2018-05-16 08:40:00

Papa Francisko ni zawadi kwa Makanisa katika majadiliano ya kiekumene


Uwepo na ushiriki mkamilifu wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni ni ushuhuda wa zawadi ya Mungu kwa Makanisa. Hili ni tukio muhimu sana katika maisha na utume wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika jitihada za mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika huduma na ushirikiano, ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.

Haya yamesemwa na Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwengu, Jumanne, tarehe 15 Mei 2018 wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Vatican kuhusiana na hija ya kiekumene ya Baba Mtakatifu Francisko mjini Geneva, huko nchini Uswiss hapo tarehe 21 Juni 2018. Hija hii ya kiekumene inaongozwa na kauli mbiu “Kutembea, Kusali na Kushirikiana” muhtasari wa dhamana na malengo makuu ya majadiliano ya kiekumene kwa wakati huu! Majadiliano ya kiekumene ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha amani, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia!

Jubilei ya Miaka 70 ya uwepo na utume wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni ni muda muafaka wa kumshukuru Mungu kwa umoja, mshikamano na mafungamano ya Makanisa duniani. Hili ni tukio ambalo litaendelea kuboresha mahusiano kati ya Makanisa katika ngazi mbali mbali. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linamshukuru kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Francisko kwa kukubali mwaliko ili kushiriki katika tukio hili muhimu kama kilele cha maadhimisho haya hapo tarehe 21 Juni 2018 huko Geneva nchini Uswiss. Maadhimisho haya ni fursa ya kupanua wigo wa Makanisa na waamini wake; ni watakati wa kuwa na mwono mpya zaidi katika maisha na utume wa Makanisa na kwamba, kwa njia ya imani, wakristo wakiwa wameungana wanaweza kutenda mambo makubwa zaidi!

Akizungumza kwa niaba ya Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo, Monsinyo Andrzej Choromanski, Afisa mwandamizi kutoka Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo na mjumbe mshauri wa Kamati ya Imani na Taratibu ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni amesema, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kushiriki tukio hili muhimu kama alama ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika kipindi cha miaka 70 iliyopita.  

Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake, anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa majadiliano ya kiekumene, ili Makanisa yaweze kutembea yakiwa yameshikamana; yanasali na kushirikiana katika huduma makini kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Kanisa Katoliki limeendelea kutoa ufadhili kwa wanafunzi wanaotaka kuboresha majadiliano ya kiekumene kutoka sehemu mbali mbali za dunia kama mchango wake katika majadiliano ya kiekumene kwa vitendo

Kwa upande wake, Askofu Charles Morerod wa Jimbo Katoliki la Lausanne, Geneva na Fribourg anakaza kusema, katika kipindi cha miaka 70 iliyopita, kumekuwepo na maboresho makubwa ya majadiliano ya kiekumene miongoni mwa Makanisa. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuhakikisha kwamba, changamoto za majadiliano ya kiekumene zinavaliwa njuga na Makanisa yote katika umoja na utofauti wake, ili kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa walimwengu ili waweze kumwamini Kristo Yesu na Kanisa lake. Geneva ni mji mkuu wa kimataifa ambamo majadiliano katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu yanafanyika kutokana na ukweli kwamba, huu ni mji ambao ni makao makuu ya ofisi za Mashirika ya Kimataifa na Kikanda. Hata maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko, yatakuwa na chapa ya kiekumene, kielelezo cha Makanisa yanayosali.

Miaka 70 iliyopita yaani kunako mwaka 1948, Baraza la Makanisa Ulimwenguni lilianzishwa likiwa na Makanisa wanachama 147 na tangu wakati huo, zaidi ya Makanisa 200 yamejiunga na kuwa ni sehemu ya Baraza hili yakiwa na waamini zaidi ya milioni 560. Itakumbukwa kwamba, Kanisa Katoliki ni mjumbe mtazamaji wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Vatican imetoa ratiba elekezi ya hija ya kiekumene ya Baba Mtakatifu Francisko mjini Geneva, nchini Uswiss kama sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 70 tangu Baraza la Makanisa Ulimwengu lilipoanzishwa.

Hii itakuwa ni hija ya siku moja na itafanyika hapo tarehe 21 Juni 2018. Kati ya matukio makuu yanayotarajiwa kufanywa na Baba Mtakatifu ni pamoja na: Sala ya Kiekumene ambamo Baba Mtakatifu atatoa mahubiri;  kuzungumza na viongozi wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia; kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Palexpo na baadaye jioni kurejea tena mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko atakuwa ni kiongozi mkuu wa kwanza wa Kanisa Katoliki kutembelea Uswiss, tangu baada ya Mtakatifu Yohane Paulo II kutembelea nchini humo kunako mwaka 2004. Itakumbukwa kwamba, Mwenyeheri Paulo VI alitembelea Baraza la Makanisa Ulimwenguni kunako mwaka 1969 mara tu baada ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na kunako mwaka 1984 Mtakatifu Yohane Paulo II akakaribishwa tena mjini Geneva katika hija yake ya kiekumene.

Baba Mtakatifu atakapowasili atapata fursa ya kufanya mazungumzo ya faragha na Rais wa Shirikisho la Uswiss Bwana Alain Berset. Baba Mtakatifu atapata chakula cha mchana na viongozi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwenye Taasisi ya Kiekumene ya Bossey, iliyoko kilometa 25 nje kidogo ya mji wa Geneva. Uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu katika kilele cha kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kuungana, kushirikiana na kushikamana kwa pamoja katika kukabiliana na changamoto mamboleo katika: umoja, utume, haki na amani duniani.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni limeendelea kujizatiti katika kukuza na kudumisha umoja wa Makanisa kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Limeendelea kuratibu na kusimamia majadiliano ya kitaalimungu miongoni mwa Makanisa na matunda ya majadiliano haya yanaanza kuonekana. Kumekuwepo na maridhiano pamoja na matamko ya pamoja kuhusu: Ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi; Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Dhamana na Utume wa Kanisa kama chombo na shuhuda wa umoja, upendo na mshikamano wa dhati, ili walimwengu waweze kumwamini Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni limekuwa mstari wa mbele kusimamia na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake, kwa kutambua kwamba, mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baraza litaendelea kuwa mstari wa mbele kutetea haki msingi za binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Baraza limeendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini kwa kuwashirikisha viongozi wa dini na Makanisa mbali mbali duniani, lakini zaidi kwa kuwashirikisha vijana wa kizazi kipya, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na mshikamano kati ya watu wa Mataifa.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni limekuwa ni jukwaa makini la kushirikishana: utajiri, amana na tunu msingi za maisha ya Kiinjili na kiutu. Limeendelea kudumisha mapokeo ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo  sanjari na kudumisha uekumene wa maisha ya kiroho; uekumene wa damu, uekumene wa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali. Baraza limeendelea kujizatiti katika kukuza na kudumisha sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Tangu mwaka 1992, Baraza la Makanisa Ulimwenguni limeragibisha haki ya mazingira kwa kutambua kwamba, uchafuzi wa mazingira una maadhara makubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.