2018-05-21 15:14:00

Miaka 315 ya maisha na utume wa Shirika la Roho Mtakatifu!


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Sherehe ya Pentekoste, Jumapili, tarehe 20 Mei 2018 amekazia dhamana na nafasi ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa, kuwa ni nguvu inayoleta mabadiliko katika Kanisa. Roho Mtakatifu anawawezesha waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, sanjari na kuendelea kulipyaisha Kanisa katika maisha na utume wake!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, ameadhimisha Sherehe ya Pentekoste kwa jumuiya na Wamisionari wa Roho Mtakatifu, kwenye Kikanisa cha Watawa Wamisionari wa Comboni, mjini Roma, kama kumbu kumbu ya kuanzishwa kwa Shirika na Padre Claude Poullart des Places, huko Ufaransa kunako mwaka 1703. Hiki kilikuwa ni kikundi cha Waseminari waliojiaminisha na kujiweka wakfu chini ya ulinzi na tunza ya Roho Mtakatifu na kwa msaada wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili huduma kwa Kanisa, hususan katika maeneo na mazingira tete na hatarishi; bila kusahau uinjishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Shirika la Roho Mtakatifu linapoadhimisha Sherehe ya Pentekoste, linamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameliwezesha kutoka kimasomaso kwenye kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu katika nchi 62 duniani, zinazohudumiwa na wanashirika 2,600 kadiri ya takwimu zilizotolewa na Padre John Fogarty, Mkuu wa Shirika la Roho Mtakatifu, mwanzoni kabisa mwa Ibada, wakati wa kumkaribisha Kardinali Parolin, kuongoza Ibada ya Misa Takatifu. Kwa namna ya pekee, familia ya Mungu imesali na kuwaombea Wamisionari wa Roho Mtakatifu wanaotekeleza dhamana na utume wao katika mazingira magumu na hatarishi.

Wamisionari wa Roho Mtakatifu wanafanya utume wao huko: Sudan ya Kusini, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ili wasikate tamaa kutokana na magumu na changamoto wanazokabiliana nazo, bali kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili kweli siku moja, amani ya kweli iweze kupatikana na kutawala katika akili na nyoyo za watu ili kuzima kiu ya maendeleo endelevu ya binadamu!

Kardinali Parolin katika mahubiri yake, amefanya rejea ya maana halisi ya Sherehe ya Pentekoste katika maisha na utume wa Kanisa. Roho Mtakatifu ni Nafsi ya tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ndiye Roho wa Bwana ambaye ameujaza ulimwengu na kuviunganisha viumbe vyote ili kujua maana ya kila sauti! Huyu ndiye Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima; atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana: aliyenena kwa vinywa vya Manabii. Ndiye aliyewashukia Mitume pamoja na Bikira Maria wakapata ujasiri na nguvu ya kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu. Huu ukawa ni mwanzo mpya wa Sakramenti ya umoja na mshikamano dhidi ya utengano uliojionesha wakati wa ujenzi wa Mnara wa Babeli.

Kardinali Parolin, amekazia kwa namna ya pekee: umuhimu wa waamini kutembea katika mwanga wa Roho Mtakatifu kwa kumwachia nafasi ili aweze kuwaongoza na kuwapatia nguvu ya kuendelea kuwa waaminifu kwa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wanaifia dhambi na utu wa kale, kwa kuenenda katika Roho, kwani hawataweza kutimiza kamwe tamaa za mwili yaani: uasherati, uchafu, ufisadi, Ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, huzushi, husuda, ulevi, ulafi na mambo yanayofanana na hayo!

Kardinali Parolin, anasema, Mtume Paulo anawataka waamini kujikita kwa kumwilisha matunda ya Roho Mtakatifu katika maisha yao yaani: upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria! Roho Mtakatifu ameliwezesha Kanisa kutoka kimasomaso kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Roho Mtakatifu analisaidia Kanisa kufunua na kuambata ukweli, kwa kuyakimbia malimwengu ili kuambata neema na ukweli wa Mungu. Roho Mtakatifu ni Sakramenti ya umoja, upendo na mshikamano; ni chachu ya toba na wongofu wa ndani; imani na matumaini ya watu wa Mungu.

Roho Mtakatifu ndiye anayeliwezesha Kanisa kuishi na kutenda kadiri ya Injili;  kupenda kadiri ya vigezo vya Yesu, yaani hata kuthubutu kuwapenda adui na kusadaka maisha kwa ajili ya Injili na Kanisa la Kristo! Roho Mtakatifu amelipatia Kanisa nguvu ya kujenga Jumuiya ya Kimisionari inayotumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Huu ni mchakato wa kuwashirikisha watu wa Mungu, furaha inayobubujika kutoka katika Injili. Roho Mtakatifu analitakatifuza Kanisa ili kuachana na malimwengu, kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, changamoto pevu katika ulimwengu mamboleo.

Roho Mtakatifu ndiye anayeliongoza Kanisa kutangaza na kushuhudia Habari Njema kwa maskini, ili kukuza na kudumisha: uhuru na ukweli. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja kwa Kanisa kushirikisha upendo wa Kiinjili. Kanisa ni Mama, Mwalimu na Mtume, kumbe, waamini wanahamasishwa kufungua nyoyo zao kwa Roho Mtakatifu aweze kuwa na roho moja na moyo mmoja! Roho Mtakatifu awajalie waamini kufungua nyoyo zao; awafundishe na kuwaonesha njia ya kufuata katika maisha na utume wa Kanisa!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican alihitimisha Ibada ya Sherehe ya Pentekoste kwa kuzima Mshumaa wa Pasaka, ishara kwamba, shamrashamra za Fumbo la Pasaka, zimefikia ukomo, sasa ni wakati wa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika uhalisia wa maisha na utume wa Kanisa. Ibada hii imeadhimishwa katika lugha mbali mbali kuonesha utajiri wa karama na maisha ya Kanisa. Imehudhuriwa pia na Kardinali Francis Arinze, tunda la maisha na utume wa Wamisionari wa Roho Mtakatifu nchini Nigeria.

Mabalozi wafuatao wameshiriki katika Ibada ya Sherehe ya Pentekoste: Mama Emma Madigan, Balozi wa Ireland mjini Vatican, Bwana Godwin George Umo, Balozi wa Nigeria mjini Vatican, Bwana Car-Henri Guiteau, Balozi wa Haiti mjini Vatican pamoja na Bwana Michel Roy, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.