2018-05-18 08:54:00

Papa Francisko: Jengeni Kanisa la Kinabii na Huduma nchini Chile!


Baba Mtakatifu, Francisko kuanzia tarehe 15-17 Mei 2018 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Chile kwa faragha kuhusu kashfa ya nyanyaso za kijinsia, kwa kufuata mchakato wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Kimekuwa ni kipindi cha kuchunguza dhamiri ili kupambananua sababu msingi zilizopelekea kuibuka kwa vitendo vya nyanyaso za kijinsia nchini humo. Baba Mtakatifu amewashirikisha Maaskofu taarifa iliyotolewa na uchunguzi uliofanywa na Askofu mkuu Charles Jude Scicluna hivi karibuni. Lengo kuu limekuwa ni kurejesha tena imani na matumaini ya watu wa Mungu kwa Kanisa nchini Chile.

Taarifa iliyotolewa na Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican inafafanua kwamba, Alhamisi, tarehe 17 Mei 2018 majira ya jioni, Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha kikao cha nne na Baraza la Maaskofu Katoliki Chile! Maaskofu 34 wamehudhuria na kushiriki kikamilifu katika mkutano huu ambao umesimikwa katika umoja na udugu; ili kuweza kukabiliana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia kwa ari na moyo mkuu.

Baada ya mkutano huu, Baba Mtakatifu amempatia kila Askofu barua ambamo anawashukuru kwa kukubali na kutikia mwaliko wake wa kufanya mang’amuzi ya pamoja dhidi ya matukio mabaya ambayo yameharibu umoja wa Kanisa pamoja na kudhohofisha utume wa Kanisa nchini Chile katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Katika mwanga wa matendo haya ya kusikitisha yaani kashfa ya nyanyaso za kijinsia; uchu wa madaraka na dhamiri, anasema Baba Mtakatifu wameweza kuzama zaidi na kuona uzito wa vitendo hivi na madhara yake hasa kwa waathirika.

Baadhi yao anasema, alipata bahati ya kuwaomba msamaha kwa niaba ya Kanisa na kwamba, Maaskofu katika utashi na umoja wao wamepania kurekebisha madhara yaliyojitokeza. Baba Mtakatifu anawashukuru kwa majitoleo yao, ambayo kila mmoja wao, ameonesha ile nia ya kujiunga na kushirikiana na wote katika mchakato wa mabadiliko na suluhu ya kudumu, itakayoanza kutekelezwa hivi karibuni kwa kuzingatia malengo ya muda mfupi, muda wa kati na yale ya muda mrefu; mambo msingi katika kuhakikisha kwamba haki inatendeka na umoja wa Kanisa unadumishwa. Mwishoni mwa barua yake, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, baada ya siku hizi za sala na tafakari, anapenda kuwaalika Maaskofu kuendeleza mchakato wa ujenzi wa Kanisa la kinabii, linalotambua umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza katika huduma kwa Kristo Yesu anayeteseka kwa baa la njaa, kama mfungwa, mkimbizi na anayenyanyasika! Amewaomba Maaskofu Katoliki wa Chile kumkumbuka katika sala zao ili aweze kutekeleza vyema maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.