2018-05-21 08:37:00

Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa


Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa anasema, Kanisa tarehe 11 Februari 2018, Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes, limeadhimisha Jubilei ya miaka 160 tangu Bikira Maria alipotekea Lourdes, Ufaransa. Kutokana na kumbu kumbu hii, Baraza la Kipapa la Ibada na Sakramenti za Kanisa limeamua kutekeleza uamuzi wa Baba Mtakatifu Francisko wa kuadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa, Jumatatu, baada ya Sherehe ya Pentekoste, kila mwaka kuanzia sasa.

Tamko hili linayataka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, kuhakikisha kwamba, yanaingiza marekebisho haya katika Kalenda ya Liturujia ya Kanisa; yanatafsiri maelekezo ya maadhimisho ya Misa Takatifu, Sala ya Kanisa na Kitabu cha Orodha ya Wafiadini wa Kanisa Katoliki. Tafsiri zote hizi zinapaswa kutumwa kwenye Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa kwa ajili ya kuidhinishwa, tayari kuanza kutumika katika maeneo yao ya uongozi.

Kardinali Sarah anasema, uamuzi huu wa Baba Mtakatifu Francisko ni kilele cha ukomavu wa Kiliturujia na Ibada kwa Bikira Maria, kama walivyofafanua Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Tamko la “Lumen gentium” yaani Mwanga wa Mataifa, linalodadavua kuhusu Fumbo la Kanisa na kwamba, Kanisa ni Fumbo la Mwili wa Kristo na wale wote wanaozaliwa ndani mwake kwa njia ya Sakramenti za Kanisa wanafanyika kuwa ni ndugu wa Kristo na washiriki wa Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu. Kwa njia ya Ekaristi takatifu, wanainuliwa ili kufikia utimilifu wa ushirikiano na upendo pamoja naye na kati yao, daima wakiendelea kujipyaisha.

Mwenyeheri Paulo VI, kunako tarehe 21 Novemba 1964 alitamka wazi kwamba, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walitambua dhima ya Bikira Maria katika Fumbo la Umwilisho na katika mpango mzima wa kazi ya ukombozi. Walichambua nafasi ya Bikira Maria katika Agano la kale; Bikira Maria katika Agano Jipya kwa utayari wake wa kushiriki katika mpango wa Mungu na kwa njia ya imani na utii akashiriki katika kazi ya ukombozi na ndiyo maana Mababa wa Kanisa wanamwita Bikira Maria kuwa ni “Mama wa walio hai”.

Bikira Maria alishiriki kikamilifu katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yake kama Mama wa Mkombozi. Alishiriki kikamilifu katika maisha ya hadhara hadi siku ile alipomwona Mwanaye wa pekee, akiinama kichwa na kukata roho pale Msalabani. Akakubali kupokea upendo wa Sadaka ya mateso na kifo chake Msalabani, alipokabidhiwa kwa Yohane, Mwanafunzi aliyempenda kwa kusema, “Mama, tazama mwanao”. Bikira Maria aliyekingiwa na kila doa la dhambi ya asili, aliendelea kusali pamoja na Mitume wa Yesu, huku wakisubiri Roho Mtakatifu aweze kuwashukia.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wakakiri kwamba, Kristo Yesu ni mpatanishi wa pekee na Bikira Maria, aliyeshiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi na kwamba, ni mwombezi kwa ajili ya wokovu wa watu. Bikira Maria na Mama ni mfano wa utimilifu wa Kanisa linalopaswa kuuiga utakatifu wa Mama wa Mungu, upendo wa kimama unaowawezesha watu kuzaliwa upya. Bikira Maria ni ishara na tumaini thabiti na faraja kwa taifa la Mungu linalosafiri hapa duniani. Bikira Maria, Mama wa Kanisa auombee umoja wa Wakristo!

Kardinali Robert Sarah anaendelea kufafanua kwamba, kwa njia ya Fumbo la Pasaka, Kristo Yesu ameangamiza mauti na kufufuka kwake akawarudishia waja wake maisha ya uzima wa milele. Kutoka ubavuni mwake alikochomwa kwa mkuki, kumetoka huko Sakramenti ya ajabu ya Kanisa zima! Huu ndio mwendelezo wa Sakramenti ya Ubatizo na Ekaristi Takatifu, inayowasukuma waamini kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Upatanisho ulioadhimishwa kunako mwaka 1975, Ibada ya Misa Takatifu kwa heshima ya Bikira Maria Mama wa Kanisa ikaadhimishwa. Mtakatifu Yohane Paulo II katika kipindi cha uongozi wake, akaridhia maneno “Bikira Maria, Mama wa Kanisa” yaongezwe kwenye Litania ya Bikira Maria wa Loreto kunako mwaka 1980.

Kardinali Robert Sarah  anasema katika maadhimisho ya Mwaka wa Bikira Maria, Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Kanisa ikaongezwa na baadaye, Mabaraza ya Maaskofu yakaomba idhini ya kuadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa, Jumatatu, baada ya Siku kuu ya Pentekoste, kuendeleza Mapokeo yaliyokuwa yametangazwa na Mwenyeheri Paulo VI. Ndiyo maana, Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua na kuthamini dhima na mchango wa Umama wa Bikira Maria; kwa ulinzi na tunza yake ya kimama kwa Kanisa linalosafari hapa duniani, ameamua kwamba, tangu sasa Siku kuu ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa, itakuwa inaadhimishwa kwa Kanisa zima, Jumatatu, baada ya Sherehe ya Pentekoste.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, waamini wataendelea kukumbuka kwamba, ikiwa kweli wanataka kuwa wafuasi waaminifu wa Kristo Yesu na Kanisa lake; ili kuguswa na kuponywa na huruma na upendo wa Mungu, wanapaswa kuzingatia mambo makuu matatu katika maisha yao ya kiroho: Msalaba, Ekaristi takatifu na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Haya ni Mafumbo makuu matatu ambayo Mwenyezi Mungu amependa kuwazawadia waja wake ili kupyaisha maisha yao, yaweze kuzaaa matunda ya wongofu na utakatifu wa maisha yanayomwelekea Kristo Yesu katika hali ya ukimya, kielelezo cha nguvu ya ukimya katika maisha ya mwamini anasema, Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News! 








All the contents on this site are copyrighted ©.