Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Makala

Askofu Kassala: familia ni chemchemi ya malezi na majiundo ya kiutu

Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki Geita anasema, familia ni kitovu cha malezi na majiundo ya kiutu, maisha ya kiroho na kitamaduni. - AP

19/05/2018 14:10

Familia ya Kikristo ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya haki, amani, upendo na mshikamano. Ni kitalu cha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kijamii na kitamaduni na ni jukwaa la uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Katika Agano Jipya, Kristo Yesu anatoa kipaumbele cha pekee kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kama njia ya kupyaisha na kutimiza mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Yesu aliwarejeshea wanandoa ile furaha ya asili, akawaonea huruma wazazi waliokuwa wanahuzunika kwa magonjwa na vifo vya watoto wao; akakazia Uso wa huruma ya Mungu katika maisha ya kifamilia.

Mababa wa Kanisa wanakaza kusema, maisha ya ndoa na familia ni mahali pa kuendeleza Injili ya uhai; kwa wazazi kuwajibika barabara kwa malezi na makuzi ya watoto wao; pamoja na wao wenyewe kusaidiana katika mchakato wa utakatifu wa maisha. Upendo ni kanuni msingi katika maisha ya kijamii. Yote haya ni mambo msingi yanayofumbata furaha ya upendo ndani ya familia, kama anavyosimulia Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia.”

Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki Geita, Tanzania anasema, familia ni vitalu na chemchemi ya miito mitakatifu ya upadre, utawa na ndoa. Familia zina wajibu na dhamana ya kuhakikisha kwamba, kweli familia inakuwa ni mahali pa kutakatifuzana; mahali pa wakuwajenga na kuwafunda mashuhuda na vyombo vya uinjilishaji, huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya watu. Familia ni shule ya kwanza ya malezi ya tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii. Kumbe, wazazi na walezi wanapaswa kutekeleza vyema dhamana hii kwa unyofu na uadilifu mkubwa. Familia ya Mungu nchini Tanzania katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, inapaswa kuwekeza zaidi na zaidi katika malezi na majiundo ya tunu msingi za kifamilia, ili kweli familia ziweze kuwa ni chachu ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya chachu ya Injili na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Wazazi watambue kwamba, wao ni wahudumu wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaozinyemelea familia nyingi duniani!

Askofu Kassala anasikitika kusema, kuna baadhi ya wakleri, watawa na hata watu wa ndoa wanaoamua kuachana na mpango wa maisha na wito wao wa awali na “kuingia mitini”, matukio kama haya yawe ni changamoto kwa familia ya Mungu nchini Tanzania kujikita zaidi katika malezi na makuzi ya watoto kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu katika ujumla wake. Askofu Flavian Matindi Kassala, mtaalam katika utume na maisha ya vijana anakaza kusema, mitikiso katika maisha ya kipadre, kitawa na ndoa ni mambo ya kawaida, jambo la msingi ni kwa wahusika kutambua changamoto zilizoko mbele yao na kuzifanyia kazi kwa njia ya sala, tafakari, mafungo ya kiroho na ushauri kutoka kwa wataalam, lakini zaidi ni mwaliko wa kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuambata neema na baraka ili kujikita katika mchakato wa utakatifu wa maisha. Wazazi wawe mstari wa mbele kuwalinda watoto wao dhidi ya nyanyaso za kijinsia zinazoweza kuwasababishia majanga katika malezi na makuzi yao. Kanuni maadili, utu wema na sheria za nchi zizingatiwe ili kuwapatia watoto malezi na makuzi bora, ili kuwajengea imani, matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

19/05/2018 14:10