2018-05-16 10:49:00

Maaskofu Katoliki Congo Brazzaville wasema, hali ni tete sana!


Baraza la Maaskofu Katoliki Congo Brazzaville, hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa mwaka kwa kuchambua hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini mwao. Maaskofu wanasikitika kusema kwamba, saratani ya rushwa inaendelea kuwapekenya wananchi kwa kiasi kikubwa, wizi na ufisadi wa mali ya umma umepamba moto na kwamba, chama tawala na wapinzani, wamekuwa hawawezi kupikika chungu kimoja, kwani wanaangaliana kwa jicho la kengeza! Haya ni mambo ambayo yanaendelea kulididimiza taifa katika kinzani na mipasuko ya kisiasa, kijamii na kiuchumi na kwamba, waathirika wakuu ni wananchi wa kawaida kabisa!

Baraza la Maaskofu Katoliki Congo Brazzaville katika Waraka wake wa kichungaji linakiri kwamba, matatizo na changamoto zinazowakabili wananchi wao kwa wakati huu ni matunda ya mchakato wa kura ya maoni iliyobadilisha katiba, bila kuwashirikisha wanasiasa kutoka katika vyama vya upinzani, hali ambayo imedhohofisha sana mahusiano na mafungamano ya kijamii, kiasi kwamba, kwa sasa kuna mpasuko mkubwa wa kijamii unaoendelea kujionesha. Matumaini ya wananchi yanazidi kufifia kutokana na hali ngumu ya maisha, hali ambayo inatishia amani na usalama wa raia na mali zao.

Kura ya maoni iliyopigwa kunako mwaka 2015 ilimwezesha Rais Denis Sassou Nguesso kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwainia Urais katika kipindi cha mwaka 2016 na akafanikiwa kupata ushindi, licha ya upinzani mkubwa uliotolewa na wananchi pamoja na vyama vya upinzani. Maaskofu wanasikitika kusema, tangu mwaka 1998 Congo Brazzaville ilianza  kuteteleka kutokana na: kinzani, ghasia pamoja na mashambulizi ya kutumia silaha za moto. Licha ya mikataba ya makubaliano ya amani kutiwa sahihi kwa nyakati mbali mbali, lakini bado kuna mapigano ya chini kwa chini yanayoendelea kutokea, kiasi cha kuhatarisha ulinzi na amani nchini humo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Congo Brazzaville linakaza kusema, kuna haja ya kubainisha matatizo, changamoto na athari zake katika maisha, ustawi na maendeleo ya wananchi, ili wananchi wote kila mtu kadiri ya nafasi na uwezo wake, aweze kuwajibika barabara. Watu wanaendelea kufa kwa baa la njaa, umaskini na utapiamlo wa kutisha. Bei ya mafuta inaendelea kuporomoka kila kukicha! Lakini kushuka kwa bei ya mafuta wanasema Maaskofu si habari yenye mashiko kwani faida ya mafuta ambayo ilikusanywa kwa miaka iliyopita, imetoweka katika mazingira ya kutatanisha na matokeo yake deni kubwa la serikali linaendelea kuongezeka na kwamba, Serikali imekubali hata masharti ambayo ni hatari sana kwa usalama na maisha ya wananchi wa Congo Brazzaville.

Matokeo yake, serikali haina fedha ya kulipa mishahara ya wafanyakazi wake; huduma ya elimu, afya na miundo mbinu inaendelea kuporomoka kila kukicha. Gharama ya maisha inazidi kupanda lakini hali ya maisha inazidi kuporomoka! Bei ya bidhaa na huduma inaendelea kuongezeka, isipokuwa bei ya bia imebaki ile ile ya zamani jambo la kushangaza sana!. Baraza la Maaskofu Katoliki Congo Brazzaville linasema, umefika wakati kwa wanasiasa wa Chama tawala na wale wa upinzani kuanzisha mchakato wa majadiliano katika ukweli, usawa na haki ili kutafuta suluhu ya changamoto na matatizo yanayoikumba nchi yao.

Mdhibiti wa deni kimataifa hana budi kupitia tena deni la nchi na hatimaye, kutoa ushauri na mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Congo Brazzaville. Wananchi wote hawana budi kujifunga kibwebwe kupambana na saratani ya rushwa na ufisadi. Baraza la Maaskofu Katoliki Congo Brazzaville linaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuwasaidia wananchi wao kupata fedha iliyokwapuliwa kutoka katika mifuko ya maendeleo endelevu, ili iweze kutumika kwa ajili ya maboresho ya huduma kwa wananchi,

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.