2018-05-16 15:44:00

Sherehe ya Pentekoste, kuzaliwa kwa Kanisa!


Masomo yetu ya leo yanatupa mwanga juu ya habari ya Roho Mtakatifu. Lengo la Mwinjili Luka kuandika Injili na kitabu cha Matendo ya Mitume ni kuonesha kwa ujumla hali halisi ya Ukristo. Pendo la Mungu linalookoa ni kwa kila mmoja, kila mahali na kwa kila kizazi. Chombo cha utendaji katika kuenenda huko ni Roho Mtakatifu. Mwinjili Luka anaweka wazi jambo hili. Angalia Injili ya leo - habari juu ya nguvu ya Roho Mtakatifu. Mwinjili Luka anaelewa wazi kuwa huu ndio mwanzo wa kanisa na wajibu wake katika kutangaza habari njema kwa njia na nguvu ya Roho Mtakatifu.

Katika somo la kwanza Mtakatifu Petro anaonesha wazi Roho huyu anatolewa kwa sababu ya kazi ya wokovu ya Yesu Kristo - Mdo. 2: 32-33 - Yesu huyo, Mungu alimfufua na sisi sote tu mashahdi wake. Basi yeye akiisha kupandishwa hata mkono wa kuume wa Mungu na kupokea kwa Baba ile ahadi ya Roho Mtakatifu, amekimwaga kitu hiki mnachokiona sasa na kusikia. Roho Mtakatifu analeta pendo la wokovu wa Kristo kwetu sisi. Ndiye Roho huyu tunayepaswa kumpokea na kutenda naye kazi kama wakristo na katika maisha yetu ya kikristo kila siku. Kinyume chake ipo hatari ya kuishi roho zetu na si Roho wa Mungu aliyetumwa kwetu toka pendo la Mungu Baba na mwanae Kristo. Kwetu sisi tunaoamini, tunaweza kusema hivyo na kushuhudia kwa sababu ya uwepo wa huyo roho. Roho huyo anafanya kazi ndani mwako.

Katika somo la pili Mtakatifu Paulo anasema hakuna awezaye kumwita Bwana isipokuwa katika Roho Mtakatifu. Ukristo wako ni mpango wa Roho katika kueneza ufalme. Pentekoste imetokea kwako. Roho Mtakatifu ana nafasi gani katika maisha yako au unamwelewaje roho mtakatifu? je unatambua uwepo wake? Je, wewe unaye Roho Mtakatifu au unaishi maisha na Roho Mtakatifu? Roho mtakatifu ni mtendaji.

Katika barua ya Mtume Paulo kwa wakorintho twaona tabia mbili za kazi ya Roho Mtakatifu. Ugawaji wa mapaji maalumu kwa waamini na zaidi tukiendelea Paulo anaorodhesha mapaji hayo. Mengine ni ya pekee kabisa kama kuongea kwa ndimi, lakini mengine ni ya kawaida ya kutekeleza katika maisha yetu ya kikristo ya kila siku kama kufundisha, kusaidia wengine kwa hali na mali na kuongoza wengine. Muhimu hapa kila tufanyacho tukisaidiana katika kweli na haki huonesha nguvu ya Roho Mtakatifu ikifanya kazi ndani yetu ni zawadi yake. Na namna ya kutambua kuwa, kama tumepokea zawadi hii au tunaishi zawadi hii ni kama tu inawasaidia wengine au kama asemavyo mtume Paulo kwa ajili ya faidi ya wote. Zawadi za Roho Mtakatifu ni kwa wale wote waaminio. Ndo maana mtume Paulo anasema kuwa zawadi kubwa kabisa ya huyo roho ni UPENDO.

Tabia ya pili ya Roho Mtakatifu ni nguvu ya kuunganisha. Roho huyo huumba upya katika roho moja. Sote tumebatizwa katika mwili mmoja. Wakati kila mkristo amepewa karama yake na roho huyo, sote tumekuwa mwili mmoja katika Kristo. Roho mtakatifu anatuunganisha sote. Kwa namna ya pekee, Injili ya leo yaunganisha uwepo wa Roho Mtakatifu na Msamaha wa dhambi. Roho Mtakatifu anahusishwa moja kwa moja na msamaha wa dhambi. Mitume wanapewa uwezo wa kusamehe dhambi. Lakini pia kwa namna ya pekee kila wakati ambapo sisi tunasameheana kati yetu tunatenda hilo kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

Ndugu mpendwa imani yako kwa Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu ni zawadi ya utumishi hata kama ni ndogo kiasi gani. Umoja wako na wengine, uwezo/utayari wako wa kusema na kusamehe kwa yule aliyekosea yote haya ni alama ya uwepo wa Roho anayetenda kazi ndani yako. Nenda kafanye hayo/sote tukatende hayo na Roho Mtakatifu ataonekana kati yetu. Huyo Roho si hewa au maneno matupu. Waraka kwa Wagalatia 5:22...... unatupatia dokezo linalotusaidia kuangalia kama kweli ndani au kati yetu yupo huyo roho wa Mungu - matokeo ya Roho:  Roho Mtakatifu huonekanaje? mkiongozwa na Roho hamkai chini ya sheria. Matendo ya mwili yanatambulikana wazi; ndiyo haya; uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, ucheza mazingaombwe, uadui, ugomvi, kijicho, hasira, ubinafsi, utengano, mafarakano, wivu, ulevi, ulafi na mengineyo kama hayo. …. Lakini matokeo ya Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, hisani, ukarimu, upole, kiasi. Hakuna sheria inayopinga hayo.

Tunaomba:

  1. Hekima - uwezo wa kupambanua kwa njia ya akili mema na mabaya, ukweli na uongo. Ni kutoa hukumu kadiri ya sheria ya Mungu.
  2. Nguvu - kushinda magumu au kuvumilia mateso kwa nguvu na uwezo toka kwa Mungu.
  3. Shauri – ili nishike njia nzuri.
  4. Akili - kutoa kweli kwa muono wa kina na kupenya kwenye ukweli wa Mungu.
  5. Elimu - kuamua kwa usahihi juu ya kweli za imani kadiri ya chimbuko halisi na kanuni za kweli zinazofumuliwa.
  6. Ibada - kumwona Mungu kuwa Baba wa wote.
  7. Uchaji wa Mungu - usikivu

Tumsifu Yesu Kristo.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.