kutoka sehemu mbali mbali wameonesha furaha na mwamko wa maisha mapya yanayobubujika kutoka katika elimu bora! Wote hawa wameweza kupata neno la faraja na baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Amewatia shime, wale wote wanaojisadaka usiku na mchana kwa ajili ya utume kwa vijana, kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, daima wakiwa na imani na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Baba Mtakatifu amewataka wasichana kuendelea kuboresha maisha yao kwa njia ya elimu, ili hatimaye, kuweza kuwajibika barabara katika ujenzi wa tunu msingi za kifamilia na kijamii, Vijana wawe na jeuri ya kutoka katika ubinafsi wao, tayari kuwashirikisha wengine karama na mapaji waliyokirimiwa na Roho Mtakatifu katika maisha yao, kwani yote haya ni kwa ajili ya ujenzi wa jamii inayowajibika barabara. Kukaa na kujifungia katika ubinafsi wao ni ugonjwa utakaowaathiri sana katika maisha. Vi vyema zaidi, ikiwa kama vijana watathubutu kuanza na kuanguka, tayari kusimama na kuendelea na safari, kuliko vijana wanaokaa vijiweni kwa ajili ya kusogoa usiku na mchana!

Vijana kutoka Mexico, wamewataka wanafunzi wenzao kuhakikisha kwamba, wanajikita katika elimu bora inayofumbatwa katika malezi na tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, kama njia ya kupambana na umaskini wa hali na kipato kwa kutambua kwamba, umaskini mkubwa ni ule wa kumong’onyoka kwa maadili na utu wema. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru wale wote wanaoendelea kujisadaka katika elimu, malezi na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya ili kuwajengea leo na kesho iliyo bora zaidi. Amewashukuru wasanii na wana michezo mbali mbali ambao wamechangia karama, mapaji na kazi zao kama sehemu ya kuendeleza huduma inayotolewa na Taasisi ya Kipapa ya "Scholas Occurentes" kila mwaka, sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.