2018-05-22 07:04:00

Changamoto mamboleo: Ukosefu wa ajira, Familia na Wakimbizi!


Mfuko wa “Centesimus Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, "CAPP", ulianzishwa rasmi tarehe 5 Juni 1993 na Mtakatifu Yohane Paulo II, kama kumbu kumbu endelevu tangu Papa Leo XIII alipochapisha Waraka wake wa Kitume “Rerum Novarum” yaani “Mambo Mapya” msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Lengo la mfuko huu ni kufafanua na kumwilisha Mafundisho Jamii ya Kanisa katika uhalisia wa maisha ya watu, kwa kuwasaidia: wafanyabiashara na wataalam katika medani mbali mbali kufahamu shughuli zinazotekelezwa na Vatican katika kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu; kwa kukazia: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mfuko huu umeendelea kuwa nyenzo muhimu sana ya ushuhuda wa Kanisa katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu.

Kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Mfuko wa “Centesimus Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro kati ya tarehe 24-26 Mei 2018 kutafanyika Kongamano la Kimataifa linaongozwa na kauli mbiu “Sera na mtindo mpya wa maisha katika kipindi cha digitali”. Askofu mkuu Diarmuid Martin wa Jimbo kuu la Dublin ambaye aliwahi kuwa Katibu mkuu msaidizi na hatimaye, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani kwa wakati ule, anasema, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanaendelea kukua na kukomaa kila kukicha kutokana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kuibuliwa na binadamu hususan katika maendeleo ya sayansi na teknoloji.

Kumbe, Mfuko wa “Centesimus Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro ni chombo cha majadiliano ya kina kati ya Mafundisho Jamii ya Kanisa na Sayansi Jamii; kati ya kanuni maadili na utu wema na watunga sera na sheria ili kusaidia mchakato wa kupyaisha utawala bora na masuala ya fedha kimataifa, ili kweli sera na mikakati ya uchumi na maendeleo isaidie mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Mama Kanisa anahimiza sera za uchumi shirikishi, mtu na mahitaji yake msingi akiwa ni kiini cha mjadala mzima! Kanuni maadili zinapaswa kuzingatiwa katika masuala ya fedha na uchumi ili kuleta usawa kati ya watu, vinginevyo ni uwepo wa kashfa ya pengo kubwa kati ya matajiri wanaokula na kusaza na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” wanaoshindia kibaba cha uji! Raslimali na mali ya dunia, zinapaswa kuwa ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Kwa hakika, sera na mifumo mipya ya uchumi inaweza kusaidia kupunguza pengo kati ya matajiri na maskini. Wachumi bora na makini, wanaweza pia kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya rushwa na ufisadi, kwani waathirika wakuu ni maskini.

Majadiliano katika ukweli na uwazi kati ya Mafundisho Jamii ya Kanisa na Sayansi jamii yanahitaji uwekezaji makini katika rasilimali watu, watakaoweza kutumia vyema kipaji chao cha ubinifu kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi katika medani mbali mbali za maisha. Kipaji cha ugunduzi ni uti wa mgongo wa ujenzi wa uchumi unaofumbatwa kwa jamii yenye ujuzi, maarifa na uelewa mpana. Uchumi shirikishi, hauna budi kuhakikisha kwamba, hata maskini wanapata fursa ya kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao yao.

Askofu mkuu Diarmuid Martin anakaza kusema, katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, Mfuko wa “Centesimus Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, umejielekeza zaidi katika: kutafakari, kutafuta na kukusanya maoni na ushauri ili kukabiliana na changamoto mamboleo katika masuala ya uchumi kwa kujikita katika mafao ya wengi. Huu ndio mchakato wa Dublin, uliopitishwa na kuanza kufanyiwa kazi tangu mwaka 2014 kwa kukazia umuhimu wa kuzingatia kanuni maadili katika mifumo ya maendeleo inayogusa medani mbali mbali za maisha ya binadamu. Pamoja na mambo yote haya, lakini pia watunga sera za uchumi na maendeleo hawana budi kuzingatia tunu msingi za maisha ya kiroho, uhuru wa binadamu na kwamba, binadamu na mahitaji yake msingi anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.

Mafundisho Jamii ya Kanisa hayana budi “kujichimbia zaidi” katika kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoendelea kuibuliwa na sera tenge kuhusu uchumi na maendeleo ya binadamu. Ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ni kati ya changamoto kubwa kwa wakati huu sehemu mbali mbali za dunia. Sambamba na hili ni “mshahara kiduchu” ambao hauwezi kukidhi mahitaji msingi ya mtu pamoja na familia yake. Hii inatokana na ukweli kwamba, watu kila kukicha wanaondoka kwenda kazini, lakini hali yao ya maisha inabaki kuwa vile vile bila mabadiliko na hata wengine wanadiriki kusema, “ni afadhali ya jana”. Kimsingi mshahara haukidhi gharama ya maisha na matokeo yake, hali ya maisha ya wafanyakazi wengi inaendelea kudidimia kila kukicha!

Changamoto ya pili ni familia ambayo inapaswa kuwa pia ni kiini cha sera na mikakati ya maendeleo endelevu, kwa kukazia ekolojia ya binadamu. Kanisa halina budi kuendelea kuwekeza katika Injili ya familia kwa kuonesha: uzuri, utakatifu, umuhimu na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko anasema, familia bado inaendelea kuwa ni kitovu cha Habari Njema ya Wokovu kwa walimwengu, kumbe, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa na Mama Kanisa, kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo ambao umegeuka kuwa kama tambara bovu! Ni wajibu wao kutangaza na kushuhudia uzuri, utakatifu na heshima ya maisha ya ndoa na familia kama njia muafaka ya kuyatakatifuza malimwengu! Familia kadiri ya mpango wa Mungu kama ilivyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu na familia jinsi ilivyo katika ulimwengu mamboleo ni changamoto pevu katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu Injili ya familia!

Changamoto ya tatu ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ambalo limegusa na kutikisa sera, mipango, uchumi na maendeleo ya Jumuiya ya Kimataifa. Hapa, pia familia za wakimbizi na wahamiaji zinapaswa kupewa kipaumbele cha pekee kama chachu ya maendeleo na wala si kama kizingiti na kikwazo katika usalama wa taifa, maendeleo na ustawi wa jamii husika. Kumbe, Mafundisho Jamii ya Kanisa na Sayansi Jamii ni sawa na chanda na pete, yanategemeana na kukamilishana kwa ajili ya kulinda na kudumisha utu,  heshima, ustawi na maendeleo ya binadamu!

Kwa upande wake, Dr. Domingo Sugranyes Bickel, Rais wa Mfuko wa “Centesimus Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro, amesema kwamba, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli atashiriki na kutoa mchango wake kuhusu “Mafao ya wengi kama agenda ya pamoja kwa Wakristo wote”. Anna Maria Tarantola amewasilisha machapisho kadhaa ambayo yametolewa hivi karibuni na Mfuko huu kama sehemu muhimu sana ya tafakari ya Mafundisho Jamii ya Kanisa katika ulimwengu mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.