2018-05-19 13:41:00

Mwenyeheri Paulo VI & O. Romero kutangazwa watakatifu 14 Oktoba 2018


Baba Mtakatifu Francisko kwenye mkutano wa kawaida wa Baraza la Makardinali, Jumamosi, tarehe 19 Mei 2018 ametangaza kwamba, Mwenyeheri Paulo VI, pamoja na Mwenyeheri Askofu mkuu Oscar Arnulfo Romero Galdamez watatangazwa kuwa watakatifu hapo tarehe 14 Oktoba 2018 wakati wa maadhimisho wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana inayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Watakatifu wengine watarajiwa katika orodha hii ni pamoja na: Mwenyeheri Vincenzo Romano, Mwenyeheri Francesco Spinelli, Mwenyeheri Maria Katharina Kasper pamoja Mwenyeheri Nazaria Ignasia wa Theresa wa Yesu.

Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu amesema, ni waamini waliomtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa matendo yenye mvuto na mashiko. Mifano yao bora ya maisha, urafiki wa kuungana na Mwenyezi Mungu; umeweza kuliangazia Kanisa na Ulimwengu mwanga wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, mambo msingi katika mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko. Wamekuwa ni mifano bora ya kuigwa kama watoto wateule wa Mungu na kamwe hawakusita kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu.

Mwenyeheri Paulo VI, alitangazwa kuwa Mwenyeheri tarehe 19 Oktoba 2014 wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, atangazwe kuwa Mtakatifu katika kipindi cha Mwaka 2018, Mama Kanisa anapoendelea kujizatiti katika kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya familia, zinazofumbata Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Ni kiongozi wa Kanisa aliyesimamia vyema mchakato wa maadhimisho na utekelezaji wa maazimio ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Akawa ni kiongozi wa kwanza wa Kanisa kufanya hija za kichungaji nje ya Italia ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo. Katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro akatoa kipaumbele cha pekee kwa majadiliano ya kidini na kiekumene kama njia ya kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika haki, amani na maridhiano. Mwenyeheri Paulo VI alizaliwa tarehe 26 Septemba 1897 na kufariki dunia tarehe 6 Agosti 1978 kwenye Ikulu ndogo enzi hizo ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma.

Mwenyeheri Askofu mkuu Oscar Arnulfo Romero Galdamez, aliyezaliwa tarehe 15 Agosti 1917, huko El Salvador na kuuwawa kikatili kutokana na chuki za kidini kunako mwaka 1980. Alikuwa ni mchungaji mwema aliyejitahidi kujenga na kudumisha amani kwa nguvu ya upendo, kashuhudia imani kwa Kristo na Kanisa lake kiasi hata cha kuyamimina maisha yake. Mwenyezi Mungu anaendelea kuwakumbuka watu wake na kwa sasa Baba Mtakatifu Francisko ameridhia kwamba, atangazwe kuwa Mtakatifu. Hii inatokana hasa na ushuhuda wake wa kuwalinda, kuwatetea na kuwahudimia maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, kiasi hata utu na heshima yao kama binadamu vikawekwa rehani. Mwenyeheri Romero alitekeleza dhamana na wajibu wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kama Askofu, mintarafu Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Wengine watakaotangazwa pia kuwa watakatifu katika kipindi cha mwaka 2018 ni Mwenyeheri Vincenzo Romano, Padre wa Jimbo nchini Italia, aliyezaliwa kunako mwaka 1751 na kufariki dunia, tarehe 20 Desemba 1831. Katika orodha hii, wamo pia: Mwenyeheri Francesco Spinelli, Padre wa Jimbo na muasisi wa Shirika la Masista Waabuduo Ekaristi Takatifu, aliyezaliwa kunako mwaka 1853 na kufariki dunia mwaka 1913. Mwenyeheri Maria Katharina Kasper, muasisi wa Shirika la Watawa fukara wa Yesu, alizaliwa mwaka 1820 huko Ujerumani na kufariki dunia mwaka 1898. Na mwishoni ni Mwenyeheri Nazaria Ignasia wa Theresa wa Yesu, Mwanzilishi wa Shirika la Watawa Wamisionari wa Msalaba wa Kanisa “Suore Misioneras Cruzadas de la Iglesia.”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.