2018-05-17 17:00:00

Dr. Abdallah Saleh Possi awasilisha hati za utambulisho mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 17 Mei 2018 amepokea hati za utambulisho kutoka kwa Mabalozi wasio wakazi wanaoziwakilisha nchi zao mjini Vatican. Balozi hawa wanatoka: Tanzania, Lesotho, Pakistan, Mongolia, Denmark, Ethiopia na Finland. Dr. Abdallah Saleh Possi, Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani ambaye pia ni Balozi wa Tanzania mjini Vatican, tarehe 17 Mei 2018 amewasilisha hati za utambulisho kwa Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Kabla ya kuteuliwa na Rais John Pombe Magufuli kuwa ni Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani hapo tarehe 19 Januari 2018, Dr. Possi alikuwa Mbunge na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na alikuwa akijishughulisha zaidi na walemavu! Amewahi kufundisha Chuo Kikuu cha Dodoma; Aliwahi kuwa Wakili kwenye Mahakama kuu ya Tanzania na mhadhiri msaidizi kwenye Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Dr. Abdallah Saleh Possi alizaliwa tarehe 25 Agosti 1979. Baada ya masomo yake ya awali na sekondari, alibahatika kupata shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye kunako mwaka 2014 akajipatia shahada ya uzamivu kutoka huko Friedrich-Alexander kwenye Chuo Kikuu cha Erlangen-Nürnberg kilichoko nchini Ujerumani. Jioni, Balozi Possi amehudhuria kwenye utetezi wa shahada ya uzamivu katika sheria kanuni za Kanisa, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, kilichoko mjini Roma, uliofanywa kwa ufundi mkubwa na Padre Celestine Richard Nyanda kutoka Jimbo Kuu la Mwanza.

Balozi Retšelisitsoe Calvin Masenyetse kutoka Lesotho, alizaliwa tarehe 4 Mei 1970, ameoa na amebahatika kupata watoto wawili. Kwa taaluma ni mwanasheria mwenye shahada ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Kitaifa Lesotho. Amewahi kuwa Katibu mkuu Wizara ya Sheria; Mbunge na Mwenyekiti wa Tume Mageuzi ya Sheria na Usalama wa raia na mwaka 2017 akateuliwa kuwa Balozi wa Lesotho nchini Ujerumani.

Balozi Ali Sulaiman MOHAMMED kutoka Ethiopia, alizaliwa kunako mwaka 1952 ameoa na kitaaluma ni mwanasheria aliyebobea. Amewahi kuwa Jaji wa Mahakama kuu na kati ya mwaka 2001 hadi mwaka 2005 alikuwa Naibu Waziri wa Sheria. Baadaye aliteulia kuwa Kamishna wa Maadili na Tume ya Kuzuia Rushwa na Mwaka 2017 akateuliwa kuwa Balozi wa Ethiopia nchini Ufaransa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.