2018-05-17 07:00:00

Sherehe ya Pentekoste: Utatu Mtakatifu unafunuliwa kikamilifu!


Siku hamsini baada ya Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo na siku kumi baada ya kupaa kwake Mama Kanisa anatualika kusherehekea sherehe ya Pentekoste. Neno Pentekoste lina asili yake katika lugha ya kiyunani πεντηκοστή (likitamkwa “Pentekostee”) ambalo linamaanisha siku ya hamsini. Sherehe ya Pentekoste ina asili yake katika dini ya kiyahudi ambapo walifanya shukrani ya mazao kwa Mungu siku hamsini baada ya pasaka ya kiyahudi (Rej Kut 23:16; Law 23:24, 42- 43). Sherehe hii iliyojulikana kwa jina la “Shavout” au sherehe ya majuma au vibanda ilikuwa pia ni kumbukumbu ya tukio la kupewa Amri Kumi (10) za Mungu mlimani Sinai. Hii ilikuwa ni sherehe wakati wa kipindi cha kuchepuka, sherehe ambayo iliashiria mwanzo mpya wa maisha. Majira ya baridi yanayotangulia kipindi hiki yana tabia ya kuonesha ufu. Mimea mingi hupoteza majani yake mithili ya mmea unaokauka. Lakini majira ya mchepuke huleta matumaini mapya na mwanzo mpya.

Kwetu sisi Wakristo sherehe hili ni adhimisho la Roho Mtakatifu kuwashukia Mitume kama utimilifu wa ahadi ya Baba, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka na huo ni mwanzo wa maisha na utume wa Kanisa, jamii mpya ya wanadamu inayoongozwa katika Sheria ya Kristo. Sheria hiyo inawezeshwa katika Roho Mtakatifu. Mtakatifu Ireneo wa Lyon alisema: “kama vile isivyowezekana kwa unga kufinyangwa na kufanya mkate bila tone la maji ndivyo isivyowezekana kwetu sisi kufanyika upya katika Kristo bila uwepo wa Roho Mtakatifu”. Jumuiya mpya ya mwanadamu inayoundwa na Kristo inawezeshwa na Roho Mtakatifu: “Waipeleka Roho yako, Ee Bwana, nawe waufanya upya uso wa nchi”. Hivyo adhimisho hili kila mwaka kama ilivyo kwa Wayahudi linapaswa kuwa chemchem mpya na chipuko ya maisha mapya ya kikristo.

Leo hii tunauona ujio huu wa Roho Mtakatifu katika Kanisa ambalo limejengwa kwa msingi wa mitume. Msingi huo ni Kristo mwenyewe ambaye ni Jiwe kuu la pembeni. Matendo makuu ya Mungu yamefunuliwa kwetu katika nafsi ya Kristo. Ni Yeye ambaye ametuondoa utumwani na kutupatia mfano wa maisha mapya. Baada ya kupaa kwake mbinguni alituagiza kuyashuhudia matendo hayo. “Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu, wakisema matendo makuu ya Mungu, Aleluya! Matendo haya yalikuwa yananenwa kwa namna ya maisha. Maisha yake aliyejazwa Roho Mtakatifu yanatufunulia matendo makuu. Hapa tunauona wito wa utakatifu ambao Kristo anatupatia, wito ambao tunautimiza vema tunapounganika na Roho Mtakatifu. Yeye anatuelekeza mpango wa Mungu uliofunuliwa kwetu katika Kristo na kutupatia ujasiri wa utekelezaji wake. Muunganiko huu thabiti na Mungu ndiyo utakatifu wa maisha ya kikristo. Watakatifu ni rafiki za Mungu; wale ambao wameunganika naye kuyatenda mambo yake makuu.

Roho Mtakatifu anapotupatia utakatifu huo ambao unatokana na upya wa maisha tuupatao katika Kristo anatusaidia pia kujua maana ya kila sauti: “Roho ya Bwana imeujaza ulimwengu, nayo inaviunganisha viumbe vyote, hujua maana ya kila sauti, Aleluya! Katika somo la kwanza muujiza huo na utendaji huo wa Roho Mtakatifu unaonekana kwani watu walielewa kila kitu katika lugha yao.

Watu katika Yerusalemu walistaajabishwa kwa kusema: “Inakuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo?” Maana yake nini maneno haya? Tunaweza kuyaelewa kwa tafakari mbalimbali kama ile hali ya kupata utambuzi wa kimungu na kuelewa maana na faida ya karama mbalimbali katikati ya jamii ya mwanadamu. Utambuzi huu unaeleweka kwa kila mmoja katika muktadha wake kwa ajili ya kukidhi haja yake. Inaelezea utajiri wa karama tofauti tunazojaliwa na mwenyezi Mungu katika kutajirishana. Pato hili ni muhimu kwetu kwanza kwa kujali na kuheshimu kila mmoja kwa nafasi yake kwa ajili ya faida ya wote na pili kwa kutupatia hamasa ya kuitendea haki na kuigawa karama tuliyopewa kwa ajili ya faida wa wengine. Hii ni kwa sababu “pana tofauti ya karama; bali Roho ni yeye yule”.

Jumuisho ya hayo yote tunayoyapata hapo juu kutoka kwa Roho Mtakatifu huonekana katika kutufanya kuwa wamoja. Tunda la Roho Mtakatifu ni kutufanya kuwa ndugu. Sakramenti ya Ubatizo ambayo inatuingiza katika kundi la wana warithi wa Mungu huwezeshwa na Roho Mtakatifu. “Hawezi mtu kusema Yesu ni Bwana isipokuwa katika Roho Mtakatifu… kukiri huko kwa imani kunawezekana tu katika Roho Mtakatifu… kwa nguvu ya ubatizo wetu, Sakramenti ya kwanza ya imani, uzima ambao una chemchemi yake katika Baba, na ambao umetolewa kwetu katika Mwana; unashirikishwa kwa ndani kabisa katika nafsi ya mtu na Roho Mtakatifu katika Kanisa” (Katekisimu ya Kanisa Katoliki, namba 683). Roho Mtakatifu anapotuunganisha na Mungu na hivyo kutufanya kuwa wana warithi wa Mungu anatuunganisha sisi kwa sisi. Undugu wetu uliopo katika Kristo unapata msingi wake katika Roho Mtakatifu.

Hivyo, leo pia hatuna budi kushehekea umoja wetu ambao kwa njia yake tutaendelea kuheshimiana, kujaliana, kusaidiana na kuimarisha mahusiano ya kiutu kati yetu. Tunapoishi katikati ya jamii ambayo inabariki na kushabikia utengano baina ya mtu na mtu na uharibifu mkubwa wa haiba na utu wa mwanadamu, changamoto inawekwa kwetu sisi Wakristo; sisi ambao kwa ubatizo wetu tumempokea Roho Mtakatifu na kwa namna ya pekee, tumeimarishwa kwa mapaji yake saba wakati wa Sakramenti ya Kipaimara. Changamoto hiyo ni kudhihirisha upya wa maisha tulioupata, upya ambao umetufanya kuwa rafiki wa Mungu kwa kutenda matendo yake na hivyo kuwa wamoja katika Kristo. Itakuwa ni sikitiko kwa jamii ya mwanadamu na ubinadamu kwa ujumla tutakapoififisha sauti ya Roho Mtakatifu.

Mara nyingi tunaelemewa sana na mielekeo ya dunia mamboleo na kumweka chemba Roho Mtakatifu. Mara ngapi tunashindwa kuonesha upendo, huruma, kusaidiana na kusameheana ndani ya familia zetu? Je, matendo hayo hurandana na matendo makuu ya Mungu? Mara ngapi tunafurahia au kuhusika katika dhuluma kati ya jamii moja au nyingine? Familia moja na nyingine? Imani moja na nyingine? Kwa hakika haya si matendo makuu ya Mungu. Kama tunafanyika kuwa watoto wa Mungu, vinasaba vyetu vinapaswa kububujisha yale yatokaye kwake kwa njia ya Kristo tukiwezeshwa na Roho Mtakatifu. Kristo katika Hekima yake ya kimungu hakututuma twende kichwa kichwa katika utume wa kuwa mashuhuda wake bali alituahidia Roho Mtakatifu aliye nguvu, mwanga, mtakasaji na anayetukumbusha kila mara. Tuifungue mioyo yetu ili kuisikiliza sauti yake na hivyo kuwa kweli mashuhuda wa Habari njema ya Wokovu kwa mwanadamu.

Mimi ni Padre Joseph Peter Mosha.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.