2018-05-21 14:58:00

Papa Francisko: Kanisa ni Mama na Mchumba mwaminifu wa Kristo!


Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa, kwa mara ya kwanza imeadhimishwa Jumatatu, tarehe 21 Mei 2018. Ibada hii kwa Bikira Maria, itawasaidia waamini kukumbuka kwamba, maisha ya Kikristo yanafumbatwa katika Fumbo la Msalaba linaloadhimishwa katika Ekaristi Takatifu, Kanisa linapomtolea pia sifa na heshima Bikira Maria, Mama wa Mkombozi, aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican amekaza kusema, sifa ya kwanza ya Mama ni upendo, Kanisa ni Mama na Mwalimu linaloonesha na kushuhudia upendo unaoliwezesha kupata watoto wapya wanaozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu. Lengo la maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa ni kuwawezesha waamini kutambua na kuthamini maana ya Umama wa Kanisa katika maisha na utume wa viongozi wa Kanisa, watawa na waamini katika ujumla wao, ili kwa pamoja waweze kukuza na kudumisha Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Injili inamwonesha Bikira Maria kama Mama wa Yesu na kwamba, umama wake umeyapamba Maandiko Matakatifu, tangu alipopashwa habari na Malaika Gabrieli kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu, hadi pale alipodiriki kusimama chini ya Msalaba na kupokea maiti ya Mwanaye mpendwa, Kristo Yesu. Mababa wa Kanisa wametafakari kwa kina na mapana Umama wa Bikira Maria katika maisha na utume wa Kanisa. Bila Umama, Kanisa linapoteza utambulisho wake wa kweli na hivyo kujikuta likiwa kama “Timu ya mpira wa miguu”. 

Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Kanisa linatekeleza dhamana na wajibu wake wa Umama dhidi ya mfumo dume unaoweza kulipeleka Kanisa mlama. Kanisa lina asili ya umama unaofumbatwa katika maisha na utume wa Bikira Maria, Mama wa Kanisa! Hivi ndivyo Kristo Yesu alivyopenda Kanisa lake liweze kuonekana na kutambulikana na wengi. Kanisa ni Mama kwani linafumbatwa katika upendo, huruma na hata wakati mwingine katika ukimya wake. Hii ndiyo changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga hata na waamini, kwa kutambua kwamba, wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa: upendo mkalimifu, huruma na tabasamu la kukata na shoka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.