2018-05-23 10:47:00

Maaskofu Katoliki Italia: Kanisa lina mchango mkubwa katika maisha!


Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake elekezi kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, Jumatatu, 21 Mei 2017 alionesha hofu na mashaka yake kwa maisha na utume wa Kanisa nchini Italia: kutokana na kupungua kwa idadi ya miito mitakatifu; ukosefu wa ushuhuda wa ufukara wa Kiinjili wenye mvuto na mashiko katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na uwepo wa idadi kubwa ya majimbo nchini Italia yanayopaswa kuunganishwa ili kuongeza tija na ufanisi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji.

Kardinali Gualtierro Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, kwa upande wake, amewapongeza Makardinali na Maaskofu wapya walioteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake. Amewakumbuka na kuwaombea Makardinali na Maaskofu waliolala katika usingizi wa amani, wakiwa na tumaini la ufufuko na maisha ya uzima wa milele. Anasema, kwa sasa kipaumbele chake cha kwanza ni huduma kwa familia ya Mungu nchini Italia, kwa kujikita zaidi katika mchakato wa maboresho ya mawasiliano kama sehemu ya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linapaswa kujiandaa kikamilifu ili kushiriki katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2018 hapa mjini Vatican. Jambo la msingi ni viongozi wa Kanisa kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo; kwa kuwashirikisha vijana wa kikazi kipya katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na kuwasaidia kukua na kukomaa: kimwili, kiroho na kiutu, tayari kufanya maamuzi magumu katika hija ya maisha yao, ikiwa ni pamoja na kujisadaka katika maisha na utume wa Kanisa kama wakleri na watawa.

Kardinali Bassetti amegusia hali ngumu ya uchumi inavyoathiri maisha ya wananchi wengi nchini Italia, kiasi hata cha kutikisha kanuni maadili na utu wema; hali ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa mipasuko ya kijamii na mapambano kati ya watu. Hali ya kisiasa kwa sasa inakwenda mrama kutokana na wanasiasa kuchanganyikiwa na uchu wa madaraka na hivyo kusahau ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Italia. Misingi ya demokrasia nchini Italia imetikiswa sana, kiasi kwamba, Kanisa lina changamoto ya kuhakikisha kwamba, tunu msingi za Kiinjili zinapenyezwa katika mchakato wa kukuza na kuimarisha demokrasia kwa ajili ya ushiriki wa wananchi wengi zaidi.

Mafundisho Jamii ya Kanisa ni amana na utajiri ambao unapaswa kumwilishwa hata katika medani za kisiasa kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu. Imani imwilishwe katika huduma kwa familia ya Mungu nchini Italia, ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, umoja, udugu na mshikamano; daima kanuni maadili na utu wema vikipewa kipaumbele cha kwanza katika maisha ya hadhara. Hizi ni kanuni ambazo zinapania pamoja na mambo mengine kuboresha hali ya maisha kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini, kwa wale waliokata tamaa; watu wanaoelemewa na woga pamoja na jeuri katika maisha. Umefika wakati wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili itakayosaidia kuunda watu wema, wakweli na waaminifu; tayari kujisadaka kwa ajili ya kukuza na kudumisha mchakato wa haki, amani na maridhiano katika maisha ya mwanadamu.

Eneo la Mashariki ya Kati na Bahari ya Mediterrania yamegeuka kuwa ni uwanja vya vita vinavyotokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani; vitendo vya kigaidi, chuki na uhasama; mambo ambayo yanapaswa kurekebishwa kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi; upatanisho, haki na amani! Kuna haja ya kujenga “Tasaufi ya Amani Ukanda wa Mediterrania", ili kuliwezesha Kanisa kushiriki kikamilifu katika mahangaiko na matumaini ya watu waliokata tamaa ya maisha.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, linamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuamua kwamba, tarehe 7 Julai 2018 atatembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Nicholaus wa Bari, ili kusali na kutafakari juu ya mateso na mahangaiko ya Wakristo huko Mashariki ya Kati. Hawa ni waamini wanaolazimika kuyakimbia makazi na nchi yao kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Baba Mtakatifu ameonesha pia nia ya kuwaalika pia viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo kuungana pamoja naye katika tukio hili muhimu! Anawaomba Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, kushiriki katika maandalizi haya kwa njia ya sala na sadaka zao! Kardinali Gualtierro Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, anahitimisha hotuba yake ya ufunguzi kwa kuonesha matumaini kwamba, Baba Mtakatifu Francisko katika tukio hili ataweza kuwaonesha dira na mwongozo sahihi wa kufuatwa katika maisha na utume wa Kanisa.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.