2018-05-19 10:13:00

Rais Patrice Talon wa Benin akutana na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 18 Mei 2018 amekutana na kuzungumza na Rais Patrice Talon wa Benin pamoja na ujumbe wake; na baadaye amebahatika pia kukutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Mazungumzo haya yamefanyika katika hali ya amani na utulivu kama sehemu ya mchakato wa kuimarisha Mkataba wa Cotonou uliotiwa sahihi kati ya Vatican na Benin hapo tarehe 21 Oktoba 2016. Viongozi hawa wawili wameridhishwa sana na ushirikiano uliopo kati ya Kanisa Katoliki na Serikali hasa katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo endelevu ya watu.

Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake, wamegusia pia hali halisi ya kijamii na kiuchumi ilivyo nchini Benin, lakini zaidi kwa kujikita katika masuala ya maendeleo endelevu ya binadamu; mapambano dhidi ya balaa la umaskini, mageuzi mbali mbali yanayoendelea kufanywa nchini Benin bila kusahau umuhimu wa majadiliano ya kidini kama njia ya kukuza na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu. Mwishoni mwa mazungumzo yao, Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake, wameyaangalia pia masuala ya kikanda na kimataifa, hususan changamoto zinazoendelea kujitokeza katika Ukanda huu, Barani Afrika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.