2018-05-19 09:04:00

Baraza la Makanisa Ulimwenguni: Ujumbe wa Pentekoste kwa Mwaka 2018


Baraza la Makanisa Ulimwenguni linapenda kuwatakia Wakristo wote heri na baraka kwa Sherehe ya Pentekoste, ambayo inaadhimishwa tarehe 20 Mei 2018 siku muhimu sana ya kuzaliwa kwa Kanisa, linalotoka katika hofu na mashaka, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 2013, wakati wa maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, kulizinduliwa Hija ya Haki na Amani kama njia ya kukabiliana na ukosefu wa haki, kupanuka kwa misigano na migongano ya kijamii; vita, ghasia na mapigano ya mara kwa mara sehemu mbali mbali za dunia.

Wajumbe wa Hija ya Haki na Amani wamejitahidi kutembelea sehemu mbali mbali za dunia, ili kujionea hali halisi. Ziara hizi pamoja na mambo mengine, zimeendelea kuwa ni kielelezo cha mshikamano na waathirika wa ukosefu wa haki, vita na ghasia sehemu mbali mbali za dunia. Kipindi hiki cha Pentekoste ni muda muafaka wa kushirikishana matunda ya ushuhuda wa mshikamano uliowezeshwa na Roho Mtakatifu.

Baadhi ya wajumbe, wamekutana na kuzungumza na wanawake walionyanyasika na kudhalilishwa utu na heshima yao kutokana na msimamo wao wa kutaka kujenga na kudumisha maisha bora zaidi ya kijamii. Wajumbe, wameendelea kuhimiza umuhimu wa familia ya Mungu kushiriki kikamilifu katika mchakato wa shughuli za kisiasa, ili kujenga utamaduni na sanaa ya kusikilizana katika ukweli na uwazi; ili kukuza na kudumisha amani na maridhiano kati ya watu. Pale ambapo bado mtutu wa bunduki unaendelea kurindima, juhudi zinaendelea kufanywa ili kuwekeana Mkataba wa Amani.

Wajumbe wa Hija ya Haki na Amani, tangu kunako mwaka 2016 wametembelea nchi kama Palestina na Israeli; Nigeria, Sudan ya Kusini na Colombia, nchi ambazo bado zinateseka kutokana na vita, ili kuimarisha matumaini ya amani kama zawadi kutoka kwa Kristo Yesu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Nchini Colombia, familia ya Mungu bado inaendelea kujibidisha kutekeleza mkataba wa amani kati ya Serikali na Kikundi cha wapiganaji wa msituni, FARC-EP. Changamoto kubwa kwa wakati huu ni ujenzi wa msingi wa haki na amani; kwa kusikilizana, kushirikiana na kuwasaidia waathirika kama alama ya maisha mapya.

Wananchi wa Colombia wanaamini kwa dhati kabisa kwamba, Mwenyezi Mungu yupo kati pamoja nao na kwamba, ataendelea kuwakirimia nguvu, kurutubisha matumaini kwa waathirika ili majadiliano yanayoendelea huko Havana yaweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani amani ya kweli, ili kuondokana na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia pamoja na vitisho kwa viongozi. Katika changamoto za kujenga na kudumisha amani, waamini wakumbuke kwamba, Roho Mtakatifu atawasaidia na kuwafariji kwani lengo ili kukuza na kudumisha Injili ya uhai, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu dhidi ya utamaduni wa kifo.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, mwaka huu, 2018 linaadhimisha Jubilei ya kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwake. Linapenda kuchukua fursa hii kuwakumbuka na kuwaombea wananchi wa Korea, Palestina na Siria, ambao bado wanaendelea kuteseka kutokana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Sherehe ya Pentekoste, iwe ni fursa kwa waamini kuungama na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo; ili kukuza na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Roho Mtakatifu awasaidie viongozi kutoka Nicaragua, Venezuela na Brazil kujikita katika mchakato wa haki, amani na maridhiano. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, mwishoni mwa ujumbe wake wa Sherehe ya Pentekoste kwa mwaka 2018 linamwomba Kristo Mfufuka anayewajalia waja wake maisha mapya, awawezeshe kusimama kidete kutafuta, kulinda na kudumisha haki, amani na maridhiano, ili wote waweze kuwa na roho moja na moyo mmoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.